|
Na Albano Midelo
WANAFUNZI 201 kuanzia
darasa la tatu hadi la sita katika shule
ya msingi Kidugalo kata ya Rwinga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wanasoma
katika vyumba viwili vya madarasa kwa kugeuziana migongo hali ambayo inachangia
kushusha taaluma katika shule hiyo.
Mwalimu mkuu wa shule
hiyo Owini Mpangala alibainisha kuwa wanafunzi 51 wa darasa la tatu na wanafunzi 56
wa darasa la nne wanasoma katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo na
wanafunzi 62 wa darasa la tano na wanafunzi 32 wa darasa la sita wanasoma
katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo.
“Madarasa mawili
kusomea katika chumba kimoja kunasababisha kila darasa kufundishwa vipindi
vinne tu kati ya vipindi nane vinavyotakiwa kufundishwa kwa siku,walimu wawili
hawawezi kuingia kwa wakati mmoja kufundisha kwenye chumba kimoja,vipindi vinne
vinapotea darasa
halifundishiki’’,alisisitiza.
Kutokana na hali hiyo
baadhi ya walimu wanakaa nje ya ofisi wakati wa kiangazi huku wakiendelea
kufanyakazi za kusahihisha madaftari ya wanafunzi wakipigwa na jua hali ambayo
inaleta kero kubwa kwa walimu na wanafunzi.
Mkuu wa shule hiyo
alisema amechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na matatizo hayo ikiwa ni
pamoja na kuyapeleka katika kamati ya shule na Baraza la madiwani ambayo
wameahidi katika msimu ujao wa fedha wanatarajia kulipatia kipaumbele hasa kero
ya upungufu wa vyumba vya madarasa,samani na ofisi ya walimu.
“Hapa kwangu uongozi
wa serikali ya kijiji umekataa kujenga vibanda vya nyasi kama ilivyo katika
shule nyingine kwa madai kuwa hapa ni mjini hawawezi kujenga vibanda vya nyasi
ni aibu,wamefyatua tofali zipo kwenye tanuri’’,alisema.
Baadhi ya walimu
wanaofundisha katika shule hiyo wamesema wanatamani kuacha kazi au kuhama
katika shule hiyo kutokana na changamoto nyingi ambazo hazijapatiwa ufumbuzi
kwa muda mrefu na kuchangia kushusha elimu katika shule hiyo ambayo ipo mjini.
Mratibu elimu kata ya
Rwinga Thomas Komba amekiri shule za msingi katika kata yake inakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo shule ya msingi Kidugalo ambapo hivi sasa
uhamasishaji unafanyika ili kumaliza kero ya upungufu mkubwa wa vyumba vya
madarasa.
Aliongeza kuwa
wananchi wa eneo la Kidugalo mwaka jana wamefyatua na kuchoma tofali kwa ajili
ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na kwamba hivi sasa kinachosubiriwa ni nguvu
toka serikalini kutoa vifaa vya kiwandani ili kuweza kufanikisha kupunguza kero
hiyo ya muda mrefu.
Halmashauri ya wilaya
ya Namtumbo ina shule za msingi 107 kati ya hizo shule 105 zinamilikiwa na
serikali na shule mbili ni za watu binafsi na mashirika ya dini.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

Hapo sasa itakuwa mchanganyiko wa hali ya juu kaazi kwelikweli. Kwa nini isiwe hivi kuwa wawe wanasoma nusu siku. Yaani kupokezana hilo darasa nakumbuka tulikuwa na mtindo huu nilipokuwa darasa la kwanza yaani la kwanza wanasoma asubuhi mpaka saa nne au sita na la pili wanakuja baada ya hapo:
ReplyDeleteKupanga ni kuchagua na kuchagua ni kupanga.
ReplyDeleteJe hali hii ndiyo hali halisi au tunaangalia tulipoangukia na kushau tulipojikwaa?