Na Albano Midelo
SIKU za
hivi karibuni baadhi ya viongozi,vyombo
vya habari na wadau wa mazingira wameilaumu mikaratusi(eucalyptus) kutokana na kudaiwa miti hiyo inanyonya maji
katika kiwango kikubwa.
Kutokana
na hali hiyo yamefanyika maazimio ya kuing’oa miti hiyo kama ambavyo inafanyika kwenye msitu wa
serikali wa milima ya Matogoro iliyopo wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Meneja wa
hifadhi ya msitu wa Matogoro Abedinego
Sakafu anasema majaribio ya upandaji wa miti ya kigeni aina ya misindano na
mikaratusi ulianza mwaka 1957 na upandaji kamili ulianza mwaka 1961 na kukamilika mwaka 1978
ambapo jumla ya ekari 867.2 zilipandwa .
Hata
hivyo Sakafu anabainisha kuwa licha ya miti hiyo kuwa na faida kibiashara siku zilivyokwenda ilibainika miti hiyo ina
madhara kwenye vyanzo vya maji vilivyopo kwenye milima ya Matogoro.
Kwa
mujibu wa mhifadhi huyo miongoni mwa madhara ambayo yalianza kujitokeza kwenye
msitu huo ni uwingi wa maji yaliokuwa yanatiririka kutoka katika mito iliyopo
yalianza kupungua na ubora wa maji pia ulipungua kutokana na kuongezeka
kwa acidity kwenye maji kuliko viwango
vinavyotakiwa kwa matumizi ya binadamu.
“Baada ya
kuona madhara hayo wizara ya maji iliiomba wizara ya maliasili na utalii ibadili
lengo la shamba la miti Matogoro kutoka kuwa la kibiashara hadi kuwa pori la
hifadhi kwa kuondoa miti yote ya kigeni na kupanda miti ya asili ambayo ni
rafiki wa maji’’,anasisitiza.
Sakafu
anabainisha kuwa kazi ya kuondoa miti ya kigeni ilioanza mwaka 2003 ipo katika
hatua za mwisho ambapo jumla ya ekari 827 zimekwishavunwa na eneo lililosalia
ni ekari 40 tu na kwamba kazi ya kuvuna miti yote inatarajia kukamilika mwaka
huu.
Hata
hivyo anasema upandaji wa miti ya asili unaendelea kwa wastani wa ekari 40 kwa
mwaka na ameitaja miti ya asili ambayo inapandwa kuwa ni minyenda,minyonyo na
migwina ambapo jumla ya ekari 550 zimeoteshwa miti hiyo na upandaji unaendelea
katika eneo ambalo uoto wa asili ni mdogo.
Hata
hivyo Sakafu anasema miti ya kigeni aina ya mikaratusi ambayo imevunwa hivi sasa inaota na kusambaa katika maeneo yaliovunwa hali inayoathiri miti ya
asili na kwamba mikaratusi inadumaza
ukuaji wa miti ya asili na wakati mwingine kuiua kabisa kutokana na ukuaji wake
wa haraka.
Enock Buja afisa maliasili wa mkoa wa Ruvuma anaelezea mashaka yake kuhusu utafiti
uliofanywa na shirika moja la nje ya nchi mwaka 2000 katika milima ya Matogoro
kwamba miti aina ya mikaratusi iliyopandwa katika msitu huo yote ivunwe kwa
madai kuwa inanyonya maji mengi kwenye
vyanzo vya maji na kwamba utafiti huo kwa maoni yake una mashaka.
“Utafiti
wa kisayansi unaonesha kuwa sio miti yote aina ya mikaratusi ikiwemo ya milima
ya Matogoro ina tabia ya kunyonya maji kwenye vyanzo vya maji,miti ile ni
rafiki wa vyanzo vya maji ndiyo maana katika misitu mingine nchini kama ile ya
SARNIWAT Njombe na Sao Hill Mafinga imepandwa miti ya mikaratusi tena karibu na
vyanzo vya maji ambavyo vimeendelea kutoa maji na hakuna dalili zozote za ukame
au maji kupungua”,anasisitiza.
Ameishauri
serikali kutafakari tena kuhusu agizo la
kuvuna miti yote ya kupandwa katika msitu huo kwa wakati mmoja na kupanda miti
ya asili jambo ambalo ametahadharisha kuwa miti ya asili inachelewa kukua hivyo
inaweza kuathiri mlima wa Matogoro na kusababisha vyanzo vya maji kukauka na
wananchi wa mji wa Songea kukabiliwa na ukame.
