Na Albano
Midelo
SEKTA ya utalii inachangia pato kubwa
la taifa kutokana na uwepo wa vivutio vingi vya utali vilivyopo katika maeneo
mbalimbali nchini kama vile hifadhi za Taifa,mapori ya wanyamapori,milima,maziwa,fukwe
,maeneo ya kihistoria, pamoja na vivutio vingine vingi.
Mapato yanayotokana na utalii hapa
nchini yanaweza kuongezeka zaidi endapo vivutio vilivyopo vitaboreshwa na
kutangazwa kwa nguvu zote ndani na nje ya nchi ili kuwavutia watalii wengi wa
ndani na nje.
Matangazo ya vivutio mbalimbali vya utalii katika vyombo vya habari vya kitaifa na
kimataifa yatawezesha vivutio hivyo kufahamika kitaifa na kimataifa hivyo idadi
ya watalii kuendelea kuongezeka mwaka
hadi mwaka na kuliingizia taifa mapato makubwa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani
ambazo zimebahatika kuwa na hifadhi nyingi za Taifa zikiwemo hifadhi ya Taifa
Arusha,Gombe,Katavi,mlima Kilimanjaro,Mahale,Mikumi,Ziwa Manyara, Ruaha,
Rubondo, Serengeti, Saadan, Tarangire, Udzungwa, Kitulo,Mkomazi na Saanane.
Katika hifadhi za wanyamapori hapa
nchini kuna wanyama kama vile simba, tembo, chui, pundamilia,nyati,nyumbu,faru
pamoja na ndege wa aina mbalimbali ambao ni kivutio cha utalii ingawa wanyama
hao wanapatikana katika hifadhi nyingine duniani.
Ukiachana na wanyama hao Tanzania pia
imebahatika kuwa na wanyama wenye kivutio cha kipekee na ni adimu kwa kuwa
hawapatikani kirahisi hali ambayo inasababisha wanyama hao kuwa na soko kubwa
kwa watalii.
Miongoni mwa wanyama hao ambao hawapatikani
kirahisi ni mnyama anayeitwa sokwe ambao hapa nchini wanapatikana kwa wingi
katika hifadhi ya Gombe na milima ya
Mahale mkoani Kigoma.
Hata hivyo inaelezwa na watafiti wa
wanyama hao ambao wanafanana na binadamu
katika tabia kwa asilimia 98 pengine ndiyo maana wanaitwa sokwe mtu kwamba hivi sasa sokwe wanatoweka kwa kasi kubwa
ulimwenguni hali ambayo inaleta hofu kubwa ya wanyama hao kutoweka na kufutika katika
uso wa dunia.
Watafiti wanabainisha kuwa Sokwe au sokwe mtu
ni mnyama ambaye alibakiza asilimia mbili tu angeweza kufanana na binadamu
kitabia kwa asilimia 100 ambapo hivi sasa anafanana kwa asilimia 98 hali ambayo
inamfanya mnyama huyu kutafutwa kwa udi na uvumba baada ya kuwa kivutio adimu
na cha kipekee cha utalii.
Baadhi ya nchi ulimwenguni tayari
zimetangaza hali ya hatari kuhusu kutoweka kwa mnyama huyo katika nchi zao
ambaye ni kivutio cha kipekee cha watalii hasa kutokana na mnyama huyo kuwa na
tabia za kibinadamu.
Kutokana na mnyama huyo kutoweka
katika sehemu mbalimbali nchini,Tanzania hivi sasa inapokea watalii wengi ambao
wanafika hapa nchini kwa lengo la kumtafuta mnyama huyu na kuweza kumuona
katika hifadhi ya Gombe na milima ya Mahale mkoani Kigoma.
Wanyama hao wakiwa katika hifadhi ya
Gombe wanaendelea kuzaliana na kuendeleza kizazi chao hasa baada ya wahifadhi
na watafiti kuwatunza na hivyo kuendelea kuwepo katika uso wa dunia kwa ajili
ya maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mhifadhi wa wanyamapori Richard Nchasi
anasema utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa sokwe mtu anaweza kuishi kati ya
miaka 40 hadi 50 na kwamba sokwe mtu wanaotunzwa katika bustani maalum wanaweza
kuishi hadi miaka 60.
“Sokwe mtu hupevuka anapofikisha umri
wa miaka kati ya tisa hadi 13 na huzaa baada ya kufikisha umri wa miaka kati ya
15 hadi 16,uzito wa sokwe mtu ni hadi kilo 120’’,alisema mhifadhi Nchasi.
