Tuesday, May 15, 2012

Samaki wanaotoa umeme wapo ziwa Tanganyika


  
Na Albano Midelo

TANZANIA ni nchi pekee katika Afrika mashariki ambayo imebahatika kuwa na vivutio vya kipekee ambavyo huwezi kuviona katika sehemu nyingine yeyote duniani.

Tanzania ina maliasili mbalimbali kama vile maziwa, Bahari ya Hindi,  milima, wanyama pori,mambo ya kale,mawe ya ajabu ,vimondo ambavyo vimedondoka toka angani pamoja na vivutio vingine vingi.


Nchi yetu imebahatika kuwa na maziwa mengi kuliko nchi yeyote katika bara la Afrika.Maziwa hayo ni pamoja na ziwa Viktoria,Tanganyika,Nyasa,Rukwa na maziwa mengine madogo.

Maziwa hayo yote licha ya kuwapatia wananchi wake kitoweo na kipato kutokana na samaki wanaovuliwa ,pia  ni kivutio kikubwa cha utalii.

 Ziwa Tanganyika lililopo magharibi mwa nchi ni miongoni mwa  kivutio cha utalii.Ziwa hilo lipo katika mikoa ya Kigoma na Rukwa na kuelekea hadi katika nchi jirani za Kongo DRC na Burundi.

Ziwa Tanganyika ni ziwa lenye sifa za kipekee sio tu katika Tanzania bali hata ukilinganisha na maziwa mengine ulimwenguni  hakuna ziwa ambalo linafanana na ziwa Tanganyika.

Ziwa Tanganyika lina sifa kuu nne ambazo pamoja na kuwa ziwa refu kuliko maziwa yote ulimwenguni likiwa na urefu wa kilometa 673 kutoka kaskazini hadi kusini mwa ziwa hilo.

Sifa nyingine ya ziwa Tanganyika ni kuwa na kina kirefu kwenda chini.Ziwa hilo linashika nafasi ya pili kwa kina kirefu ulimwenguni baada ya nafasi ya kwanza kuchukuliwa na ziwa Baikar ambalo lipo  katika nchi ya Rusia.

Kina cha ziwa Tanganyika ni kilometa 1.47 au meta 1470  hivyo ziwa hilo kuwa na kina cha kipekee ambacho ni kivutio cha utalii kianchoweza kuwasukuma watalii  kufika katika ziwa hilo kuona maajabu hayo.

Ziwa hilo linawashangaza wengi kwa ukubwa na ujazo wake ambao ni kilometa za ukubwa 18,900 na kwamba ziwa hilo linachukua asilimia 17 ya maji yote baridi ulimwenguni.

Kana kwamba haitoshi ziwa Tanganyika lina utajiri mkubwa  wa viumbe hai wa aina mbalimbali wakiwemo samaki,mamba,viboko pamoja na viumbe wengine wa majini.

Watu wanaotaka kujifunza kupitia ziwa hilo wanapata fursa ya  mambo mbalimbali ya kibaiolojia na kiuchumi hasa kutokana na samaki wa aina  mbalimbali waliomo katika ziwa hilo.

Ziwa Tanganyika lina aina za samaki zaidi ya 400  na  kati ya aina hizo za samaki kuna aina ya samaki ambao wana uwezo wa kutoa umeme wanaofahamika kwa jina la electric fish haya ni maajabu  mengine ya dunia ambayo yanawashangaza wengi.

Kutokana na sensa ya samaki ya mwaka 1999 ziwa Tanganyika linakadiriwa kuzalisha samaki kati ya tani 165,000 hadi 200,000 zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 80 hadi milioni 100.Miongoni mwa samaki maarufu katika ziwa hilo ni dagaa,migebuka,kambale,sangara,magege,samaki wa mapambo,singidae na kuhe.

Mhifadhi wa kutoka hifadhi ya Gombe Noelia Mnyonga ambaye analifahamu vyema ziwa Tanganyika,  akizungumzia samaki ambao wanatoa umeme,anabainisha kuwa aina hiyo ya samaki wanatoa umeme pale wanaposogelewa na adui hivyo kuwa kivutio adimu na cha kipekee ulimwenguni.

“Samaki huyu kwa kuwa anatoa umeme iwapo angetangazwa ndani na nje ya nchi watalii wengi wangemimika kwenda katika ziwa Tanganyika ili kwenda kumuona na hivyo serikali kupata kipato kikubwa”,anasisitiza Mnyonga.

