Friday, April 26, 2013

Bonde la Songwe mbioni kugeuka jangwa



 Na Albano Midelo
Mto Songwe unaomwaga maji ziwa Rukwa ukiwa katika hatari


TANGU mwaka 1961 hadi 1970 Bonde la Songwe wilayani Chunya mkoani Mbeya  lilikuwa ni ardhi oevu,yenye uoto wa kijani na msitu mnene wenye miti mbalimbali ya asili.

 Wakati huo  wakulima waliweza kuzalisha mazao ya chakula kwa wingi kutokana na bonde kuwa na ardhi oevu yenye maji yaliokuwa yanatiririka kutoka mto Songwe ambao unaanzia milima ya Umalila Mbeya na kumwaga maji yake ziwa Rukwa  .

 Bonde la Songwe ambalo linaundwa na kata za Totowe,Galula,Namkukwe,Kanga na Mbuyuni wakati huo lilikuwa linavutia maisha ya viumbehai wakiwemo binadamu, wanyamapori na  ndege wa aina mbalimbali ambao walikuwa wanaimba kwa furaha.

 Mtu ambaye alifika kwenye bonde la Songwe miaka ya 1970 akitembelea leo kwenye bonde hilo hawezi kuamini kwa kile ambacho atakiona kutokana na mabadiliko makubwa ya  kimazingira ambayo yamejitokeza hivi sasa na kutaharisha maisha ya  viumbe hai.


Katika bonde la Songwe hivi sasa miti imetoweka na ardhi imebaki uchi,mto Songwe ambao ndiyo mto pekee unaomwaga maji yake ziwa Rukwa kwa mwaka mzima upo katika hatari ya kutoweka,ziwa Rukwa limesinyaa kuwa dogo na kina chake kinapungua kwa kasi.

 Miti karibu yote iliyokuwa kivutio katika Bonde la Songwe haipo tena,Bonde  limejaa makorongo makubwa ambayo yanatokana na mmomonyoko wa ardhi,vumbi zito na  vimbunga vya mara kwa mara limekuwa ni jambo la kawaida katika bonde hili.

 Unapofika kwenye bonde hili kuanzia mwezi wa Aprili hadi Novemba utaona upepo wenye vumbi zito ambao unaweza kudhani mvua inataka kunyesha,vumbi hilo huwa zito kiasi kwamba huwezi kumuona mtu aliye mbele yako.Hali hii inawafanya wakazi wa Bonde hilo kujifungia ndani ya nyumba zao kuepukana na vumbi hilo.

 Vumbi hilo  ambalo unaweza kuliita mvua ya vumbi huchukua kati ya saa nne au siku nzima,hali ambayo huleta kero kwa wakazi kushindwa kuwajibika ipasavyo katika kazi mbalimbali za kiuchumi,kijamii na burudani.

  Katika Bonde la Songwe wakulima  waliweza kulima mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, alizeti, ufuta, mtama,viazi vitamu,mpunga bila kuweka mbolea ya chumvichumvi,hivi sasa  Bonde hilo linakabiliwa na njaa kila mwaka kutokana na ukame unaotokana na bonde kukosa mvua za uhakika.

Ziwa Rukwa kwenye bonde hili,tangu uhuru limetoa ajira katika sekta ya uvuvi ambapo wavuvi wameweza kusomesha watoto wao,kujipatia kipato kwa kuuza samaki na kupata kitoweo ambacho kinajenga afya kutokana na samaki wanaopatikana kwenye ziwa hilo.

Moja ya fukwe ziwa Rukwa upande wa Bonde la Songwe imekauka kilometa nane
Hata hivyo maisha ya wakazi wa Bonde hili yapo hatarini baada ya athari za kimazingira kuanza kujitokeza kutokana na uharibifu wa mazingira ikiwemo kuanza kusinyaa kwa vyanzo muhimu vya maji ambavyo ni mto Songwe na ziwa Rukwa .

