Yataka mitihani ya kidato cha nne kusahihishwa upya
SERIKALI imechukua uamuzi mgumu na
kuamua kuwafariji wanafunzi waliofeli mitihani ya kuhitimu kidato cha nne mwaka
2012 baada ya kufuta matokeo hayo na kuamua yaandaliwe upya kwa kutumia
utaratibu uliotumika mwaka 2011.
Uamuzi huo wa Serikali umetokana na
matokeo mabaya ya mitihani huo yaliyosababisha zaidi ya asilimia 60 ya
wanafunzi kupata sifuri.
Kutokana na matokeo hayo, Serikali
iliunda Tume inayoongozwa na Profesa Sifuni Mchome kuchunguza matokeo hayo ili
kupata ufumbuzi wa kudumu.
Muda mfupi baada ya tamko la
Serikali, baadhi ya wadau wa elimu wameeleza kufurahishwa na uamuzi huo, huku
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kikiikosoa hatua hiyo, kuwa imekiuka sheria na
kupora madaraka ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).
Akitoa kauli ya Serikali bungeni
kuhusu taarifa ya awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo ya Mtihani wa
Taifa Kidato cha nne mwaka 2012 , Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema wameagiza Necta kuweka viwango ili
matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi zao.
“Standardization ifanyike ili
matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi wazizoziweka katika kusoma kwa
mazingira, hali halisi ya Tanzania na uamuzi wa taifa kuongeza idadi ya shule
na wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora unaendelea,” alisema Lukuvi.
Lukuvi alisema Necta imeelekezwa
kuwa licha ya sheria ya kuanzishwa kwake kuruhusu kufanya marekebisho ya
mchakato wa mtihani, marekebisho yoyote ya kubadilisha utaratibu wa kupanga
viwango vya ufaulu na madaraja ya mitihani yanatakiwa yahusishe wadau wote
wanaohusika na mitalaa, ufundishaji na mtihani.
“Wakati Tume inaendelea kukamilisha
kazi yake, uamuzi wa Necta kutumia utaratibu mpya wa kupanga viwango vya ufaulu
na madaraja ya matokeo ya mitihani uliotumika 2012 usitishwe,” alisema Lukuvi
na kuongeza:
“Badala yake Necta itumie utaratibu
uliotumika mwaka 2011 kwa kidato cha nne na sita kwa mitihani yote, ikiwamo
utaratibu wa Standardization na kutoa matokeo mapya kwa kuzingatia maelekezo
haya.”
Pia, Serikalli imeagiza mchakato wa
tuzo wa taifa (National Qualifications Framework) na Mfumo wa Kutahiniwa/
kuthamini maendeleo ya mwanafunzi masomo yake (National Assessment Framework)
ukamilishwe haraka iwezekanavyo.
Katika mtihani wa mwaka 2012,
wanafunzi 367,756 walifanya mtihani huo na waliofaulu ni 126,847. Waliofaulu
kwa kwa madaraja ya kwanza hadi la tatu ni 23,520 sawa na asilimia 6.4 na
daraja la nne ni 103,327 sawa na asilimia 28.1, huku 240,909 ambao ni asilimia
65.5 wakipata daraja sifuri.
CHANZO
GAZETI LA MWANANCHI

No comments:
Post a Comment