-Mtihani wa Taifa unabebwa kichwani
Na
Albano Midelo
NI safari ya siku
mbili kutoka mjini Songea makao makuu ya
mkoa wa Ruvuma hadi kuweza kuifikia shule ya msingi Ndonga iliyopo wilayani
Nyasa mwambao mwa ziwa Nyasa.
Basi linaishia katika
mji mdogo wa Liuli ziwa nyasa na kutoka hapo inakulazimu kukodi pikipiki hadi
katika kijiji cha Njambe kata ya Kihagara ambapo ndiyo mwisho wa usafiri wa
pikipiki na kuanzia hapo inakulazimu kutembea kwa miguu kwa takribani saa moja
hadi kukifikia kijiji cha Ndonga.
Shule ya msingi
Ndonga imejengwa juu ya mlima wa Liwundi,unapofika katika kijiji cha Ndonga
inakulazimu kupanda mlima wenye mwinuko mkali wenye makorongo kwa takriban
zaidi ya saa moja hadi kufika kileleni ndipo unakutana na shule hii.
Asilimia 90 ya
wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Ndonga wanaishi chini ya mlima hivyo
inawalazimu kwa siku tano yaani Jumatatu hadi Ijumaa kupanda na kushuka mlima kwa saa mbili hali ambayo
imesababisha shule hiyo kukabiliwa na utoro uliokithiri kwa wanafunzi ambao
unafikia kwa siku kati ya asilimia 60 hadi 70.
Akizungumza kwa niaba
ya mwalimu mkuu,mtaaluma wa shule ya msingi Ndonga Amos Kilongo anasema shule
hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinachangia kushusha taaluma kwa
wanafunzi mwaka hadi mwaka na kwamba hakuna juhudi zozote zinazofanywa na
serikali ya kijiji wala ngazi ya wilaya kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.
“Nakupongeza sana kwa
kuweza kupanda mlima wenye muinuko mkali na kufika hapa shuleni,hatujawahi
kupokea wageni kutoka ngazi ya wilaya tangu shule hii ilipoanzishwa mwaka
1995,shule haijawahi kukaguliwa tangu mwaka 1995 ilipokaguliwa wakati
inaanzishwa’’,alisisitiza.
Sera ya elimu
inaeleza wazi kuwa kila shule ya msingi inatakiwa angalau ikaguliwe kila mwaka
kwa lengo la wakaguzi kuwakumbusha walimu na kutoa mwongozo wa ufundishaji
wenye tija na uendeshaji wa shule kulingana na maelekezo ya wizara ya elimu.
Kulingana na mwalimu
wa shule ya Ndonga,shule hiyo yenye wanafunzi 309 wanaosoma kuanzia darasa la
awali hadi la saba inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya kusomea hali
inayosababisha darasa la awali lenye wanafunzi 37 kusomea chini ya mti.
Anabainisha kuwa
shule hiyo ina vyumba vinne tu vya madarasa hali ambayo imesababisha madarasa
mawili kusomea katika chumba kimoja na kwamba kuna madarasa mawili ambayo
yameezuliwa na upepo kwa zaidi ya mwaka mmoja hayajaezekwa hali ambayo
inasababisha wanafunzi kusomea huku wakipigwa na jua na mvua.
“Mazingira duni ya
kujifunzia yaliopo katika shule hii yamesababisha utoro wa wanafunzi kufikia
kati ya asilimia 60 hadi 70 kwa siku,walimu tunafanyakazi katika mazingira
magumu ,shule ina nyumba moja tu ya mwalimu mkuu yenye vyumba vitatu ambayo
tunaishi walimu watatu na familia zetu,mimi nimeamua kuishi
jikoni kwa kuwa mwalimu mkuu ana familia kubwa hali ni mbaya’’,alisema kwa
uchungu.
Mwalimu wa taaluma
katika shule hiyo Amos Kilongo anasema hali ni mbaya kutokana na mazingira duni
yaliyopo katika shule hiyo ambapo takwimu za ufaulu kuanzia mwaka 2007 hadi
2011 zinathibitisha kiwango cha ufaulu kuwa chini ambapo shule hiyo hivi sasa
ina wanafunzi 50 wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu.
Mwaka 2011 wanafunzi
waliohitimu darasa la saba katika shule hiyo walikuwa ni 29 waliofaulu ni
wanafunzi watano kati yao wavulana ni
wanne na msichana mmoja,mwaka 2010 waliohitimu walikuwa ni 24,waliofaulu
ni wavulana wawili tu,mwaka 2009 waliohitimu
walikuwa wanafunzi 32,waliofaulu ni wanane kati yao wavulana watano na
wasichana watatu,mwaka 2008 waliohitimu walikuwa 60 waliofaulu 48 kati yao
wavulana 22 na wasichana 26.
Hata hivyo
anabainisha kuwa mwaka 2007 katika shule hiyo hapakuwepo na wanafunzi wa darasa
la saba kutokana na wanafunzi wachache waliofaulu darasa la nne ambao
waliunganishwa na darasa la tatu hivyo kuwa wanafunzi 60 waliohitimu mwaka 2008.
“Kutokana na
mazingira duni ya shule hiyo ikiwemo kijiji kukosa barabara ya kuweza kupita
gari ,kila mwaka wakati wa mitihani ya Taifa ya darasa la saba shule hiyo
imepewa route maalum ambapo gari la mitihani linaishia katika kijiji cha Njambe
na baada ya hapo mkuu wa msafara mlinzi pamoja na msimamzi wanabeba mitihani kichwani na kutembea kwa
zaidi ya kilometa saba hadi juu la mlima ambapo ipo shule hii’’,alisema.
Walimu watano wote
wanaume wanaofundisha katika shule hii wakiwemo Gorge Mbapira,Joel Makelele,Amos
Kilongo Edward Msuya na Atanas Mhagama wamekata tamaa kuendelea kufundisha katika mazingira duni ambayo
yanawakosesha huduma zote muhimu ikiwemo mawasiliano,afya,usafiri,maduka na
huduma zote muhimu.
Mratibu elimu kata ya
Kihagara Severine Ngwenya anasema shule ya Ndonga licha ya kupewa fedha za
mpango wa uboreshaji wa elimu ya msingi MMEM mwaka 2002 hadi 2005 bado
mazingira ya shule hiyo ni duni kwa kuwa hakuna chumba hata kimoja cha darasa
ambacho kimepigwa sakafu badala yake wanafunzi wanasomea kwenye vumbi.
“Hali ya shule ya
Ndonga kwa ujumla wake ni mbaya na haifai kwa kufundishia na kujifunzia,shule
haifikiki kwa gari wala pikipiki bali kwa mguu unapanda mlima kwa saa
mbili,hata wilayani hawajawahi kufika katika shule hiyo’’,alisema.
Edward Ndunguru afisa
mtendaji wa kijiji cha Ndonga anaitaja mikakati ambayo inachukuliwa hivi sasa
na kijiji hicho ni kufyatua tofali 200,000 hata hivyo tofali zilizofyatuliwa ni
60,000 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa na nyumba za
walimu katika shule hiyo.
Mbunge wa jimbo la
Mbinga mashariki Kapt.John Komba ambaye shule hiyo ipo katika jimbo lake
amekiri kijiji cha Ndonga kuwa ni miongoni mwa vijiji ambavyo vinamsumbua
kichwa,hata hivyo amesema yupo tayari kusaidia kutoa vifaa vyote vya ujenzi wa
shule hiyo iwapo wananchi watakubali kuihamisha
shule kutoka mlimani na kuijenga eneo
linalofikika kirahisi.
Afisa elimu msingi
katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga David Mkali ambaye anawajibika katika
wilaya ya Nyasa amesema ameandaa takwimu za mapungufu mbalimbali yaliojitokeza
katika shule za msingi ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa,madawati,walimu
na nyumba za walimu kisha kuweka mpango mkakati wa kukabiliana na matatizo
hayo.
“Natambua changamoto
zinazoikabili shule ya msingi Ndonga,kijiografia shule hiyo haifikiki hali
ambayo inasababisha wakaguzi kushindwa kwenda kuikagua kila mwaka hata wakati
wa mitihani inakuwa na route maalum,shule kuihamisha toka mlimani ni gharama
kubwa sio jambo rahisi inawezekana ukawa mpango wa muda mrefu’’,alisema Afisa
elimu.
Afisa elimu huyo
ameitaja mikakati mingine ya kuinua kiwango cha ufaulu kuwa ni kuzitembelea
shule za msingi kwa kushirikiana na idara ya ukaguzi wa shule ili kufuatilia
utendaji kazi wa walimu na kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitafutia
ufumbuzi wa kudumu.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

No comments:
Post a Comment