Tuesday, August 20, 2013

Big Results Now ni Kioja au Faraja?



. Na mwandishi wetu,
Serikali inao maofisa wa elimu katika kila kata nchini ambao wangetumika kabisa kukusanya kero za elimu na Serikali kuu kuzifanyia kazi.Kinachoonekana sasa ni kama mpango mwingine wa kuendeleza porojo kwa kufanya vikao vinavyotumia fedha nyingi badala ya kuboresha elimu.Hali ya elimu nchini inaonekana kuendelea kuwa mbaya licha ya ahadi nyingi za Serikali  kuiboresha.
Mojawapo ya sababu za kuwepo kwa hali hiyo mbaya, inaelezwa ni mazingira duni ya kufundishia, uhaba wa vifaa na walimu kutoridhishwa na malipo kwa kazi wanazofanya.
Agosti 15, mwaka huu Serikali ilizindua utekelezaji wa mkakati wa ‘Matokeo Makubwa Sasa’ katika elimu nchini, huku sekta hiyo ikionekana kudidimia.

Elimu ni miongoni mwa sekta sita zilizochaguliwa katika Mpango wa Serikali hivi karibuni wa kuleta Matokeo Makubwa Sasa. Sekta nyingine ni Nishati, Maji, Miundombinu, Kilimo na Fedha. Sekta hizi sita zimechaguliwa ziwe za mwanzo katika kutekeleza Mpango huu wa Serikali ili kuiletea nchi matokeo makubwa kwa haraka.
Sekta hizi zinabeba msingi wa kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi kwa ujumla na kuchochea ustawi wa maisha bora kwa Watanzania wote.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa aliyezindua utekelezaji huo, Jijini Dar es Salaam, anasema katika sekta ya elimu, washiriki 34 kutoka taasisi 31 zikiwemo za Serikali na zisizo za Serikali, washirika na wadau wa maendeleo ya elimu walikutana kati ya 25 Februari hadi 05 Aprili, 2013, kutafakari kwa kina changamoto zinazoathiri sekta ya elimu.
Changamoto kubwa iliyoainishwa ni kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi kimeongezeka, ubora wa elimu umeshuka, hususan kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu katika Elimu ya Msingi na Sekondari. Kuboresha elimu ni kichocheo muhimu katika kuleta maendeleo nchini. Ingawa ufaulu siyo kiashiria pekee cha ubora wa elimu, kwa sasa ni muhimu kutumika kupima ubora wa elimu nchini kwetu.
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne yalivyokuwa
Asilimia 60 ya watahiniwa walipata alama sifuri yaani walifeli.
Mchanganuo ni kama hivi;
Matokeo ya kidato cha nne 2012: Alama 1 (0.4%) Alama 2 (1.6%) Alama 3 (3.9%) Alama 4 (26.0%) Alama 0 (60.1%).
Baadhi ya wananchi wanasema huenda ikawa ni mipango mizuri, cha msingi ni itekelezwe kwa vitendo. Hata hivyo baadhi wana hofu kwamba hakuna chochote cha maana kinaweza kutokea kwa sababu kwa staili ya sasa walimu hupatikana kutokana na waliofeli.
CHANZO MWANANCHI

No comments:

Post a Comment