Anaongeza kuwa watalii hao baada ya kusikia habari za samaki anayetoa umeme hakuna ubishi wangependa kufika ziwa Tanganyika na kuona samaki huyo anatoaje umeme na kwamba aina hiyo ya samaki haipatikani katika maziwa mengine duniani zaidi ya ziwa Tanganyika.

Baadhi ya watalii wanapenda kujifunza maisha ya viumbe wa majini akiwemo samaki huyo anayetoa umeme hivyo wanapopata fursa ya kufika katika maziwa  kama ziwa Tanganyika wangependa kufanya utafiti wa aina mbalimbali za samaki na kufahamu aina na tabia za samaki.

Ukiachia samaki huyo anayetoa umeme,ziwa Tanganyika pia lina aina nyingine za samaki wakiwemo dagaa maarufu wa kigoma.Katika miji ya Kigoma na Sumbawanga  wakazi katika miji hiyo wanafanya biashara ya dagaa hao wanaovuliwa katika ziwa Tanganyika.

Biashara ya dagaa kutoka ziwa hilo endapo itaboreshwa  na wadau wake kujipanga vizuri dagaa hao wanaweza kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi na kuinua maendeleo yao kiuchumi.

Hata hivyo baadhi ya wakazi katika miji hiyo wanapeleka dagaa hao katika nchi za jirani ikwemo Kongo DRC,Burundi na Zambia katika kiwango ambacho hakitoi mapato makubwa.

Mhifadhi wa ziwa Tanganyika anatoa wito kwa serikali kutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika ziwa hilo kwa kujenga viwanda vya kusindika dagaa ili hatimaye dagaa hao waweze kupelekwa kuuzwa nje ya nchi katika viwango vya kimataifa ili kutoa faida kubwa zaidi .

Ziwa Tanganyika lingeweza kuwasaidia wananchi wanaoishi katika ziwa hilo hususani mikoa ya Kigoma na Rukwa endapo wangejiunga katika vikundi na kupata mtaalamu ambaye angewafundisha mambo ya kitalii na kufanya utalii wa uvuvi.

Vikundi hivyo kupitia utalii wa uvuvi wangeonyesha njia  zao za asili za kuvua samaki,upikaji wa samaki kwa njia ya asili ,uhifadhi wa samaki kwa njia ya asili hivyo kuwavutia  watalii kuona hatua mbalimbali za uvuvi wa asili.

Watalii wengi hawajaona njia za asili za kuvua,kupika na kuhifadhi samaki kutokana na ukweli kuwa wao wamezoea kuvua samaki kwa kutumia mitambo maalum.

Wananchi wanaozunguka hifadhi ya ziwa Tanganyika wanaweza kufaidika na uvuvi wa kitalii na kwamba pato watakalolipa watalii hao litakwenda moja kwa moja katika serikali za vijiji au vikundi vyao.

Kwa kuwa tayari watalii watakuwa wamefika katika hifadhi hiyo ya ziwa Tanganyika,pia wananchi watapata fursa ya kuuza samaki hao kwa watalii huku wakionyesha utamaduni wao kwa ngoma za asili ambapo watalii watatozwa fedha za kuangalia utalii huo wa kiutamaduni na kujiongezea kipato.

Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya ameshauri  kuimarisha ushirikiano baina ya nchi jirani za Kongo DRC , Burundi na Tanzania ili kulifanya ziwa Tanganyika kuwa na matumizi endelevu kwa kuwa ziwa hilo limezungukwa na nchi hizo.

Ameshauri mabalozi katika nchi hizo wasaidia kuunganisha utalii kutoka katika nchi zote sanjari na kuboresha mazingira ya ziwa Tanganyika ili kuwalinda viumbehai waliomo ndani ya ziwa ziwa hilo.

Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa kina cha ziwa Tanganyika kinapungua mwaka hadi mwaka kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira  ambao unaendelea kufanywa kutokana na shughuli mbalimbali za kibidamu.

“ Watu wanakata miti ovyo kwenye hifadhi ya ziwa Tanganyika,vyanzo vya maji vinavyotiririka kuelekea kwenye ziwa hilo vimeharibiwa katika kiwango kinachotisha hivyo kuathiri ziwa hilo ambalo ni muhimu kwa uchumi wa Taifa’’anasisitiza mhifadhi wa ziwa hilo.

Anashauri wadau wote wa mazingira katika nchi zinazozunguka ziwa Tanganyika kuungana kwa pamoja katika kulinda mazingira ya ziwa Tanganyika hasa kuhamasisha kupanda miti katika maeneo mbalimbali hivyo kufanya ziwa Tanganyika kuwa endelevu.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129.


No comments:

Post a Comment