|
Kiongozi huyo mstaafu alitoa
msimamo huo jana jijini Dar es Salaam katika kongamano juu ya utamaduni wa
Kiislamu Afrika Mashariki ambapo Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji.
“Imani ni nafsi ya mtu na
haitakiwi kumlazimisha kula nyama iliyochinjwa na mwenzie. Na kama unaona
aliyochinja mwenzio ni kibudu basi usile chinja yako, kula hata ukitaka
kula chura, mjusi, konokono, kula utakacho ruksa ilimradi tu usiingie
katika jinai,” alisema.
Mwinyi alikumbusha kuwa hata
wakati wa utawala wake majaribu kama hayo yaliwahi kumtokea, lakini
alijitahidi kuweka sawa kwa kumwambia kila mtu ale kile anachofikiri ni
chakula bila kumlazimisha mwenzake.
Alisema Watanzania wamezaliwa
ardhi moja na kwamba kinachotakiwa ni kuwa na misingi ya kuvumiliana, na
kwamba sifa ya Uislamu ni pamoja na kuwa na uvumilivu.
Aliongeza kuwa Uislamu si
kufanya vurugu kama inayotafsiriwa na makundi ya wanaotaka kuvunja amani ya
nchi kwa kutumia jina la dini ya Kiislamu.
Pia alimshukuru Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Ulimwengu wa Kiislamu Duniani (Rabita), Dk. Abdullah Mohsin
Al-Turki kwa kuichagua Tanzania katika kuhubiri amani.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne
Maghembe ambaye alimuwakilisha Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilal katika
kongamano hilo, alisema kuwa utamaduni wa Kiislamu Afrika Mashariki na
duniani kwa ujumla ni kuvumiliana katika dini.
Pia aliwataka Waislamu
kujiendeleza katika elimu, akisema kuwa hata Mtume alihamasisha hayo,
lakini Waislamu wameshindwa kuyafuata.
Prof. Maghembe alitoa mfano kuwa
Waislamu wana Chuo Kikuu kimoja wakati dhehebu moja la Lutherani lina vyuo
vikuu 11, akisema ni vyema wakaungana na kujenga vyuo kwa ajili ya kusaidia
kuongeza wasomi katika taaluma mbalimbali.
“Suala la elimu ya dunia pia ni
muhimu, lakini mfano mzuri wa elimu kushuka ni katika mikoa ya Pwani ambako
ndiko ilipoanzia. Mathalani mwaka 1995 wanafunzi walioanza darasa la kwanza
walikuwa 35,000 lakini waliomaliza darasa la saba ni 9,000. Hapa inaonesha
Waislamu tunarudi nyuma,” alisema.
Akizungumza katika kongamano
hilo, Dk. Abdullah Mohsin Al-Turki alisema katika nchi ya Saudia wanaishi
watu tofauti, lakini wakiwa katika upendo huku akisisitiza kikubwa ni
kuheshimiana.
Alisema Rabita imekuwa ikifanya
kazi katika nchi mbalimbali za Nigeria, Gabon, Jamhuri ya Kongo na baada ya
ziara yake nchini hapa atahitimisha kwa kuitembelea Sudan.
Kongamano hilo limeandaliwa na
Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania likiwa na lengo la
kusisitiza amani nchini.
CHANZO TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment