![]() |
| Pichani ni sehemu ya mlima uliouzwa bila ridhaa ya wanakijiji |
Na
Albano
Midelo
MLIMA ambao umetengwa kwa ajili ya
hifadhi ya msitu katika kijiji cha Nkali
kata ya Liuli wilayani Nyasa mkoani Ruvuma umeuzwa na baadhi ya viongozi wa
Halmashauri ya kijiji hicho bila ridhaa ya wananchi.
Mlima huo wenye ukubwa wa hekta zaidi ya 100 unaofahamika kwa jina la Hitombi
hiveli yaani mlima wenye vilele viwili uliopo kilometa mbili kutoka fukwe za
ziwa Nyasa umeuzwa hekta 20 tangu mwaka
2008 na mnunuzi ameanza shughuli za kibinadamu juu ya mlima huo hali
ambayo inahatarisha usalama wa viumbe hai waliomo katika msitu huo.
Hitombi hiveli ni mlima wenye msitu
mnene uliotengwa na kijiji kwa ajili ya hifadhi kutokana na mlima huo kuwa makazi ya wanyama pamoja na viumbehai wengine wakiwemo wadudu,mimea na wanyama adimu kama mbega wenye rangi nyeupe na nyeusi ambao wapo hatarini kutoweka.
Victor Komba ni mwenyekiti wa kamati
ya mazingira katika kijiji cha Nkali anawataja Viumbe wengine ambao
wanapatikana katika msitu huo ni sungura pori, ngedere, nyani, digidigi,
mbweha, nungunungu, panya buku wakubwa wenye uzito hadi kilo 25, makazi ya wadudu wa aina mbalimbali, utajiri wa mimea
mingi ya asili kama uyoga wa asili na makazi ya ndege maarufu aina ya ngwazi
mwenye uwezo wa kuvua samaki.
Kaimu mtendaji wa kijiji cha Nkali
Barnaba Mbele anasema mlima huo ulitengwa na kuhifadhiwa kuwa moja ya maeneo
ya hifadhi ya msitu wa kijiji hicho lengo likiwa ni kuuhifadhi kutokana na ukweli kuwa mlima huo umekuwa
chanzo cha mvua katika vijiji vinavyozunguka kata ya Liuli.
Amevitaja vijiji ambavyo vinazunguka
kata ya Liuli na vinautegemea mlima huo kwa ajili ya mvua kuwa ni pamoja
na Hongi,Nkali,Liuli,Puulu na Nkalachi
na kwamba kitendo cha baadhi ya viongozi kuuza sehemu ya mlima huo bila ridhaa
ya wananchi wote hakikubaliki na kwamba mnunuzi anatakiwa kusimama kuendelea
kufanyakazi za kibinadamu katika mlima huo hadi hapo mgogoro huo
utakapokamilika.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nkali, Menas
Kilimo anadai kuwa viongozi watatu wa Halmashauri ya kijiji hicho wanadaiwa
kuuza sehemu ya mlima huo tangu mwaka
2008 ambapo mnunuzi ameanza kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye mlima huo
bila kujali athari za kimazingira zinazoweza kujitokeza.
Viongozi wanaotuhumiwa kuuza mlima huo ni
wajumbe watatu wa Halmashauri ya kijiji hicho ambao ni Aidan Mbungu, Desderius
Mbunda na Mathias Chilambo ambao kwa pamoja wanadaiwa kuuza eneo la ukubwa wa
hekta 20 kati ya hekta 100 za mlima huo.
Kaimu mtendaji wa kijiji cha
Nkali Barnaba Mbele alidai kuwa viongozi hao kwa kushirikiana na
mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho Mathayo Konjakonja pamoja na mtendaji
mstaafu wa kijiji hicho Sarah Chitunji, inadaiwa katika kipindi cha mwaka 2007/2008
waliuza sehemu ya mlima bila ridhaa ya
wanakijiji .
Mbele alibainisha kuwa tangu wakati
huo hadi sasa wananchi walikuwa wanalalamika kuhusu kitendo hicho huku mnunuzi
wa sehemu ya mlima huo ameanza kufanya shughuli za kibinadamu tangu mwaka 2011 .
