Na Albano Midelo
 |
| Bandari ya Ndumbi,makaa ya mawe husafirishwa |
WANANCHI wa kijiji cha Liyombo
kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wameonyesha wasiwasi wao juu ya
kudaiwa kutoroshwa kwa makaa ya mawe pamoja na ulipwaji wa fidia watakazo pata,baada ya kufahamika kuwa
kijiji hicho kimejengwa juu ya mwamba wa makaa ya mawe.
Baadhi ya wakazi
wa kijiji hicho kilichopo
katika kata ya Ruanda ambao ni Elia Hyera,John Mbepera na Joakimu Nchimbi
wakizungumzia suala hilo wametoa wito kwa serikali kusimamia na kuhakikisha
wanalipwa fidia pamoja na kuwa makini na kufuatilia sampuli za makaa hayo
zinazopelekwa nje ya nchi.
“Hawa wawekezaji
wamechukua sampuri tani 1000 na kupeleka nchini Afrika ya kusini kwa njia ya
,meli kupitia bandari ya Ndumbi ziwa Nyasa, kwa ajili ya utafiti wa
awali,halafu wanasema bado zinatakiwa tani 10,000 ili kukamilisha utafiti na
kuwaridhisha wanunuzi wa makaa hayo nje ya nchi,sisi wananchi wanatuchanganya
mara wanasema majibu yanaonyesha kuwa mkaa huo ni bora hatujui tena tani
nyingine za nini,wizara ya madini inatakiwa kusimamia hali hii isije ikiwa ni
janja ya nyani’’,alitahadharisha Elia Hyera.
Kampuni ya Tancoal Energy
Limited (TANCOAL) , shirika la Taifa la maendeleo ( NDC), pamoja na shirika la Pacific Corporation ya Afrika Mashariki
(PCAM), walianza utafiti wa kuchimba makaa ya mawe katika kijiji cha Liyombo mwaka 2008 ambapo
utafiti umebaini eneo hilo kuwa na mkaa wa kutosha na wenye ubora.
Utafiti ambao umefanyika umebaini
kuwa kijiji cha Liyombo kipo juu ya mwamba bora wa makaa ya mawe ambapo Meneja
wa uchimbaji ya TANCOAL ambayo ina hisa ya asilimia 70 Gordon Mc Cormack,alisema kuwa mwelekeo wa kazi hiyo ni kupata nishati ya
kutosha itakayo saidia uchumi wa mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Alibainisha kuwa mgodi huo unatarajia kuwa
chanzo kikubwa cha utoaji wa makaa ya mawe hapa nchini na kusambaza kwa
wahitaji wote wa nishati hiyo hapa nchini vikiwemo viwanda na nje ya nchi na
kwamba kitakuwa chanzo kikuu cha umeme kimataifa na msaada katika gridi ya umeme ya taifa ambayo hivi sasa umeme wake hautoshelezi na kusababisha
mgawo wa umeme.
Mtaalamu wa miamba Alex
Sostenes alibainisha zaidi kuwa makaa hayo ya mawe yamesambaa maeneo
yote ya Ngaka na Liyombo pamoja na maeneo mengine ya jirani na kijiji cha Liyombo na
kwamba mashine ya utafiti kwa utalaamu itatoboa shimo moja kijijini hapo ili
kubaini wingi wa mkaa na ubora wake na kuwataka wanakijiji wasiwe na wasiwasi
juu ya nyumba zao ama mali zao.
Hata hivyo mkurugenzi mkuu wa
TANCOAL Emmanuel Costantinides amethibitisha kuwa mkaa wa mawe wa kijiji cha Liyombo ni mkaa
bora kutokana na majibu ya sampuri zilizopelekwa nchini Afrika Kusini kwa
uchunguzi kupitia Bandari ya Ndumbi Ziwa Nyasa.
“Kiasi cha tani 1000
zimesafirishwa kupelekewa nchini Afrika ya kusini kwa uchunguzi wa awali kwa
madhumuni ya kujiridhisha ambapo matokeo yameonyesha dalili nzuri kwa kuwa
mkaa unaonyesha ubora wake haufanani
na mkaa wa mawe unaochimbwa katika nchi yeyote duniani,mkaa wa Mbinga ni bora kuliko mikaa mingine yote duniani’’,alisisitiza.
Hata hivyo alisema tani 10,000
zinahitajika kupelekwa nchini
Afrika ya kusini kama sampuri kutoka
eneo la utafiti ili wanunuzi waweze kujiridhisha zaidi ingawa hali hiyo
inaleta hofu kwa wakazi wa kijiji hicho ambao wanashauri ni bora utafiti
ungefanyika hapa hapa nchini ili kusifanyike hujuma ya kusafirisha maliasili
nje ya nchi kwa kisingizio cha utafiti huku watanzania wakibakia kuambulia
mashimo kutokana na uharibifu wa mazingira.
Mgodi
wa makaa ya mawe ya Liyomba na Ngaka
wilayani Mbinga umekadiriwa kuwa na zaidi ya tani 400 milioni za mkaa wa
mawe. Kiasi hicho, kwa mujibu wa wataalam, kinaweza kuchimbwa kwa kipindi cha
zaidi ya miaka 100.
Hata
hivyo sera Taifa ya madini ya mwaka 1997 inasisitiza juu ya sekta binafsi
kuendeleza madini, na wakati huo huo Serikali ikiwa na jukumu la kuidhibiti,
kuikuza, kuiwezesha na kuiendelea.Sekta
ya madini inachangia takribani asilimia 2.3 ya pato la Taifa, ambayo
inakadiriwa kufikia asilimia 10 ifikapo 2025.
|
No comments:
Post a Comment