Na Albano Midelo
MGOGORO mpaka wa ziwa Nyasa
kati ya Tanzania na Malawi umeimarisha mshikamano kwa wananchi wa nchi hizo
mbili ambao wanaishi mpakani Kiongozi limebaini.
Baadhi ya wananchi wanaoishi
mwambao mwa ziwa Nyasa katika maeneo ya Mbambabay,Liuli na Kihagara wamesema
mgogoro ambao unaendelea kuzungumzwa na viongozi wa kitaifa baina ya Tanzania
na Malawi umesababisha mahusiano yao maeneo ya mipakani kuimarika na kuongezeka.
Samweli Mawanja katibu kata mstaafu
wa Liuli anasema wananchi wa mipakani
baina ya Tanzania na Malawi wamekuwa wanatembeleana na kufanya biashara
mbalimbali bila wasiwasi wowote licha ya viongozi wa kitaifa kusikika kushindwa
kufikia muafaka wa mpaka wa ziwa Nyasa kati ya nchi hizo mbili.
“Tumekuwa tunasikia katika
vyombo vya habari vya Tanzania na Malawi vikizungumzia mgogoro huu,lakini
nataka kukuambia kwamba wananchi wa Malawi wanafika hapa kila siku kuleta
biashara zao na sisi watanzania tunakwenda kila siku katika nchi ya Malawi kupeleka biashara mbalimbali hakuna vurugu ni
amani na utulivu’’,anasisitiza Mawanja.
Kwa mfano jana usiku kuna boti
la Malawi limeingia na kuleta shehena ya sukari toka Malawi,idadi ya watu wa
Malawi wanaofika hapa ni kubwa zaidi ukilinganisha na watanzania,wananchi wa
Malawi wengi wanalaani na kusikitishwa Rais wao kugombana na watanzania na
wameahidi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2014 kumuangusha anasema Mawanja.
Charles Chawila ni diwani wa
kata ya Liuli anasema wavuvi wa Tanzania wamekuwa wanaendelea na kazi ya uvuvi
katika ziwa Nyasa kwa amani na utulivu
na kwamba kauli kali zinazotolewa na viongozi wa kitaifa wa nchi zote
mbili haziendani na hali halisi ambayo inaendelea tangu kuibuliwa upya kwa
mgogoro huo kwa kuwa wananchi wanaendelea kushirikiana vizuri katika sekta za
kiuchumi,kijamii na kiutamaduni.
“Viongozi wengi pengine
hawajui,kuna watanzania wengi wa mwambao mwa ziwa Nyasa ambao wameoa na kuolewa
Malawi na kuna watu wa Malawi wengi ambao wameoa na kuolewa Tanzania mgogoro
huu ambao unakuzwa na vyombo vya habari kupitia wanasiasa sio mkubwa kama
inavyoelezwa’’,anasisitiza.
John Chiume ni mtanzania ambaye
anaishi na kufanya biashara katika kisiwa cha Likoma nchini Malawi kwa zaidi ya miaka 30 sasa, anasema wananchi
wa Malawi hawafurahishwi na kitendo cha Rais wao Joyce Banda kuibua mgogoro wa
mpaka wa ziwa Nyasa ambapo amedai huenda kitendo hicho kikamuathiri kisiasa
Rais huyo katika uchaguzi mkuu ujao.
Gorge Mkate(70) mkazi wa
Mbambabay anasema Mgogoro huo ulianza enzi ya hayati Rais Kamuzu Banda ambaye
miaka ya sitini alikuwa anazungumza
kwenye redio yao,kwamba ziwa lote ni la
Malawi pia wilaya ya Rungwe na hadi
Mbeya ni sehemu ya Malawi.
“Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1968 alimwita Kamuzu Banda ni kichaa,alikasirika
kwa sababu ya madai ya Kamuzu kwamba sehemu za kusini ya Tanzania ni za
Malawi,alidai hata makao makuu ya wilaya mpya Mbamba Bay na sehemu zingine
mkoani Ruvuma karibu na Ziwa Nyasa kwamba ni za Malawi’’,alidai Mkate.
Amesema nchi ya Malawi ina
mikoa mitatu ambayo aliitaja kuwa ni Lilongwe,Mzuzu na Brinytre na kwamba wananchi wengi wa Malawi wapo
Tanzania katika maeneo ya mpakani wakishirikina vizuri na watanzania ambapo
hadi sasa hakuna tatizo lolote licha ya madai yanayoendelea kuchochea mgogoro
kuonekana kama ni mkubwa.
Gidion Ntare mvuvi wa samaki
katika ziwa Nyasa anasema wamekuwa wanaendelea kufanyakazi ya uvuvi hadi
katikati ya ziwa Nyasa bila wasiwasi wowote wa kushambuliwa na nchi ya
Malawi ambapo madai ya kuibuka kwa
mgogoro wa ziwa Nyasa wamekuwa wanausikia kupitia vyombo vya habari .
