Tuesday, April 30, 2013

Ugonjwa wa kansa unavyotishia ustawi wa mwanamke



Na Albano Midelo

WANAWAKE hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo matatizo wakati wa kujifungua ambapo kila mwaka akinamama zaidi ya 8000 hufariki kutokana na matatizo ya uzazi.

 Kana kwamba hilo halitoshi wanawake pia wanakabiliwa na tatizo jingine la kiafya ambalo ni ugonjwa wa saratani au kansa ya kizazi ambayo inaelezwa ndiyo kansa inayoongoza katika kusababisha vifo vitokanavyo na kansa kwa akinamama waliopo katika nchi zinazoendelea.

Utafiti unaonesha kuwa akinamama zaidi ya 500,000 hupatwa na ugonjwa wa kansa ya uzazi kila mwaka ulimwenguni, kati ya hao akinamama 250,000 hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo ambapo hapa nchini wanawake 4000 wanagundulika kila mwaka.

 Ugonjwa huo nchini Tanzania umeelezwa kukua kwa kasi, huku waathirika wa tatizo hilo wakiwa ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 25 na 30. Daktari wa Kitengo cha Patholojia cha Uchunguzi wa Magonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam Innocent Mosha anasema, kati ya wagonjwa 17 na 20 hugundulika na saratani kila siku katika hospitali hiyo ya taifa.


“Kwa mwaka wagonjwa wanaogundulika kuwa na saratani katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni zaidi ya 4,000, takwimu hizo ni za Hospitali ya Taifa Muhimbili tu, bado kuna Ocean Road, mikoani na hospitali nyingine binafsi’’,alisisitiza Dk.Mosha.

 Daktari Bingwa wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili mjini, Dk.Henry Mwakyoma anazitaja saratani kuu zinazoongoza nchini kuwa ni pamoja na saratani ya shingo ya kizazi, tezi dume, ngozi, mifupa, tezi kwa watoto na wakubwa, damu, kongosho, ubongo na ini.

Ugonjwa wa saratani umekuwa tishio katika nchi za Afrika zilizo chini ya Jangwa la Sahara ikiwamo Tanzania ambapo kwa mwaka 2010, takwimu zinaonesha ugonjwa huo umeua watu milioni 9.9 duniani.

Mratibu wa kampeni ya kupambana na ugonjwa huo nchini kutoka Taasisi ya Tanzania 50 Plus, Mchungaji Dk. Emmanuel Kandusi,amesisitiza kuwa saratani ni hatari ukilinganisha na takwimu za magonjwa mengine.

Takwimu za magonjwa za mwaka 2010 zinazoonyesha kuwa ugonjwa wa  malaria uliua watu 500,000, kifua kikuu milioni 2.1, UKIMWI milioni 1.8 na Saratani iliongoza kwa kuua watu milioni 9.9.

Hata hivyo Dk.Kandusi anabainisha kuwa asilimia 75 ya watu waliokufa kwa ugonjwa wa saratani (sawa na milioni 7.4), walitoka katika nchi zinazoendelea.

Amezitaja dalili za saratani ya tezi dume, kuwa ni pamoja na mgonjwa hupata udhaifu katika kujisaidia haja ndogo, hisia ya kutaka kupata haja ndogo kila wakati hasa nyakati za usiku, mkojo kutoka wenyewe, maumivu au kuhisi muwasho wakati wa haja ndogo na uume kusimama kwa shida.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa jarida la Man, amezitaja sababu zinazochangia ugonjwa huo kuwa ni pamoja na ulaji wa vyakula vyenye mafuta vikiwemo, nyama, chips mayai, pombe na kutofanya mazoezi.



Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka katika hospitali ya rufaa ya misheni ya Peramiho iliyopo nje kidogo ya mji wa Songea mkoani Ruvuma Dk.Gaudence Komba anasema hapa nchini takwimu zinaonesha kuwa kansa au saratani ya kizazi ndiyo inayoongoza kwa kusababisha vifo.



Dk.Komba anazitaja saratani nyingine ambazo zinafuatia katika kusababisha vifo kwa wanawake kuwa ni pamoja na   saratani inayoitwa kitaalamu Kapodsarcoma na saratani ya matiti.



Hata hivyo anasema zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani ya kizazi hufika katika vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa wamechelewa yaani  ugonjwa ukiwa tayari umeenea sana jambo ambalo anasema saratani hizo inakuwa ni vigumu kutibika kwake kwa kuwa ugonjwa unakuwa tayari umeenea sehemu mbalimbali za mwili.





Amezitaja sababu zinazobabisha wagonjwa wa saratani ya kizazi kuwa ni pamoja na kwenda hospitali wakiwa wamechelewa kuwa ni pamoja na kukosekana kwa  huduma za uchunguzi wa awali(screening) hasa katika  maeneo ya vijijini pamoja na kutokuwa na uelewa kuwa saratani ya uzazi inaweza kuzuilika kwa kufanyiwa uchunguzi wa awali.



Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya wanawake anasisitiza kuwa ugonjwa wa saratani ya kizazi ukiwa katika hatua za mwanzo unaweza kutibika kabisa kwa njia ya upasuaji au kwa njia ya mionzi.



Hata hivyo kulingana na Dk.Komba,katika nchi zilizoendelea uchunguzi wa awali unafanywa mara kwa mara katika nchi hizo,umepunguza kabisa saratani ya uzazi kwa akinamama na kwamba njia inayotumika kufanya uchunguzi iitwayo kitaalum Cytology, imeonekana kuwa ni ngumu kutumika katika nchi  za dunia ya tatu kama Tanzania.



Kulingana na daktari huyo njia hiyo inahitaji wataalamu wa hali ya juu hali ambayo anasema inasababisha gharama ya huduma hiyo kuwa ni kubwa na hatimaye kushindwa kufanyika katika nchi zinazoendelea.



Kutokana na hali hiyo shirika la afya duniani(WHO) kwa kushirikiana na wadau wengine wa afya ulimwenguni limegundua njia inayoonekana kuwa mbadala kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania,njia ambayo kitaalaum inaitwa visual inspection with acetic acid(VIA) ambapo huduma hiyo inaweza kutolewa hata katika vituo vya afya na zahanati kwa kuwatumia wahudumu waliopo kama wauguzi na waganga.



Dk.Komba anasema tayari WHO inasaidia serikali za nchi mbalimbali kuanzisha na kuendeleza huduma hiyo ambapo majaribio ya huduma hiyo tayari yamefanyika katika wilaya mbalimbali na kupata mafanikio makubwa ili kuanzisha huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya afya za wanawake.



 Changamoto kubwa inayowakabili wanawake ni kwamba licha ya saratani ya kizazi ambayo inaongoza kwa kusababisha vifo vingi vya wanawake ulimwenguni,saratani nyingine ambayo inatajwa kuwa ni miongoni mwa saratani zinazogharimu maisha ya wanawake  ni saratani ya matiti.



Chama cha madaktari wanawake nchini(MEWATA) kwa kushirikiana, vyombo vya habari nchini na wadau wengine  katika miaka ya karibuni vimekuwa mstari wa mbele katika kufanya kampeni kabambe ya kuhakikisha wanawake wanajitokeza kupima ili kutambua mapema iwapo wana saratani hiyo ya matiti ili waweze kupatia matibabu mapema.



Takwimu kutoka MEWATA zinaonesha kuwa kati ya wanawake zaidi ya 55,000 waliopimwa saratani ya matiti,wanawake 113 wamegundulika kuwa na saratani ya matiti.



Hata hivyo takwimu hizo za MEWATA zinabainisha kuwa  kati ya wanawake hao waliopimwa, wanawake 2498 wamegundulika kuwa na matatizo ambayo hayahusiani na saratani ya matiti.MEWATA kwa kushirikiana na wizara ya afya na ustawi wa jamii imekuwa ikiandaa tiba kwa wanawake waliogundulika kuwa na saratani ya matiti kulingana na sehemu ambayo ugonjwa huo umefikia.



Wataalamu wa saratani ya matiti wanasema iwapo  ugonjwa huo ni uvimbe na saratani haijasambaa ,mgonjwa atapelekwa kufanyiwa upasuaji na kupatiwa tiba na kwamba endapo saratani hiyo itakuwa imesambaa inabidi mgonjwa akatibiwe kwa mionzi katika Taasisi ya saratani iliyopo katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es salaam.



Kulingana na wataalamu,saratani ya matiti ni uvimbe usiokuwa na maumivu ambao mwanamke yeyote anaweza kuwa  anao bila ya yeye mwenyewe kujijua na kwamba inashauriwa kila mwanamke awe na ufahamu kuhusu afya yake na mwili wake pamoja na  kujenga tabia ya kujichunguza mwenyewe mara kwa mara.

 Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema zaidi ya asilimia 70 ya visa vya ugonjwa wa saratani vinaweza kuzuiliwa na kwamba saratani inaweza kuzuilika ikiwa nchi zitaongeza uwezo wao wa kudhibiti saratani.

Kwa mujibu wa WHO nusu ya nchi kote duniani hazina uwezo wa kukabiliana kikamilifu na ugonjwa huo, na wala hazina mpango tekelezi wa kuudhibiti , ambao unajumuisha kuzuia, kugundua mapema, kutibu na huduma za uuguzi.

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa watu milioni 7.6 wanafariki dunia kila mwaka kutokana na saratani, huku takriban watu milioni 13 wakiwa wanapatikana na kansa kila mwaka.




                            

No comments:

Post a Comment