Wakati wa masika maelfu ya tani za mchanga,tope na takataka nyingine  husombwa  na kuingia mto Songwe na kupelekwa  ziwa Rukwa hali ambayo inasababisha kina cha maji cha mto na ziwa kupungua  kwa kasi.

 Athari hizo za kimazingira zinachangiwa na   idadi kubwa ya mifugo ambayo inaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa kwenye Bonde la Songwe huku wafugaji hao wahamiaji kutoka kanda ya ziwa wakifanya uharibifu wa mazingira kwa kufyeka miti ovyo kwa lengo la kujipatia kuni,mkaa na mashamba.

 Afisa mifugo,kilimo na ushirika katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya Adamu Mbale  anasema idadi ya ng,ombe katika bonde zima kati ya mwaka 1961 hadi 1970 ilikuwa ni 800 tu hali iliyosababisha mazingira katika bonde hilo kuwa ya kuvutia.

 Mbale anabainisha kuwa idadi ya ng’ombe kwenye Bonde hilo iliongezeka kwa kasi na kuathiri mazingira  katika kipindi cha kuanzia mwaka 1981 hadi 1990 ng’ombe walifikia 173,681,mwaka 2000 ng’ombe walifikia 186,800 na hadi kufikia mwaka 2010 idadi ya ng’ombe ilifikia 286,800.

 Mbale anasema eneo linalofaa  kwa ajili ya malisho wilayani Chunya ni hekta 1,353,300 na kwamba eneo ambalo limepimwa na kutengwa kwa kwa ajili ya  malisho ni 622,397.

 Diwani mstaafu na mwenyekiti wa kamati ya mazingira Bonde la Songwe William Mahenge anabainisha kuwa wafugaji  katika bonde hilo wanamiliki makundi makubwa ya ng’ombe kati ya 200 hadi 5000 kwa mfugaji mmoja  na kusisitiza kuwa  mifugo ni sababu kubwa ya mazingira ya bonde hilo kuharibika.

 Mifugo mingi imesababisha fukwe za ziwa Rukwa upande wa Bonde la Songwe zilizopo kwenye vijiji vya kata ya Totowe   kukauka na kusababisha ziwa hilo kupungua  ukubwa na kina hali inayohatarisha uwepo wa ziwa hilo ambalo linashika nafasi ya nne kwa ukubwa hapa Tanzania likitanguliwa na maziwa ya  Tanganyika,Viktoria na Nyasa.

 Fukwe ambazo zinapotea kwa kasi ni pamoja na fukwe ya Handeni ambayo imekauka kwa kilometa 10,Ihovyo kilometa tatu,Mtanda kilometa saba,kisiwani kilometa tisa,kambipotea kilometa tano,Kwaboko  kilometa sita na fukwe ya Mchangani kilometa tano.Kina cha maji katika fukwe hizo  hivi sasa ni chini ya  meta moja .

 “Fukwe hii ya kisiwani mwaka 1998 ilikuwa kilometa nane kutoka hapa ,unaweza kutembea katika kina cha maji chini ya magoti hadi umbali wa meta 300 ndani ya ziwa,hali hii ikiendelea ziwa hili linaweza kukauka au kuwa bwawa ’’, anasema John Mwakyoma mvuvi katika ziwa Rukwa.

 Peter Sasawata na Stanley Rwamba  ni wavuvi katika fukwe ya Mtanda wanasema fukwe hiyo mwaka 1994 ilikuwa kilometa saba kutoka hapo ilipo leo na kwamba chanzo kikuu cha kukauka kwa fukwe ni mifugo mingi ambayo inaingia kunywa maji na kula malisho ndani ya ziwa kila siku.

 “Mimi nimeishi katika kijiji cha Ihovyo kwa miaka 11 wakati nafika hapa maji ya ziwa hili ulikuwa unayakuta baada ya kutembea kwa dakika tano tu lakini hivi sasa inakulazimu kutembea zaidi ya saa mbili ndipo unalikuta ziwa ’’,anasema Beston Mwambene mwalimu wa shule ya  msingi Ihovyo .