Hivi karibuni wananchi wa vitongoji vya Mshale na Muungano wanaozunguka mlima huo baada ya kubaini mnunuzi anaendelea na kazi
juu ya mlima huo waliamua kwenda kwa mwenyekiti wa sasa wa kijiji cha
Nkali, Venancy Kilimo wakidai mlima huo urudishwe mikononi mwa wananchi na
uendelee kuwa hifadhi.
Bernad Challe,Amoni Bwanga,Musa Haule
na Joseph Sangana wakazi wa kijiji cha Nkali wamemtaka afisa mtendaji wa kijiji
cha Nkali Denis Mangwea asimamie sakata hilo ili viongozi hao wanaotuhumiwa wapelekwa
katika vyombo vya sheria huku wakitoa rai kwa mwenyekiti wa kijiji hicho kufufua kamati ya ulinzi na usalama ili
kuongeza ulinzi dhidi ya mlima huo.
Charles Chawila diwani wa kata ya
Liuli amekiri ofisi yake kupata taarifa za
sehemu ya mlima huo wa asili kudaiwa kuuzwa na kwamba ofisi yake
inatarajia kufanya mazungumzo na mnunuzi wa sehemu ya mlima huo ili asiendelea kufanya shughuli za kibindamu hadi
mgogoro huo utakapopatiwa ufumbuzi.
“Mlima huu ni muhimu katika kata yangu
kwa kuwa unachangia kwa asilimia 90 mvua zinazonyesha kila mwaka hivyo siwezi
kukubali uharibifu wa mazingira
kuendelea kufanyika katika mlima wa hifadhi hata kama mnunuzi anadai ameuziwa
kihalali na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya kijiji ambao
hawakuwashirikisha wananchi’’,alisisitiza Chawala.
Hata hivyo sheria ya ardhi ya vijiji
ya mwaka 1999 fungu la nane inaelekeza kuwa Halmashauri ya kijiji ina jukumu la
kusimamia ardhi yote ya kijiji kwa kuzingatia utunzaji wa ardhi,maliasili na
mazingira na kwamba Halmashauri ya kijiji itagawa ardhi baada ya kuruhusiwa na
mkutano wa kijiji na sio vinginevyo.
Kulingana na sheria hiyo mkutano wa
kijiji unatakiwa kuwa na wanakijiji wasiopungua 100 ambao wanaweza kupeleka
malalamiko yao ya namna Halmashauri ya kijiji inavyoshindwa kusimamia ardhi ya
kijiji kwa Halmashauri ya wilaya ambayo itamtaarifu kamishina wa ardhi ili
hatua ziweze kuchukuliwa.
Dk.Rugemeleza Nshala ni mtaalamu wa
ardhi na mwanasheria anabainisha kuwa kisheria mtu binafsi anaruhusiwa kumiliki
ardhi na kutahadharisha kuwa haruhusiwi
kumiliki visiwa vya karibu,fukwe au mlima
ambapo sheria ya ardhi ya mwaka 2004 inazuia mtu kufanyakazi eneo la
meta 60 kutoka kingo za mito,maziwa na bahari ambapo kiulimwengu hairuhusiwi
kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya meta 200.
Injinia Stella Manyanya ni mbunge na
mjumbe wa Bodi ya utalii mkoa Ruvuma anatoa wito kwa wadau wote wa sekta ya
utalii mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kuwa
wanayalinda maeneo yote yaliohifadhiwa ili yasiendelee kuharibiwa na hatimaye
kuathiri kwa namna moja au nyingine mazingira na sekta ya utalii katika ukanda wa kusini.
Tangu serikali ilipotangaza
kufunguliwa kwa Mtwara korido pamoja na kutangazwa kwa wilaya mpya ya Nyasa
wawekezaji wengi wamekuwa wanajitokeza kutafuta maeneo ya uwekezaji
mwambao mwa ziwa Nyasa huku baadhi yao wakipata maeneo kwa njia haramu
ikiwemo kuwatumia viongozi wa vijiji bila kuwahusisha wananchi.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

No comments:
Post a Comment