Hata
hivyo utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu nchini (TAFORI), umebaini
kuwepo kwa aina kadhaa ya miti ambayo kwa kiwango kikubwa inanyonya maji mengi.
Kulingana
na utafiti wa TAFORI miti hiyo ni Mikaratusi jamii ya Camaldulensis ambayo hunyonya maji kiasi cha milimita 1,240 kwa
mwaka na Mikaratusi aina ya Microrhea
inayonyonya maji milimita 1,050 kwa mwaka, Mikaratusi ya aina ya Patula nayo hunyonya maji kiasi cha
milimita 665 kwa mwaka.
Changamoto
iliyopo hivi sasa ni kwamba miti mingi aina ya mikaratusi imekwishaondolewa isipokuwa tatizo la kujiotea kila inapovunwa
ndilo linalosumbua na kuathiri miti ya asili ambayo imepandwa.
TAFORI kuhusu ukweli wa miti ya kigeni na matumizi ya maji
imebainisha kuwa mwaka 2000 eneo la mashamba
ya miti ya kigeni aina ya mikaratusi duniani kote lilikaribia hekta milioni 18
kati ya hizo asilimia 37 ya eneo hilo lilikuwa barani Afrika na asilimia 73 ya
eneo hilo lipo Afrika ya kusini.
Taarifa
ya TAFORI inabainisha kuwa mashamba
mengine makubwa ya mikaratusi barani
Afrika yapo katika nchi za Morocco,Angola,Ethiopia na Tunisia na kwamba katika Afrika mashariki nchi ya
Kenya inaongoza kwa mikaratusi
ikifuatiwa na Uganda na Tanzania na kwamba maeneo ya mikaratusi katika nchi za
Burundi na Rwanda ni maradufu ya maeneo ya nchi ya Kenya.
Kutokana
na utafiti huo TAFORI inabainisha kuwa Tanzania haijumuishi kwenye nchi maarufu
kwa upandaji wa mikaratusi na kwamba haiwezi kuchukua nafasi ya kwanza kubaini
madhara ya mikaratusi.
Hata
hivyo utafiti ambao umetolewa na TAFORI
kuhusu miti ya kigeni na matumizi ya maji unaonesha
kuwa mikaratusi iliyopo katika nchi ya Sudan kwa mwaka
matumizi yake ya maji ni milimita 1240 wakati mikaratusi katika nchi ya
Pakstani matumizi ya maji kwa mwaka ni milimita 1500.
Utafiti
huo unaonesha kuwa mikaratusi iliyopo nchini Kenya kwa mwaka matumizi ya maji
ni milimita 830 na miti aina ya misindano Tanzania katika msitu wa Sao
hill kwa mwaka hutumia maji milimita
665.
Kulingana
na utafiti huo matumizi ya maji kwa mwaka kwa miti mingine na mazao ukilinganisha
na mikaratusi unaonesha kuwa miti aina ya mvinje iliyopandwa Bura nchini Kenya kwa mwaka inatumia maji milimita 5437, jamii ya mpingo katika eneo la
Bura Kenya kwa mwaka inatumia maji milimita 1143 na Mgunga nchini Paktan
unatumia milimita 2100 za maji kwa mwaka.
Utafiti
huo unaonesha kuwa mazao ya kilimo nchini Pakstani yakiwemo ngano kwa mwaka
yanatumia milimita 330 za maji,pamba milimita 460,mahindi nchini Marekani kwa
mwaka yanatumia maji milimita 630 na pamba ya Marekani inatumia maji milimita
630.
Zao la
korosho hapa nchini katika wilaya ya Nachingwea kwa mwaka linatumia maji
milimita kati ya 814 hadi 1409,mpunga nchini Pakstan kwa mwaka unatumia maji
milimita 1620 na miwa katika nchi ya
Pakstani inatumia maji milimita 1400 kwa mwaka.
Utafiti
huo unaonesha kuna miti kama mvinje na mgunga inatumia maji mengi kuliko
mkaratusi na kwamba yapo baadhi ya mazao kama mpunga na miwa ambayo yanatumia
maji karibu sawa au zaidi ya mikaratusi.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment