Msaidizi
wa zamani wa Padri (Katekisita) katika Kigango cha Kanisa Katoliki Kijiji cha
Mkwajuni, Florian Mwamosi (70) amekufa baada ya kuzikwa akiwa hai katika
kaburi moja na mtu anayedaiwa kumuua kwa njia ya kishirikina.
Tukio
hilo limetokea katika Kitongoji cha Maweni kijijini hapo wilayani Chunya mkoani
Mbeya.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani alikiri kutokea kwa tukio
hilo akieleza kuwa lilitokea saa 9:00 mchana katika kijiji hicho cha
Maweni Mkwajuni wilayani Chunya.
“Marehemu
aliuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa na mawe kwa tuhuma za
kuhusika na uchawi na kusababisha kifo cha Peter Robert,” alisema.
Kamanda
Athumani alisema kuwa uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea na kwamba
wahusika wote wa tukio hilo wamekimbia na kuzihama nyumba zao, hivyo polisi
wanaendelea na msako wa kuwatia mbaroni watuhumiwa na kwamba tayari
kaburi hilo limefukuliwa jana kutenganisha maiti hizo.
Mashuhuda
wa tukio hilo walisema kuwa marehemu huyo ambaye alikuwa akituhumiwa kwa
ushirikina aliwahi kuwa Katekista wa kigango hicho hadi mwaka 2007.
Wameeleza
kuwa Mwamosi alikwenda kuhudhuria mazishi ya Peter Robert (28)
katika kitongoji hicho cha Maweni, baada ya kufuatwa nyumbani kwake na
watu wakitaka aende kwa sababu yeye ni mmoja wa wazee wa mila katika kitongoji
hicho.
“Bwana
Mwamosi alikuwa akituhumiwa kwa uchawi kwa muda mrefu na wenzie
wawili, hivyo alipofika makaburini ilianza minong`ono ya watu na huku
wengine wakiguna na ndipo alipoombwa aingie kaburini kwa ajili ya
kupokea jeneza lililobeba mwili wa marehemu Peter Robert,” alisema mkazi
mmoja wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Joseph.
Alisema
kuwa baada ya kuingia kaburini akiwa na watu wengine watatu wenzake walitoka
kwa haraka na kumwacha Mwamosi peke yake ndipo kundi la watu waliokuwa eneo
hilo la makaburi walianza kumshambulia kwa kumpiga mawe huku wakimwamuru akae
chini.
Shuhuda
huyo alisema kuwa baada ya kukubali kukaa chini akiwa ndani ya kaburi hilo,
walianza kumfukia na alipofukiwa nusu ya mwili wake waliingiza jeneza la
marehemu Peter na kuliweka juu yake na kuanza kulifukia kaburi hilo.
“Baada
ya kukaa chini ndani ya kaburi hilo ndipo walianza kumfukia kwa udongo na
baadaye wakachukua jeneza la marehemu na kuliweka juu yake, kisha kumfukia na
udongo na taratibu za mazishi ziliendelea kwa ajili ya marehemu
Peter,”alisema.
Alidokeza
kuwa chanzo cha tukio hilo ni marehemu Robert kuugua ghafla tumbo, ndipo ndugu
zake walipoamua kumpeleka kwa mganga wa jadi kwa ajili ya kupata matibabu na
baada ya siku tatu alifariki dunia.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI
Jamani huu kweli uungwana?
ReplyDelete