Thursday, November 22, 2012

Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kitovu cha utalii kusini


Na Albano Midelo
HIFADHI ya Taifa ya Ruaha iliyopo kusini mwa Tanzania ndiyo hifadhi kubwa kuliko zote nchini yenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,226.
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni ya pili kwa ukubwa katika bara la Afrika,baada ya hifadhi ya Kafue iliyopo nchini Zambia.Hifadhi hii ni maarufu kwa wanyama wa aina ya kudu wakubwa na wadogo ambao wanapatikana kwa wingi.
Uhifadhi na ustawi wa hifadhi hii unategemea kwa kiasi kikubwa mto Ruaha  ambao pia una samaki wa aina mbalimbali pamoja na viboko na mamba.

Hifadhi ya Ruaha ina wanyama kama swalapala na pofu ambao ni mawindo ya kudumu ya wanyama kama simba,chui,fisi,mbweha na mbwamwitu.
Mhifadhi mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha Stefano Qolli  anabainisha kuwa hifadhi hiyo ina idadi kubwa ya tembo wanaokusanyika katika eneo moja kuliko eneo linguine lolote Afrika mashariki na kwamba hifadhi hiyo ina sifa ya kuwa na  aina za wanyama na mimea karibu yote inayopatikana katika nchi za kusini na mashariki mwa Afrika.

Ikiwa katikati ya Tanzania umbali wa kilometa 128 magharibi mwa mji wa Iringa,hifadhi hii inafikika kwa urahisi kwa ndege za kukodi kutoka jijini Dar es salaam,Arusha,Iringa na Mbeya.Pia hifadhi hii inafika kwa urahisi kwa njia ya barabara.
Mhifadhi mkuu huyo anasema mambo ambayo mtalii anaweza kufanya katika hifadhi hii ni pamoja na safari za miguu porini,kuangalia magofu yanayosadikiwa kuwa ni maskani ya watu wa kale katika kijiji cha Isimila kiasi cha kilometa 120 kutoka Iringa na kwamba magofi hayo ni miongoni mwa maeneo muhimu yenye historia ya kale barani Afrika.
“Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii kuangalia wanyama wakubwa ni wakati wa kiangazi kati ya mwezi Mei hadi Desemba,kuangalia ndege na maua ni wakati wa masika kati ya mwezi Januari hadi Aprili,malazi na hoteli za kitalii zinapatikana,pia maeneo ya kupiga kambi yapo’’anasisitiza.
Hata hivyo mhifadhi mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha anasema licha ya hifadhi hiyo kubwa kubwa kuliko zote nchini,idadi ya watalii wanaofika ni wachache ukilinganisha na takwimu katika hifadhi nyingine za taifa nchini .
Amezitaja baadhi ya sababu zinazosababisha watalii kuwa wachache ni pamoja na miundombinu mibovu ya barabara,uchache wenye hoteli zenye hadhi ya kitalii na kwa matumizi ya hifadhi hiyo kwa mwaka ni zaidi ya shilingi bilioni mbili wakati mapato yake kwa mwaka hayazidi shilingi bilioni 1.5.
Barabara ya lami kutoka Iringa kuelekea kwenye hifadhi hiyo inaishia katika kijiji cha Kalenga yalipo makumbusho ya Chifu Mkwawa,baada ya hapo barabara ni ya vumbi iliyojaa makorongo  hali ambayo ni kero kwa watalii wanaopenda kutembelea hifadhini hivyo kupunguza idadi ya watalii kila mwaka.
“Iwapo barabara ya lami itajengwa hadi katika kijiji cha Tungamalenga kinachopakana na hifadhi hii au kuishia katika geti kuu la kuingilia hifadhini,basi watalii wengi wanaweza kuvutiwa kutembelea hifadhi hii ambayo ni kubwa kuliko zote nchini’’,anasema.
“Hifadhi ya Taifa ya Ruaha haitangazwi kikamilifu kama zinavyotangazwa hifadhi za kaskazini,hata filamu zinazorushwa kwenye vituo vyetu vya luninga nchini ni zile ambazo picha zake zilipigwa katika hifadhi ya Taifa Serengeti,umefika wakati sasa wadau wote wa utalii kuelekeza nguvu kuhamasisha utalii hifadhi ya Ruaha’’,anasisitiza.
Kwa upande wake ofisa utalii wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha Pellagy Marandu anasema katika kipindi cha mwaka 2006/2007 hifadhi ilipokea watalii zaidi ya 19,000 kati yao watalii zaidi ya karibu 14,000 walitoka nje huku watalii 5000 wakiwa ni wa ndani.
Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2007/2008 idadi ya watalii katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliongezeka hadi zaidi ya 22,000 kati yao watalii kutoka nje ni zaidi ya 13,000 na watalii wa ndani walikuwa ni zaidi ya 8000.
Hata hivyo Marandu anasema idadi ya watalii katika kipindi cha mwaka 2008/2009 ilipungua katika hifadhi hiyo ambapo kulikuwa na watalii 19,000 kati yao watalii wa kutoka nje ni 11 na watalii wa ndani ni 8000 ambapo katika kipindi cha mwaka 2009/2010 idadi ya watalii ilikuwa ni zaidi ya 19,000.
Kulingana na Marandu idadi ya watalii wa ndani wanaotembelea kwenye hifadhi hiyo imeendelea kuwa ndogo kutokana na wananchi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu utalii ambapo wengi bado wana mtazamo potofu kudhani kuwa sifa kubwa ya mtalii ni  raia wa kigeni ambaye anayetoka nje ya nchi.
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha imefanikiwa katika kukabiliana na ujangili ambao unafanyika ndani ya hifadhi hiyo ambapo katika kipindi cha miaka minne zaidi ya watu 1000 wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujihusisha na ujangili kwenye hifadhi.
Mkuu wa idara ya ulinzi katika hiyo Paulo Gwaha anasema watu hao walihusishwa na ujangili wa wanyama na samaki waliokuwa wakiwavua katika mto Ruaha mkuu ambao unapita ndani ya hifadhi hiyo na kwamba baadhi ya majangili walikamatwa wakitumia silaha za kisasa zikiwemo zile ambao zilitumika katika vita ya Idd Amini wa Uganda kati ya mwaka 1978 hadi 1979.
Kulingana na  Gwaha kati ya majangili hao waliokamatwa,katika kipindi cha mwaka 2007/2008 walikamatwa majangili 521 na majangili 574 walikamatwa katika kipindi cha mwaka 2009.2010.
Katika kipindi cha mwaka 2010/2011 jumla ya majangili 745 walikamatwa na kwamba tangu Desemba 2011 hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2012 jumla ya majangili 480 walikamatwa na kwamba idadi kubwa ya majangili walikamatwa kabla hawajasababisha madhara katika hifadhi hiyo.
“Ujangili katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha unaathiri baoanuwai mbalimbali iliyopo na kulikosesha Taifa mapato,hata hivyo idadi ya askari na vitendea kazi kwa pamoja havitoshi kukabiliana na hali hiyo,wakati mahitaji ya askari katika hifadhi hiyo ni 246 waliopo ni 131 na hawana silaha za kutosha’’,anasisitiza.
Changamoto nyingine ambazo zinaikabili idara ya ulinzi katika hifadhi hiyo ni upungufu wa magari kwa ajili ya doria na kwamba magari yaliopo ni ya zamani yamechakaa hivyo kuifanya kazi ya doria kuwa ngumu  licha ya kwamba kikosi hicho kinajitahidi kutimiza wajibu wao ili kukabiliana na majangili.

No comments:

Post a Comment