Na
Albano Midelo
UTORO ni moja ya
changamoto kubwa inayozikabili shule nyingi za msingi katika wilaya ya Nyasa
ambazo zipo mwambao mwa ziwa Nyasa mkoani Ruvuma.
Shule za mwambao mwa
ziwa Nyasa zinakabiliwa na utoro unaotokana na sababu mbalimbali zikiwemo
wanafunzi kujihusisha na uvuvi,biashara ndogo ndogo,mazingira duni ya
kujifunzia na ukosefu wa chakula cha mchana .
Shule ya msingi Mango
iliyopo katika kata ya Kihagara wilayani Nyasa ni miongoni mwa shule ambayo
kabla ya mwaka 2007 ilikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi watoro hali ambayo
ilikuwa inachangia kushusha taaluma katika shule hiyo.
Shule ya msingi Mango
ni miongoni mwa shule kongwe mwambao mwa ziwa Nyasa ambayo ilianzishwa na
kanisa katoliki mwaka 1933 kabla ya kuchukuliwa na serikali,hivi sasa ina
wanafunzi 508 kati yao wavulana 275 na wasichana 233.
Mkuu msaidizi wa
shule hiyo Marion Mchilas anasema mahudhurio ya wanafunzi hivi sasa katika
shule hiyo ni asilimia 97 ukilinganisha na awali ambapo mahudhurio yalikuwa
kati ya asilimia 60 hadi 75.
Amesema wazazi na
walezi kwa muhula wanachangia mahindi na maharage kwa ajili ya chakula cha mchana na kwamba mpango huu
umepunguza utoro kwa asilimia 30 hivi sasa wanafunzi wanaohudhuria masomo muda
wote wakiwemo wanafunzi waliokuwa watoro wa kila siku.
“Katika shule hii
wanafunzi wengi wanaishi mbali na maeneo ya shule hali ambayo ilikuwa
inasababisha utoro kabla ya kuanzia mpango huu wa kutoa chakula cha mchana
shuleni,mtendaji wa kijiji ametusaidia sana kuwahamasisha wazazi na walezi
waliokuwa wagumu hivi sasa karibu wote wanachangia’’,alisema.
Anabainisha kuwa
kutokana na shule kutoa chakula shuleni kumechangia shule hiyo kufanya vizuri
katika taaluma ikiwemo kuwa na matokeo mazuri ya mtihani wa Taifa wa darasa la
saba kila mwaka.
Takwimu zinaonesha
kuwa shule ya msingi Mango mwaka 2007 wanafunzi waliohitimu darasa la saba
walikuwa 62 kati yao wanafunzi waliofaulu walikuwa ni 58,mwaka 2008 shule hiyo
ilifaulisha wanafunzi 25 kati ya 30 waliohitimu na kwamba kati ya 25 wanafunzi
wanane walichaguliwa kwenda katika shule zenye vipaji maalum.
Kulingana na takwimu
za ufaulu katika shule hiyo mwaka 2009 wanafunzi waliohitimu darasa la saba walikuwa 92 kati yao wanafunzi 75 walifaulu,mwaka
2010 wanafunzi waliohitimu walikuwa 30
kati yao wanafunzi 17 walifaulu na mwaka 2011 wanafunzi 31 walifaulu mtihani wa
Taifa kati ya wahitimu 62.
Mchilas amesisitiza
kuwa ukaguzi wa shule ambao unafanyika kila mwaka katika shule hiyo kutoka kitengo
cha ukaguzi wilaya kumechangia shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma ambapo
amesema kitengo cha ukaguzi ni muhimu kwa maendeleo ya shule za msingi.
Pamoja na mafanikio
hayo mkuu huyo wa shule amezitaja changamoto ambazo zinaikabili shule hiyo kuwa
ni pamoja na upungufu wa vyumba vinne vya kusomea kati ya vyumba 11
vilivyopo,upungufu wa walimu wanane,hivi sasa shule ina walimu sita tu.
