Na
Albano Midelo
SERIKALI kupitia
wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi iliamua kuanzisha mfumo wa elimu ya awali
katika shule za msingi kwa lengo la kuwaandaa watoto wenye umri kuanzia miaka
mitano.
Wizara ya elimu
imedhamiria kuhakikisha kuwa watoto wenye umri wa miaka mitano hadi sita
wanasoma darasa la awali kabla ya kuanza kuingia shule ya msingi wanapokuwa na
umri wa miaka saba.
Uchunguzi uliofanywa
katika kata za Kihagara na Liuli umebaini kuwa madarasa ya awali katika shule
hizo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali hali ambayo inaathiri utoaji wa
elimu hiyo muhimu kabla ya kuanzia shule za msingi.
Mwalimu wa taaluma
katika shule ya msingi Ndonga kata ya Kihagara Amos Kilongo anasema shule hiyo
ina darasa la awali lenye wanafunzi 37 ambao wanasomea kwenye mti kutokana na
kukosekana kwa chumba cha darasa na kwamba mwalimu anayefundisha katika darasa
hilo ni aliyemaliza kidato cha nne.
“Wanafunzi wa darasa
la awali hawana darasa wanasomea chini ya mti,pia darasa halina madawati wa awali
wanakaa wakati wa mvua wanafunzi hao
wanasome katika kanisa katoliki ambalo tumewaomba wamiliki wa kanisa hilo wamekubali
kutusaidia’’,alisisitiza.
Mwalimu mkuu wa shule
ya msingi Kihagara Anet Ngindo anasema shule hiyo ina darasa la awali lenye
wanafunzi 52 ambao wanasomea chumba cha shule ya msingi wakifundishwa na
mwalimu ambaye hajapata mafunzo ya ualimu na sio mwajiriwa analipwa posho
kupitia michango inayochangwa na wazazi.
Mwalimu mkuu katika
shule ya msingi Tumbi Evaristo Ndiwu
anasema katika shule yake kuna darasa la awali lenye watoto 45 ambalo halina
chumba cha kusomea ambapo mwalimu wake hana taaluma ya ualimu ni mhitimu wa
kidato cha nne analipwa posho kutokana na michango ya wazazi na walezi.
Katika shule ya
msingi Mango,mkuu wa shule hiyo anasema katika shule yake kuna darasa ka awali
lenye wanafunzi 60 ambao hawana chumba cha kusomea na wanafundishwa na mwalimu ambaye hajapata
mafunzo ya ualimu sio mwajiriwa badala yake analipwa posho na wazazi kati ya
shilingi 30,000 hadi 50,000 kwa mwezi.
Mwalimu mkuu wa shule
ya msingi Ngehe Silivanus Mbeya anasema katika shule yake kuna darasa la awali
lenye watoto 36 ambalo halina chumba cha kusomea na linafundishwa na mwalimu
ambaye amehitimu kidato cha nne hana mafunzo ya ualimu analipwa posho na wazazi
ambayo haikidhi mahitaji ya mwalimu huyo.
Katika shule ya
msingi Puulu mwalimu mkuu wa shule hiyo
Cathibert Maluka anasema katika shule yake kuna darasa la awali lenye wanafunzi
90 na kwamba wanafunzi hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo na
ukosefu wa madawati ambapo wanafunzi wote wanasoma kwa kukaa chini.
“Darasa la awali
katika shule yetu limebahatika kuwa na walimu wawili ambao wamepata mafunzo
rasmi ya kufundisha wanafunzi wa darasa la awali hali ambayo inawawezesha kutoa
elimu ya awali kulingana na malengo ya wizara ya elimu licha ya wanafunzi
kusomea chini’’,alisema .
Mwalimu mkuu wa shule
ya msingi Nkali Erasmus Haule anasema
shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 210 ina darasa la awali lenye wanafunzi 45
ambao hawana darasa badala yake wanasomea kwenye banda ambalo jioni linatumika kama klabu cha pombe
na kwamba mwalimu anayefundisha hajasomea.
Katika shule ya
msingi Hongi kwa mujibu wa mwalimu mkuu
Simon Ndunguru shule hiyo ina darasa la awali lenye wanafunzi 52 changamoto
kubwa hakuna chumba maalum cha kusomea na kwamba mwalimu anayefundisha sio
mwajiriwa na wala hajasomea kufundisha darasa la awali.
Katika shule ya
msingi Mwongozo yenye wanafunzi 654 inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa darasa
la awali lenye watoto 81 halina sakafu lina mwalimu mmoja ambaye hana mafunzo
ya ualimu ,hajaajiriwa analipwa posho na wazazi wenye watoto hao
Baadhi ya wadau wa
elimu katika kata za Kihagara na Liuli ambao ni Neema Msumba,John Ndunguru,Joel
Makelele,Melikion Mapunda na Victor Komba wametoa wito kwa serikali kuhakikisha
kuwa kila shule ya msingi inajenga darasa rasmi kwa ajili ya elimu ya awali
badala ya shule nyingi kutumia vyumba vya shule ya msingi.
Wameitaka wizara ya
elimu na mafunzo ya ufundi kuhakikisha kuwa kila darasa la awali inapeleka
walimu waliopata mafunzo rasmi ya namna ya kufundisha watoto wa awali badala ya
tabia ambayo inafanywa na shule nyingi kuwatumia vijana ambao wamehitimu kidato
cha nne huku wakiwa hawajapata elimu ya ualimu.
Mratibu elimu kata ya
Liuli Abrahamu Challe amesema kata yake imejipanga kuhakikisha kuwa changamoto
zote zinazoikabili elimu ya awali katika kata yake yenye shule saba
zinatafutiwa ufumbuzi haraka ikiwemo kuwa na chumba rasmi kwa ajili ya
awali,walimu na madawati.
Challe ametoa wito
kwa serikali kutumia mfumo wa uboreshaji wa elimu ya awali kama ilivyokuwa kwa
uboreshaji wa elimu ya msingi na sekondari kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa kwa kila shule na
kusisitiza kuwa vifaa vyote vya ujenzi vitolewe na serikali na wananchi waachie
ujenzi.
Afisa elimu msingi
katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga David Mkali ambaye anahusika na wilaya
ya Nyasa anasema elimu ya awali ni sera ya wizara ya elimu kuhakikisha kila
shule ya msingi inakuwa na darasa la awali kwa lengo la kuinua elimu hapa
nchini.
Ameahidi kushirikiana
na viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani,watendaji wa
vitongoji,vijiji,kata,tarafa pamoja na wenyeviti wa vijiji kuhakikisha
wanahamasisha wananchi katika maeneo yao kusimamia ujenzi wa madarasa ya awali
na kutengeneza madawati ili watoto hao waweze kusoma katika mazingira bora.
“Ni ukweli madarasa
ya awali yaliyo mengi yanafundishwa na walimu wasiopata elimu ni kutokana na
uhaba mkubwa wa walimu uliopo katika shule nyingi nchini,lengo ni kuhakikisha
tunapata walimu wa kutosha ikibidi hata kuwatumia walimu wanaostaafu kufundisha
katika madarasa ya awali’’.alisisitiza.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

No comments:
Post a Comment