Na Albano
Midelo
WANAFUNZI wa shule
tatu za msingi zaidi ya 500 katika kata ya Rwinga wilayani Namtumbo mkoani
Ruvuma wanasomea kwenye madarasa yaliojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi.
Uchunguzi uliofanywa
katika shule tatu kati ya saba zilizopo kwenye kata hiyo ambayo ipo mjini
Namtumbo umebaini kuwa katika shule ya
msingi Rwinga wanafunzi 296 wanasomea kwenye vibanda vya miti
vilivyoezekwa kwa nyasi.
.
Mwalimu wa taaluma
katika shule hiyo Onesmo Mbawala alisema
idadi kubwa ya wanafunzi katika shule hiyo wanasomea katika vibanda vya nyasi
kutokana na shule hiyo kuwa na upungufu wa vyumba 12 vya kusomea ambapo vyumba
vilivyopo ni vinne tu na kwamba shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1975 ina jumla ya
wanafunzi 592.
Katika shule ya
msingi Selous jumla ya wanafunzi 108 wa madarasa ya tano na sita wanasoma
kwenye vibanda vya nyasi hali ambayo walimu wanasema inachangia kushusha
taaluma kwa wanafunzi.
Mwalimu wa taaluma katika shule hiyo Sheweji
Simba alisema shule hiyo iliyoanzishwa
mwaka 2007 ina jumla ya wanafunzi 477 huku ikiwa na vyumba vinne tu vya
madarasa kati ya mahitaji ya vyumba nane hali ambayo imesababisha baadhi ya
wanafunzi kusomea kwenye vibanda vya nyasi .
Katika shule ya
msingi Mkapa ambayo imepewa jina la aliyewahi kuwa kiongozi mkuu wa nchi Rais mstaafu Benjamin Mkapa pia kuna
wanafunzi wanaosomea kwenye vibanda
viwili vya nyasi kwa kuwa shule hiyo ina
vyumba vinne tu kati ya mahitaji ya vyumba nane.
Mkuu wa shule hiyo
Hans Mwailima alisema shule hiyo yenye wanafunzi 306 madarasa matatu yanasomea
katika chumba kimoja ambapo kuanzia
darasa la tatu hadi la sita wanasomea
kwenye vibanda vya nyasi kwa zamu .
“Unajua wanafunzi
wana tabia ya kutaniana hivyo endapo darasa moja wakisoma kwenye vibanda vya
nyasi kila siku wenzao wanawatania hivyo kukata tamaa na wengine kuwa watoro
hivyo tumeamua wote wawe wanasoma kwenye vibanda vya nyasi kwa zamu ili kujenga
mvuto wa mazingira ya kusomea’’,alisema.
Mratibu elimu kata ya
Rwinga Thomas Komba amekiri shule tatu
kati ya saba katika kata yake ambazo ni Rwinga,Mkapa na Selous wanafunzi
kusomea katika vibanda vilivyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi na
kusisitiza kuwa shule za Minazini,Kidagulo,Migelegele na Mandepwende ndizo
shule pekee katika kata hiyo ambazo hazina vyumba vya madarasa vilivyoezekwa
kwa nyasi.
“Shule zangu tatu za Rwinga,Mkapa na Selous katika kata
yangu zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa hali ni mbaya
tunafanya jitihada za kuhamasisha jamii ili waweze kujitolea kufyatua tofali
kuzichoma kwa kushirikiana na serikali
ili kupata vyumba zaidi na kumaliza kero hii ya aibu’’,alisisitiza.
Makamu mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Kasimu Ntara alidai kuwa kuwa kuwepo kwa
madarasa yaliojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi katika wilaya hiyo
kunatokana na kuanzishwa shule nyingi za msingi .
“Mpango wa uboreshaji
wa elimu ya msingi MEM nchini ulisababisha kuanzishwa kwa shule nyingi
hivyo baada ya kuondoka kwa MMEM serikali imeshindwa kumudu ujenzi wa vyumba vya madarasa jitihada zinaendelea
kufanyika kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa’’,alisisitiza.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

Bado tu jamani hata baada ya miaka 50 ya uhuru sasa sijui tusema bora elimu au elimu bora?
ReplyDelete