Kumekua
na madai mazito kuhusiana na ugawaji fedha unaofanywa na mgombea huyo na
kwamba anatumia mbinu ya kugawa fedha hizo kwa njia ya mtandao.
Akizungumzia
madai hayo ya rushwa, Kaimu Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Hanang’ Samson
Sanga alikataa kuzungumzia kuhusu taasisi yake kufanya kazi zake kwa siri kwa
maelezo kwamba kwa sasa ofisi yake haiwezi kuzungumzia suala hilo.
Wiki
hii, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah alinukuliwa akisema
taasisi yake inafuatilia kwa karibu uchaguzi huo ndani ya CCM ili kubaini
watu wanaotumia rushwa.
Dk.
Hoseah alitoa kauli hiyo akijibu hoja mbalimbali za washiriki wa kongamano la
kujadili utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa kupambana na rushwa nchini
na mapendekezo yanayopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa mpango wa awamu
ya tatu (2012 – 2016).
“Tatizo
ni kwamba wagombea wengi wa nafasi ya uongozi wamekuwa wakijiandaa kutoa
rushwa wakati wa uchaguzi na kwa bahati mbaya hata wananchi ambao ni wapiga
kura ni kama wanajiandaa kupokea rushwa kila uchaguzi unapokaribia, hili ni
tatizo kubwa,” alisema Dk Hosseah na kuongeza:
“Tunaendelea
kufuatilia, lakini ni kazi kubwa kwelikweli kwa mfano, sasa tunafuatilia
uchaguzi wa ndani wa CCM na tunafanya hivi ili kuhakikisha kwamba hatupati
viongozi wanaotokana na rushwa, maana tukiwa na viongozi wa aina hii hatuwezi
kushinda vita hivi.”
Katika
kikao kilichofanyika Jumapili ya Septemba 2, mwaka huu na kuongozwa na
katibu wa CCM Wilaya ya Hanang’ Allan Kingazi, wajumbe wa kikao hicho
walipitisha jina la Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Leonsi Marmo
huku Dkt Nagu akitoswa kufuatia kudaiwa kuwa na majukumu mengi ya kikazi
ikiwemo ubunge na uwaziri.
Wakizungumzia
maamuzi ya vikao vya juu vilivyopitisha jina la Dk. Nagu kuwa mmoja wa
wagombea wa nafasi hiyo, baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya ya
Hanang’ walioomba kutotajwa majina yao gazetini walisema kamati hiyo
haikuwatendea haki.
“Kamati
kuu haikutenda haki kabisa, kwa kuwa imepuuza maamuzi yetu, haiwezekani sisi
tufanye maamuzi tena kwa kufuata kanuni za CCM ilizotunga yenyewe halafu
maamuzi yetu yabadilishwe na kuonekana sio sahihi, huku ndio kunakopeleka
pabaya hiki chama,”alisema mmoja wa wajumbe waliodaiwa kupigia kura jina la
Dkt.Nagu kutopitishwa katika kikao kilichofanyika Septemba 2 mwaka huu.
|
No comments:
Post a Comment