Kulingana na mhifadhi huyo,sokwe mtu
wanaishi kwa kutegemea vyakula ambavyo vinatokana na mimea kama vile
ndizi,matango,matikiti,karoti,mchicha na matembele.
Watafiti na wahifadhi wa sokwe katika
hifadhi hiyo wanasema wamekuwa wanafanya utafiti wa wanyama hao tangu asubuhi
hadi jioni na hivyo kuchunguza tabia zao mbalimbali wanazozionesha.
Mhifadhi
kutoka hifadhi ya Gombe Noelia Mnyonga anasema hifadhi ya
Taifa ya Gombe ni ndogo kuliko zote nchini ikiwa na jumla ya
kilometa za mraba 52 tu ,hata hivyo hifadhi hiyo inapata umaarufu mkubwa kwa
kuwa na makazi machache yaliosalia ya
sokwe ulimwenguni.
Mnyonga anabainisha kuwa hifadhi ya
Gombe ipo umbali wa kilometa 16 kaskazini mwa mji wa Kigoma ikiwa katika ukanda
mwembamba wa msitu unaokatizwa na miteremko mikali inayoingia katika mwambao
mwa ziwa Tanganyika.
Hata hivyo anasema hifadhi ya Taifa ya
Gombe ilipata umaarufu duniani baada ya mtafiti wa tabia za sokwe duniani
Dk.Jane Gooddall kufanya utafiti kuhusu maisha na tabia ya sokwe wa Gombe kwa
muda wa miaka 40 na kuandika vitabu kadhaa kuhusu wanyama hao.
Mmoja wa watafiti wa mnyama huyo Issa Salala anasema kuwa sokwe katika hifadhi hiyo wakiwa na afya njema wanakuwa wachangamfu,anayataja
magonjwa ambayo yanaongoza kuwashambulia sokwe kuwa ni mafua ambayo
yanawaathiri sana wanyama na wasipotiwa haraka husababisha vifo kwa sokwe hao.
Hata hivyo anasema kwa kawaida
inapogundulika ugonjwa wa mafua umemshika sokwe,watalaamu wa afya za wanyama
wanachukua hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa mnyama huyo anapata matibabu
haraka ili kunusuru maisha ya mnyama huyo adimu ulimwenguni.
Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika hivi
karibuni katika hifadhi za Gombe,Mahale na Kibondo zimebaini kuwa sokwe mtu
katika hifadhi hizo wanafikia 2000 ukilinganisha na idadi ya sokwe mtu karibu
4000 waliokuwepo miaka kumi iliyopita na kwamba sokwe mtu akizaa ananyonyesha
kwa miaka miwili na wanazaa kila baada ya miaka minne hadi mitano.
Hifadhi ya Taifa ya Gombe ukiachia
kuwa na sokwe,lakini pia hifadhi hiyo ina wanyama wengine wakiwemo kima wenye
mikia myekundu na kima wa bluu hali
ambayo inawafanya watalii wanaoingia ndani ya hifadhi hiyo kuwa salama kwa
safari za miguu kwa kuwa hakuna wanyama jamii ya paka kama simba na chui.
Kwa upande wa hifadhi ya Taifa ya
Mahale iliyoundwa na vilima vilivyojipanga na kufunikwa na misitu minene ni hifadhi jirani na Gombe na inapakana na
ziwa Tanganyika ikiwa na kilometa za mraba 1613 ni hifadhi yenye makazi ya
jamii adimu zilizobakia za sokwe barani Afrika.
kaimu mkurugenzi mkuu wa Hifadhi za
Taifa TANAPA Ahmed Mbugi anasema katika hifadhi ya Taifa ya Mahale kundi kubwa la sokwe huonekana katika vilima
na mabonde ambapo mabaki ya matunda yaliyoliwa na kinyesi kibichi ni miongoni
mwa vitu vitakavyowaongoza watalii hadi kuwafikia viumbe hawa adimu.
“Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi za
Taifa Gombe na Mahale ni wakati wa kiangazi kati ya mwezi Julai hadi Oktoba kwa
kuwa sokwe hawapendi kutembea nyakati za mvua’’,anasisitiza Mbugi.
Mtalii anaweza kwenda katika hifadhi ya Taifa
ya Gombe na Mahale kwa usafiri wa anga,nchi kavu na reli hadi mjini Kigoma
kisha kupanda boti kuvuka ziwa Tanganyika hadi makao makuu ya hifadhi hizo.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

Inapendeza pale tunapoendelea kuzitangaza hifadhi hizi....
ReplyDelete