Changamoto nyingine
amezitaja kuwa ni upungufu wa vitendea kazi ambapo shule hiyo ina upungufu
mkubwa wa vitabu vya kiada na ziada hali ambayo imefikia darasa moja kuwa na
vitabu vitatu kwa kila somo linalofundishwa kila siku yaani Hisabati,Kiswahili
na Kiingereza.
Mkuu huyo ameelezea
masikitiko yake kwa shule hiyo kongwe ambayo inafanya vizuri kitaalamu,walimu
wote katika shule hawana nyumba hali ambayo inawafanya walimu kwenda kupanga
uraiani ambako hakuna nyumba nzuri zinazokidhi viwango zikiwemo zilizoezekwa
kwa nyasi.
“Shule hii haina hata
nyumba moja ya mwalimu,mimi mwalimu mkuu pia sina nyumba ya kuishi,zipo nyumba
zinazomilikiwa na kanisa katoliki ambazo zimechakaa,zinavuja, zimebomoka na
hakuna mtu anayeweza kuishi,tumewaomba kamati ya shule kwa kushirikiana na
serikali ya kijiji watujengee nyumba utekelezaji bado’’,anasema.
Mkuu wa shule ya
msingi Nambira Erasmus Haule anasema wanafunzi katika shule hiyo wanapata
chakula cha mchana kwa kuchangiana wanafunzi waliotengeneza kikundi cha watu
watano ambalo kila mmoja amepangiwa siku moja mzazi wake kuandaa chakula na
kuleta shuleni .
Chakula cha mchana
katika shule ya msingi Puulu kwa mijibu wa mwalimu mkuu Carthibet Maluka
kumesababisha mahudhurio ya wanafunzi kuwa zaidi ya asilimia 95 na shule
kufanya vizuri kitaaluma kwa mfano mwaka 2009 waliohitimu darasa la saba
walikuwa 89 waliofaulu walikuwa 87,mwaka 2010 walifaulu 65 kati ya wahitimu 68
na mwaka 2011 walifaulu 70 kati ya wahitimu 73
Uchunguzi ambao
umefanywa katika shule 10 za msingi katika kata za Liuli na Kihagara umebaini
kuwa kuna maendeleo makubwa ya taaluma katika shule ambazo wanafunzi wanapata chakula cha mchana kwa
kujiunga katika vikundi .
Wazazi na walezi
wamekuwa wanachangia gharama za kuandaa chakula ambapo kila mmoja amepangiwa
siku yake ya kuleta chakula shuleni hali hiyo imesaidia mahudhurio ya wanafunzi
kuwa mazuri kati ya asilimilia 90 hadi
95 kwa siku.
Baadhi ya shule za
msingi ikiwemo shule ya msingi Mango,Mwongozo,Nambira,Hongi,Muungano na
Kihagara wazazi na walezi baadhi yao wanakataa kuchangia chakula katika shule
zao hali ambayo inasababisha watoto wao kukosa chakula cha mchana na kuchangia utoro.
Hata hivyo wazazi na
walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hizo wameshauri walimu kuzingatia ratiba maalum ya masomo kwa
wanafunzi badala ya ratiba ya sasa ambayo wanafunzi wanatumia muda mwingi
kufanyakazi za mikono badala ya masomo darasani.
Afisa elimu msingi wa
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga David Mkali ambaye pia anasimamia wilaya mpya
ya Nyasa akizungumzia kuhusu utoaji wa chakula cha mchana katika shule za
msingi amesema asilimia zaidi ya 80 katika shule za msingi wanatoa chakula cha
mchana kwa wanafunzi.
Amesema hali hiyo
imesababisha utoro wa wanafunzi kupungua katika kiwango kikubwa ambapo shule
nyingi mahudhurio kwa siku ni zaidi ya asilimia 90 na kwamba wilaya pia
imejipanga kukabiliana na sababu nyingine za utoro ikiwemo baadhi ya wanafunzi kujihusisha na
uvuvi ambapo wanatumia sheria na kufanya vikao na wadau katika eneo husika ili
kumaliza kabisa utoro.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

No comments:
Post a Comment