“Wavuvi wanaendelea kuvua usiku
na mchana hadi katikati ya ziwa haijawahi kutokea eti kuna mvuvi
ameshambuliwa hali ni ya amani na
utulivu,wavuvi wanakufa kutokana na ajali za mitumbwi katika ziwa Nyasa ambazo zinasababisha wavuvi
wengi kupoteza maisha kila mwaka’’,alisema.
Hata hivyo Ntare anasema
wamekuwa wanakwenda kufanya uvuvi katika nchi ya Malawi ambapo hali ya maisha
ya wavuvi wa Malawi ni bora zaidi kuliko Tanzania wanatumia vifaa vya
kisasa,wavuvi ndiyo wanaongoza kwa
utajiri katika nchi ya Malawi ndiyo sababu kuna wavuvi wengi wa Tanzania
wameamua kwenda kufanyakazi ya uvuvi nchini Malawi ambako serikali imewawezesha
samaki wanaovuliwa hupelekwa kuuzwa katika nchi za Zimbawe,Afrika ya kusini na
Botswana.
Martin Challe ameiomba serikali ya Tanzania kuhakikisha
katika kipindi hiki cha mgogoro wa mpaka wa ziwa Nyasa maeneo yote ya mwambao
mwa ziwa yanaendelezwa kwa kuwa yamesahaulika tangu uhuru ukilinganisha na
maeneo ya mwambao mwa ziwa Nyasa upande wa Malawi ambapo kuna maendeleo
makubwa.
Challe anadai kuwa ukifika
mwambao mwa ziwa Nyasa upande wa Malawi barabara zake ni za viwango vya lami,uvuvi
wa kisasa,hata fukwe za ziwa Nyasa upande wa Malawi zimeboreshwa na wawekezaji wameboresha sekta ya utalii wa
fukwe ambapo upande wa Tanzania hali ni mbaya kuanzia uvuvi duni, barabara na
hata fukwe bora zilizopo bado hazijatambuliwa hadi sasa.
Chanzo
cha mgogoro wa ziwa Nyasa kimetokana na mikataba yenye utata iliyoachwa na
wakoloni waingereza, ambapo kwa kulitambua hilo marais waliotangulia hasa
Bakili Muluzi na Bingu wa Mutharika wa Malawi na wenzao Julius Nyerere, Ali
Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wa Tanzania waliendeleza mazungumzo. kutokana na makubaliano kati ya Waingereza waliokuwa watawala
wa Nyasaland na Wajerumani waliokuwa watawala wa Tanganyika, mpaka halali baina
ya nchi hizo ulikuwa katikati ya ziwa Nyasa.
Hivi sasa jopo la usuluhishi wa sakata la mgogoro wa ziwa Nyasa limeundwa wakiwemo marais wa zamani barani Afrika ambao ni Festus Mogae (Botswana),Thabo Mbeki (Afrika Kusini) na Joachim Chissano (Msumbiji) ambaye ndiye mwenyekiti..
Tayari nchi ya Malawi imetangaza kujitoa
katika mazungumzo ya mgogoro wa mpaka kati yake na Tanzania kwenye Ziwa Nyasa,
ambapo Serikali ya Tanzania kupitia waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa
kimataifa Bernad Membe imeitaka nchi hiyo kuacha kutapatapa na kamwe isithubutu
kugusa eneo hilo la mpaka.
Waziri
Membe kwa niaba ya serikali amesema kama nchi hiyo itakiuka, Serikali ya
Tanzania itaomba ushauri wa nini cha kufanya kutoka kwa jopo la usuluhishi .
Kauli
hiyo ya Serikali imekuja siku chache baada ya Rais wa Malawi, Joyce Banda
kusema kuwa mgogoro huo sasa utapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki
(ICJ), kwa madai kwamba juhudi za usuluhishi wa kidiplomasia zimeshindikana.
Hata
hivyo, uamuzi huo wa Malawi ni kinyume na makubaliano baina ya nchi hizo mbili
yaliyofanyika Novemba 7 mwaka jana, jijini Dar es Salaam ambapo serikali zote
zilikubaliana kwamba jopo hilo ndiyo sehemu ya mwisho ya makubaliano.
Waziri
huyo wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa alisema kuwa tangu kuibuka kwa
mgogoro huo, Malawi imekwenda kulalamika katika nchi za Uingereza, Marekani,
Umoja wa Afrika (AU) na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa
Afrika (SADC).
Mgogoro
huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi bila kushauriana na Tanzania kutoa
leseni kwa kampuni mbili za kigeni kutafuta mafuta baada ya kubainika kuwa
katika eneo la ziwa Nyasa kuna kiasi
kikubwa cha Mafuta.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment