MKURUGENZI wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi(KIUMA)
wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma Dk.Matomora Matomora amewatahadharisha wauguzi
na madaktari nchini kujiepusha na vitendo vya rushwa wanapowahudumia wagonjwa.
Dk.Matomora alitoa tahadhari hiyo wakati anazungumza kwenye
mahafali ya chuo cha uuguzi cha KIUMA
ambapo jumla ya wahitimu 79 walitunukiwa vyeti baada ya kuhitimu mafunzo
ya uuguzi ya miaka miwili.
Alisisitiza kuwa uhai wa mgonjwa unamtegemea muuguzi na
daktari hivyo ni dhambi kubwa na kitu kibaya kwa muuguzi kuanza kuchangisha
fedha kutoka kwa mgonjwa na jamaa zake ambapo amewashauri iwapo mshahara
hautoshi ni vema kumdai mwajiri husika
badala ya kuomba rushwa kwa wagonjwa ambao hawana hatia bali wanahitaji huduma za
afya.
Awali akitoa taarifa ya chuo hicho Bi. Elvira Makota ambaye
ni mkuu wa chuo cha uuguzi KIUMA alibainisha kuwa katika chuo hicho wanachuo
walianza mwezi Agosti 2010 wakiwa wanachuo 84 ambapo waliomudu kuhitimu ni
wanachuo 79.
Makota alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu chuo
cha uuguzi KIUMA kimeweza kuzalisha wauguzi 191 ambao hivi sasa wanafanyakazi
ya uuguzi karibu mikoa yote Tanzania.
Akisoma risala ya wahitimu wa chuo hicho kwa niaba ya wenzake
mwanachuo Luciana Haule amepongeza mfadhili wa Taasisi ya KIUMA Profesa
Dr.Deichmann ambaye ni Rais wa misioni ya Neno na Tendo kutoka nchini Ujerumani
ambaye amewezesha vijana kutoka mikoa ya kusini kupata elimu kwa gharama nafuu.
Hata hivyo risala hiyo imezitaja changamoto mbalimbali
zinazokikabili chuo hicho kuwa ni pamoja na ukosefu wa umeme wa uhakika
unaosababisha mazingira ya wanachuo kujisomea kuwa magumu,pia chuo kimekosa
mawasiliano ya mtandao wa intaneti hali inayosababisha wanachuo kukosa taarifa
mbalimbali na upungufu wa wauguzi katika hospitali ya KIUMA unaathiri wanachuo
katika mazoezi ya vitendo.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika mahafali hayo Profesa
Dk.Deichmann Rais wa misioni ya Neno na Tendo kutoka nchini Ujerumani ameahidi
kuendelea kuisaidia Taasisi ya KIUMA kutokana na maendeleo makubwa ya kiroho na
kimwili yaliopatikana.
Taasisi ya KIUMA inaendesha Taasisi mbalimbali ambazo ni chuo
cha uuguzi,hospitali,chuo cha ufundi,chuo cha Biblia,sekondari na chuo cha
ualimu ambacho kinatarajia kuanza mwaka huu kozi ya stashahada.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129 
No comments:
Post a Comment