![]() |
| Mto Lunyere ambao maji yake yamechafuliwa na zebaki kutoka migodini |
Na Albano Midelo
MAISHA ya wakazi wa kata za Tingi na
Liparamba katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, yako hatarini.
Wanakunywa maji ya mto Lunyere ambayo
yamechanganyika na kemikali ya zebaki (mercury) inayotumiwa katika kusafisha
dhahabu.
Tayari wataalam wametamka kuwa maji ya
Lunyere “hayafai kwa matumizi ya binadamu na viumbe hai vingine.”
Takwimu zilizopatikana makao makuu ya
kata hizi mbili zinaonyesha kuna watu wapatao 25,000 katika vijiji vyake 16
ambavyo vinatumia maji ya mto Lunyere.
Wachimbaji wadogo wa dhahabu
huchenjulia madini yao katika mto Lunyere na wengine katika vijito vinavyoingia
katika mto huo unaotiririkia mto mkubwa, Ruvuma.
Getruda Payovera, ambaye ni afisa wa
maabara wa Wizara ya Maji, ofisi za kanda ya Songea, ana kile kinachoweza
kuitwa “ujumbe kwa watu wote.”
Anasema zebaki ikinywewa kwenye maji au
kuvutwa kwa pumzi, yaweza kuingia moja kwa moja kwenye damu na “...inakwenda
kutua kwenye ubongo na kusababisha ubongo kusimama...”
Mwaka 2009 wataalam walifanya uchunguzi
wa maji ya mto Lunyere, kutoka kitongoji cha Songeapori.Uchunguzi ulifanywa na
taasisi za Water Laboratory Unity na Chemical and Environmental Services za
jijini Dar es Salaam.
Matokeo yake ambayo mwandishi
ameonyeshwa, yalionyesha wazi kuwa maji ya mto Lunyere yana “kiwango kikubwa na
cha kutisha” cha kemikali ya zebaki inayoweza kuua binadamu na viumbehai
vingine.
Kiwango cha kemikali ya zebaki
kilichoelezwa kuwa “ni kikubwa na cha kutisha,” kimewekwa kwa vipimo vya
kitaalam kuwa ni Hg/ug 0.02.
Maji salama kwa matumizi ya binadamu na
viumbe vingine hai, ameeleza Payovera, yanapaswa kuwa na kiwango cha zebaki cha
mg/n.m (mercury not mentioned), yenye maana kwamba hakuna kabisa
kemikali ya zebaki katika maji.
Taasisi za uchunguzi zilibaini pia kuwa
maji ya mto Lunyere yana kiwango kikubwa cha taka/tope ambacho kinavuka kiwango
kinachokubalika kitaifa na hata cha Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kiwango cha taka ambacho kinakubalika
kitaifa kinaelezwa kitaalam kuwa ni etu 30; kiwango cha kimataifa
ni etu 5 – 25. Lakini maji ya Lunyere yana etu 1,141, jambo
ambalo Payovera ameeleza kuwa “ni hatari sana.”
Uchimbaji dhahabu wa mtu mmojammoja
ulianza mwaka 2004 katika kijiji cha Darpori na ndio mwanzo wa uchafuzi wa mto
Lunyere kwa kemikali ya zebaki.
Uchafuzi umeenea katika vyanzo vya maji
vilivyopo kwenye milima ya Sufuri A na Namba Tisa, nchini Msumbiji na katika
kijiji cha Darpori kilichopo mpakani, upande wa Tanzania.
Mto Lunyere hupita katika hifadhi ya
wanyamapori ya Liparamba inayounganisha Tanzania na Msumbiji, kisha kuungana na
mto Ruvuma na kumwaga maji yake katika Bahari ya Hindi.
Mwandishi aliingia nchini Msumbiji hadi
kijiji cha Mpapa kilichopo kata ya Lupilichi mkoa wa Lichinga na kuona vyanzo
vya mto Lunyere katika vilima vya Sifuri A.
Katika vijiji vya Mpapa, Kitonga na
Namba Tisa, wachimbaji wanasafishia vifaa vyao vya uchenjuaji dhahabu, vyenye
kemikali, katika mto Lunyere.
Wilbert Mahundi, mwenyekiti wa Mfuko wa
Wachimba Madini (Tanzania Mineral Mining Trust Fund – TMMTF), anasema
zebaki inaweza kusababisha kansa ya tumbo, ini, koo na ngozi.
Anasema zebaki ni nzito, haiyeyuki kwa
urahisi na hugota chini ya vyanzo vya maji kama mto na kuvutia viumbehai kama
samaki kuila.
Mtaalamu katika Shirika la Utafiti na
Maendeleo Tanzania (TIRDO) anayehusika na mazao ya mizizi, Anselimo Moshi,
anatahadharisha kuwa mazao ya mizizi, kama vile muhogo, yasilimwe karibu na
maeneo ya machimbo ya madini au mabondeni ambako zebaki inatumika na
kutiririkia kwenye maji.
Anasema zebaki hufyonzwa kwenye maji
hayo na huweza kuwa na madhara yaleyale kama iliyonywewa kwenye maji au kuliwa
kwenye samaki.
Uvundikaji mihogo kwenye maji ili
kutengeneza makopa, anaeleza Moshi, haustahili kutumia maji yenye zebaki kwani
huweza kubakiza sumu ndani ya chakula hicho.
| Wachimbaji madini wakiwa mgodini Dapori Mbinga |
Dk. Salla Paul, mkuu wa Chuo cha
Maofisa Tabibu, Songea anataja baadhi ya dalili za aliyeathirika kwa zebaki
kuwa ni pamoja na mwili kuwa na vidonda vya mara kwa mara, ukurutu, kupoteza
kumbukumbu, macho kupoteza uwezo wa kuona na homa za matumbo.
Dalili nyingine ambazo zinatajwa pia na
Dk. Joseph Mapunda wa chuo hicho, ni viganja vya mikono na wakati mwingine
mwili mzima kuwa na rangi ya njano; mwili kukosa nguvu, kukosa hamu ya kula,
kuongezeka kwa mapigo ya moyo, kutapika, maumivu ya kichwa ya mara kwa mara,
kwikwi na kiu isiyoisha.
Kuhusu samaki, Wilbert Mahundi anasema
mfumo wa chakula wa samaki hauna uwezo wa kuyeyusha zebaki; kwa hiyo kama
anakunywa kemikali hiyo, basi sumu inaendelea kubaki mwilini mwake siku zote.
Amesema, mtu ambaye atakula samaki
mwenye zebaki, anaweza kupata madhara kwa kuwa “utayarishaji samaki kwa ajili
ya chakula, iwe kwa kupika au kuchoma, hauna uwezo wa kuondoa kabisa zebaki
ndani ya samaki.”
Mbali na binadamu, maji yenye kemikali
ya zebaki kutoka vijito vya Mkurusi na Mihomba na yanayoingia Lunyere,
yanatumiwa na wanyama katika hifadhi ya wanyamapori ya Liparamba na viumbe hai
walioko katika mito hiyo.
Miongoni mwa wachimba dhahabu
wanaochangia sumu katika mito Lunyere na Ruvuma, ni Watanzania wapatao 10,000
walio katika machimbo madogo ya dhahabu nchini Msumbiji.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Darpori
kilichopo kata ya Tingi, wilayani Mbinga, Rafael Mapunda anasema tangu ameanza
kutoa vibali vya kuruhusu Watanzania kuingia nchini Msumbiji kwa ajili ya
kuchimba na kununua dhahabu, “takwimu zangu zinaonesha wamevuka wachimbaji
wanaokaribia 10,000.”
Awali, wachimbaji wengi walikuwa katika
kijiji cha Darpori chenye vitongoji vya Lunyere, Songeapori, Tanzania One na
Njarambe.
Serikali mkoani Ruvuma ilipotumia nguvu
za sheria kuzuia matumizi ya zebaki, wananchi wengi wakakimbilia Msumbiji
ambako hakuna katazo la uchimbaji kwenye vyanzo vya mito.
Shughuli zote za uuzaji na ununuzi wa
madini kutoka Tanzania na Msumbiji, zinafanywa na raia wa nchi zote mbili
katika kijiji cha Darpori.
Mwandishi aliwakuta wachimbaji, katika
vikundi vya watatu au wanne, kwenye kitongoji cha Songeapori upande wa
Tanzania, ambao wanaendelea kuchimba dhahabu na kutumia zebaki katika
kuisafisha. Maji yenye zebaki yanatiririkia mtoni Lunyere. Uchafuzi wa mto
Lunyere unafanywa na wananchi wa Tanzania na Msumbiji.
Ngwatura Ndunguru, afisa mkuu mstaafu
katika wizara ya maliasili na utalii; na aliyewahi kuwa mbunge Mbinga
Mashariki, anasema ufumbuzi wa uchafuzi wa Lunyere sharti ufanywe kwa kuhusisha
nchi zote mbili.
Anapendekeza kila nchi kuchukua hatua
za kuzuia uchafuzi, lakini anasema itabidi mikataba ya maji ya kimataifa
itumike ili kupata ufumbuzi wa uchafuzi wa Lunyere na hatimaye mto Ruvuma
ambamo yanatemwa maji yenye kemikali hatari.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766363129

No comments:
Post a Comment