Monday, May 14, 2012

Masalia ya Bernadeta yahamishiwa kanisa kuu


Na Albano Midelo
HATIMAYE waumini wote sasa wanaruhusiwa kugusa na kufanya maombezi kwenye masalia ya mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta Mbawala baada ya masalia hayo kuhifadhiwa ndani ya kanisa kuu la mtakatifu Mathias Kalemba mjini hapa.
Zoezi la kuyahamisha masalia hayo kutoka katika kanisa la Askofu mkuu uaskofuni jimbo kuu la Songea ambako yalihifadhiwa kwa muda na  kuyapeleka katika sehemu maalum ndani ya kanisa kuu la kiaskofu kulifanywa Jumapili hii na   Askofu mkuu wa jimbo kuu la Songea mhashamu Norbert Mtega.

Askofu mkuu Mtega alifanya zoezi hilo baada ya adhimisho takatifu la misa ya tatu kwenye kanisa kuu hilo ambapo waumini walijipanga kwenye mistari hadi ndani ya kanisa dogo la kiaskofu ambako mhashamu Mtega aliongoza waumini  kutoa heshima nakugusa sanduku la masalia ya mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta kisha waumini walianza kubeba sanduku hilo katika maandamano kurudi   ndani ya kanisa kuu.
Akizungumza mara baada ya zoezi la kuhamisha masalia hayo kukamilika na kuhifadhiwa katika  jengo maalumu ndani ya kanisa kuu,mhashamu Mtega alibainisha kuwa sasa waumini wote wanaruhusiwa kufika katika eneo hilo na kugusa  mahali yalipohifadhiwa masalia hayo pamoja na kufanya sala za maombezi kupitia mtumishi huyo waMungu.
“Sasa tumekwisha kuweka masalia ya mtumishi wa Mungu hapa kanisani hadharani,tangu sasa tutaanza kutoa heshima kwake na yeyote ambaye ataingia hapa kanisani anataka kusali katika masalia haya atakuja hapa wakati wowote ambapo tutaacha wazi ili muumini siku yeyote anaweza kugusa na kusali katika masalia ya Sr.Bernadeta Mbawala.
Askofu mkuu mtega katika nafasi hiyo amewashukuru waumini wa kanisa kuu hilo kujitolea kujenga eneo maalumu ndani ya kanisa kwa kutumia sadaka za waumini wenyewe kwa ajili ya kuhifadhi masalia ya mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta.
“Tangu sasa mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta Mbawala atakuwa nanyi ndani ya kanisa hili akiwaombea na kuweza kusali na kumutuza Mungu pamoja nanyi,atawaombea katika shida zenu zote yakiwemo mateso na magonjwa mbalimbali kupitia maombezi yake ‘’,alisema askofu mkuu Mtega. Uzinduzi wa mchakato wa kumtangaza  mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta Mbawala kuwa Mwenyeheri ulizinduliwa rasmi  na Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega katika kanisa kuu la kiaskofu la mjini Songea mapema mwaka huu.
Mwenyekiti wa parokia ya Songea John Komba alisema jengo hilo maalum la kuhifadhia masalia ya mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta Mbawala lililojengwa ndani ya kanisa kuu la mtakatifu Mathias Kalemba limegharimu shilingi milioni mbili ambazo ni sadaka za waumini pamoja na kazi za kujitolea hadi kukamilisha ujenzi huo kwa muda mfupi.
Padre Joseph Mgaya wa seminari kuu Peramiho msemaji wa mchakato huo amethibitisha masalia ya mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta Mbawala kuhamishiwa katika sehemu ya wazi ndani ya kanisa kuu la mtakatifu Mathias Kalemba na kusisitiza kuwa sasa waumini watakuwa na fursa nzuri ya kugusa na kufanya maombi.
“Siku ya Jumamosi yaani siku moja kabla ya kuhamisha masalia hayo toka kanisa dogo la uaskofuni ambako yalikuwa yamehifadhiwa kwa muda,baadhi ya wanakamati  wa mchakato tulifanya ukaguzi katika eneo ambalo kimejengwa kibanda maalum ndani ya kanisa tuliridhika na kuidhinisha masalia hayo kuwekwa hap kanisani mahali pa wazi’’,alisisitiza.
Hata hivyo padre Mgaya ametoa wito kwa waumini ambao wanataka kutoa ushuhuda wa mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta kuendelea kujiandikisha kwa maparoko  katika ofisi zote za parokia na kwamba  kamati inaendelea kukutana na watoa ushuhuda na kufanya mahojiano ya ana kwa ana.
Baadhi ya waumini ambao walishiriki katika misa maalum ya kuhamisha masalia hayo hadi mahali pa wazi ndani ya kanisa kuu la mtakatifu Mathias Kalemba wamefurahisha na kitendo cha kanisa kuyaweka masalia hayo mahali ambapo kila mmoja anapata fursa ya kugusa na kufanya maombezi.
Agnela Kimanga,Christina Kayombo na  Editha Sangana wakazi wa Lizabon  mjini hapa wamesema walikuwa wanatamani kugusa na kufanya maombi kwenye sanduku la Sr.Bernadeta lilipohifadhiwa katika kanisa la uaskofuni ,lakini walikuwa wanaogopa na kwamba sasa wanaweza kugusa wakati wowote kwa kuwa masalia hayo yapo mahali pa wazi kanisani.
Kiongozi limeshuhudia waumini wakimiminika katika kanisa kuu la mtakatifu Mathias Kalemba kila siku kanisa linapokuwa wazi kwa lengo la kugusa na kufanya maombezi kwenye sanduku la Sr.Bernadeta mara baada ya masalio hayo kuhamishiwa katika kanisa hilo Jumapili iliyopita
Makao makuu ya kanisa katoliki Vatican  yametoa ruhusa kwa jimbo kuu katoliki la Songea kuanza mchakato wa utafiti  kuhusu maisha,fadhila za uhodari,sifa ya utakatifu na nguvu za kimaombezi za Sr. Bernadeta Mbawala ili aweze kutangazwa kuwa mwenyeheri na hatimaye mtakatifu.
Sr. Bernadeta Mbawala aliyezaliwa Oktoba 27,1911 katika kijiji cha Likuyufusi wilayani Songea mkoani  Ruvuma alifariki Novemba 29,1950 na kuzikwa  katika makaburi ya Abasia ya Peramiho ambapo mapema mwaka huu masalia yake yalifukuliwa kwa lengo la kuanza mchakato wa kutangazwa mwenyeheri kisha mtakatifu.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129







No comments:

Post a Comment