 Mwambene anabainisha kuwa Kupungua kwa kina cha maji  kisanyasi kunasababisha ukubwa wa ziwa Rukwa kupungua,kina kikiwa kifupi ziwa litaongezeka kwa muda kisha litarudi nyuma kwa kasi  na kwamba kuongezeka kwa joto kutasababisha kiasi kikubwa cha maji kupotea kwenda angani  hatimaye ziwa hilo linaweza kuwa bwawa.

 “Kama kweli serikali inataka kuliokoa bonde la Songwe lisigeuke jangwa na ziwa Rukwa lisipotee kwenye uso wa Dunia,waache kuendekeza siasa kwenye mazingira, ziwa Rukwa litakauka, wakulima wanazidi kusogeza mashamba ya mpunga kwenye fukwe za ziwa’’,anasisitiza Mwambene.

 Kuwepo kwa mifugo mingi kwenye Bonde la Songwe sio tu kumechangia kuleta athari za kimazingira kwenye bonde hilo,bali pia kumesababisha migogoro kati ya wafugaji na wakulima.

Migogoro hiyo imesababisha majeruhi na vifo kwenye bonde hilo kwa mfano mwaka 2006 wafugaji watano walikufa  na wengine 11 kujeruhiwa vibaya katika kijiji cha Totowe bonde la Songwe.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Totowe Paskalia Luwi anasema wafugaji walifikwa na mauti hayo kutokana na chuki ya muda mrefu iliyojengeka kutokana na tabia yao ya kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.

Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro katika kukabiliana na uingizaji wa mifugo ametoa wito kwa   wakuu wa wilaya tisa zinazopakana na wilaya yake wasitishe utoaji wa vibali vya kusafirishia mifugo hasa Ng'ombe wanaoingia wilayani humo.



  

Afisa wa bonde la maji la Rukwa  Idris Msuya anasema“mifugo iliyopo ziwa Rukwa inatisha hata mimi mwenyewe nilipoiona mara ya kwanza ilinichanganya,nimeshuhudia  maelfu ya mifugo  ambayo inaishi, kula na kunywa  maji  ziwa Rukwa kwenye fukwe za kijiji cha Totowe.hali hii inatisha’’,anasema.

 Hata hivyo Msuya anakiri kina cha maji cha ziwa Rukwa kinaendelea kupungua mwaka hadi mwaka kutokana na uharibifu wa mazingira unaochangiwa  na idadi kubwa ya ng’ombe katika wilaya zinazozunguka ziwa Rukwa ambazo alizitaja kuwa ni Chunya, Mbeya, Sumbawanga, Mpanda, Mbozi na Nkasi.

Kulingana na Msuya, Ziwa Rukwa hivi sasa lina wastani wa kina cha juu cha maji cha mita 800, kina cha chini ni mita nne , eneo la maji la ziwa hilo ni  kati ya kilometa 800 hadi 2300 kutegemeana na kiasi cha  mvua inayonyesha.

Makamu wa Rais Dk.Mohamed Ghalib Bilal akizungumza katika moja ya siku ya mazingira duniani alisema  baadhi ya gharama za uharibifu wa mazingira  tumekwishaanza kuzibeba  ambapo  kutokana na uharibifu huo vina vya maji katika mabwawa, mito na maziwa  vimekuwa vikishuka.

Utafiti tayari imebaini kuwa katika kipindi cha mwaka  1970 hadi 2006 Ziwa Rukwa limepungua kwa kiasi cha zaidi ya kilomita saba, kina na ukubwa wa ziwa Manyara umepungua kwa asilimia 65, na ukubwa wa Ziwa Jipe umepungua kwa asilimia 65.

Ni dhahiri kuwa, hatuwezi kuitazama miaka 50 ijayo kwa matumaini bila kutafakari hali ya mazingira. Hali hii isipodhibitiwa haraka, mifumo ya mvua itabadilika, vyanzo vya maji vitakauka, ubora wa maji utaathirika, bioanuai itatoweka, maeneo mengi yatakuwa kame.

No comments:

Post a Comment