MATOKEO mabaya waliyoyapata
wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 yamesababisha shule za
sekondari za serikali kukosa wanafunzi 10,000 waliopaswa kuanza masomo
Julai 29, mwaka huu.
Kutokana na upungufu huo
serikali imeamua kusitisha usajili wa shule za sekondari za serikali na
imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuboresha shule zilizopo
kwa kuhakikisha zinakuwa na miundombinu bora kwa wanafunzi wa kidato cha
tano na sita.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Philip Mulugo, ndiye aliyetangaza upungufu huo jijini Dar
es Salaa.“Mwaka jana tulisajili shule
mbili za kidato cha tano na sita, ambazo ni Miono iliyopo Bagamoyo na
Tandahimba ya Mtwara… tumekubaliana mwaka huu hatutaongeza shule nyingine,
tuboreshe zilizopo kwanza,” alisema Mulugo.
Mulugo alisema kutokana na
uchache huo wa wanafunzi wenye sifa za kujiunga na kidato cha tano, hasa wa
masomo ya Sayansi ya Jamii, serikali imeamua kutoongeza idadi ya shule za
sekondari kama inavyofanya kila mara kulingana na idadi ya wanafunzi wenye
sifa za kujiunga na shule husika.
Mulugo alisema watahiniwa 34,213
kati ya 431,650 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012
wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano na watakaokwenda kwenye shule 207
zilizopo hapa nchini.
Mulugo alisema idadi ya
waliofaulu inajumuisha wanaokwenda kwenye vyuo vya ufundi na Taasisi ya
Menejimenti ya Maendeleo ya Maji.
Kwa mujibu wa Mulugo, watahiniwa
binafsi 193 walifaulu na kati yao watahiniwa 76 waliokuwa na sifa za kwenda
kidato cha tano hawakuchaguliwa, kwa sababu mbalimbali, ikiwamo umri zaidi
ya miaka 25 huku mmoja wao akiwa si raia.
“Waliochaguliwa ni 34,213, kati
yao wanaokwenda kidato cha tano ni 33,683 na ufundi ni 530, ufaulu huo ni
ongezeko la asilimia 8.9 ikilinganishwa na wanafunzi 31,423 waliochaguliwa
mwaka 2012.
“Kati ya hao wanaokwenda sekondari
wasichana ni 10,300 na wavulana ni 23,383, hiyo ni sawa na ongezeko la
wanafunzi 2,824, sawa na asilimia 9.15 ikilinganishwa na wanafunzi 30,859
waliochaguliwa mwaka 2012,” alisema Mulugo.
Kuhusu ufaulu wa masomo ya
sayansi, naibu waziri huyo alisema wavulana wameongezeka, ambapo kati ya
23,383 waliochukua masomo ya sayansi ni 13,708 sawa na asilimia 58.62
wakati waliobaki walichaguliwa kwenye msomo ya sayansi ya jamii.
Mulugo alisema kati ya wasichana
10,300 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano, wasichana 5,038 sawa na
asilimia 48.91 walichaguliwa kwenye masomo ya sayansi huku 5,262 sawa na
asilimia 51.09 wakipelekwa kwenye masomo ya sayansi ya jamii.
Kwa upande wa vyuo vya ufundi,
Mulugo alisema waliofaulu ni 530, kati yao wavulana ni 416 na wasichana ni
114, na kusema idadi ya wasichana imeongezeka kutoka 47 mwaka jana, sawa na
asilimia 142.55.
Akifafanua zaidi, alisema
kuanzia mwaka huu wamerejesha utaratibu wa wanafunzi wanaoingia kidato cha
tano wataanza masomo wiki ya tatu ya Julai, badala ya Aprili kama
ilivyokuwa miaka minne iliyopita.
CHANZO:GAZETI LA TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment