Friday, August 23, 2013

Ziwa Rukwa kugeuka bwawa mwaka 2023

Ziwa Rukwa likiwa katika hatari ya kugeuka bwawa

Albano Midelo

Utafiti umebaini ziwa Rukwa upande wa wilaya ya Chunya Mbeya linandelea kusinyaa kwa kasi  kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu wilayani humo.

Ziwa Rukwa linapita katika wilaya za Chunya na Momba mkoani Mbeya,wilaya za Sumbawanga na Nkasi mkoani Rukwa na wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.

 Utafiti ambao umefanyika mwezi Juni mwaka huu katika wilaya ya Chunya umebaini kuwa mto Lupa ambao ni mto mkubwa kuliko mito yote inayoingiza maji katika ziwa hilo ukitoa wilayani Chunya umekauka kabisa na hivi sasa hakuna maji ambayo yanatiririka kwenda ziwani kupitia mto huo.

Miaka michache nyuma mto Lupa ulikuwa unatiririsha maji karibu mwaka mzima isipokuwa mwezi Novemba ndiyo ulikuwa unaweka visiwa lakini kwa mara ya kwanza mwaka huu hadi kufikia mwezi Juni mto umekauka kabisa na hakuna maji yanayoingia ziwa Rukwa kutokea mto Lupa jambo ambalo linahatarisha uwepo wa ziwa Rukwa.


Hata hivyo  Mto Songwe unaomwaga pia maji yake ziwa Rukwa ambao unaanzia milima ya Umalilia wilayani Mbeya ndiyo mto pekee uliobakia kutokea wilayani Chunya unaendelea kumwaga maji yake mwaka mzima katika ziwa Rukwa .

Kutokana na uharibifu mkubwa unaotishia kukauka kwa ziwa Rukwa serikali wilayani  Chunya imeamua kuchukua maamuzi magumu ya ya kusimamisha biashara ya kilimo  kwenye ardhi oevu pembezoni mwa ziwa Rukwa na mito ya Lupa na Songwe ambavyo vinachangia kuharibu vyanzo vya maji ambapo hivi sasa mito na ziwa vipo katika hatari ya kukauka.

Moja ya fukwe katika kijiji cha Totowe iliyokauka kwa km 10
 Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro anasisitiza kuwa malisho ya mifugo na kilimo katika ardhi oevu inasimamishwa kuanzia mwaka huu na kwamba serikali kuanzia sasa itakuwa kama msumeno unaokata pande zote kwa kupambana na wafugaji wanaolisha mifugo katika ardhi oevu pamoja na wakulima wanaoendesha kilimo katika maeneo oevu ambayo hayaruhusiwi kisheria.

“Sisi kama serikali tumeweka mkakati mzito wa kuhakikisha kuwa watoto wetu watakapokuwa watu wazima walikute ziwa Rukwa likiwa salama na  samaki wa aina mbalimbali,hivi sasa ziwa linajaa tope na mchanga kutokana na uharibifu wa mazingira ya mito na ziwa,hatua zisipochukuliwa kesho na kesho kutwa ziwa linaweza kugeuka kuwa bwawa’’,alisema.

Kulingana na mkuu wa wilaya sheria ipo wazi ya faini ya shilingi laki tatu kwa mtu anayelima katika ardhi oevu, kulisha mifugo au kulima kwenye eneo la hifadhi

Mkuu wa wilaya ameyataja madhara ya mito mikubwa ya Songwe na Lupa kushindwa kupeleka maji katika ziwa Rukwa ni pamoja  wakazi wote wa tarafa za Songwe na Kwimba ambao wanategemea samaki kama kitoweo kukosa samaki,wavuvi watakosa ajira,chakula bora kitakosekana na viumbehai wote wanategemea ziwa hilo watapata athari mbalimbali za kimazingira na hata wengine kutoweka kwenye uso wa dunia.

Mifugo mingi iliyopo katika bonde la Songwe inayokadiriwa kuwa zaidi ya 500,000 imesababisha fukwe za ziwa Rukwa upande wa Bonde la Songwe zilizopo kwenye vijiji vya kata ya Totowe   kukauka na kusababisha ziwa hilo kupungua  ukubwa na kina hali inayohatarisha uwepo wa ziwa hilo ambalo linashika nafasi ya nne kwa ukubwa hapa Tanzania likitanguliwa na maziwa ya  Tanganyika,Viktoria na Nyasa.

 Fukwe ambazo zinapotea kwa kasi ni pamoja na fukwe ya Handeni ambayo imekauka kwa kilometa 10,Ihovyo kilometa tatu,Mtanda kilometa saba,kisiwani kilometa tisa,kambipotea kilometa tano,Kwaboko  kilometa sita na fukwe ya Mchangani kilometa tano.Kina cha maji katika fukwe hizo  hivi sasa ni chini ya  meta moja .

 “Fukwe hii ya kisiwani mwaka 1998 ilikuwa kilometa nane kutoka hapa ,unaweza kutembea katika kina cha maji chini ya magoti hadi umbali wa meta 300 ndani ya ziwa,hali hii ikiendelea ziwa hili linaweza kukauka au kuwa bwawa ’’, anasema John Mwakyoma mvuvi katika ziwa Rukwa.

 Peter Sasawata na Stanley Rwamba  ni wavuvi katika fukwe ya Mtanda wanasema fukwe hiyo mwaka 1994 ilikuwa kilometa saba kutoka hapo ilipo leo na kwamba chanzo kikuu cha kukauka kwa fukwe ni mifugo mingi ambayo inaingia kunywa maji na kula malisho ndani ya ziwa kila siku.

 “Mimi nimeishi katika kijiji cha Ihovyo kwa miaka 11 wakati nafika hapa maji ya ziwa hili ulikuwa unayakuta baada ya kutembea kwa dakika tano tu lakini hivi sasa inakulazimu kutembea zaidi ya saa mbili ndipo unalikuta ziwa ’’,anasema Beston Mwambene mwalimu wa shule ya  msingi Ihovyo .

 “Kama kweli serikali inataka kuliokoa ziwa Rukwa lisipotee kwenye uso wa Dunia,waache kuendekeza siasa kwenye mazingira, ziwa Rukwa litakauka, wakulima wanazidi kusogeza mashamba ya mpunga kwenye fukwe za ziwa’’,anasisitiza Mwambene.

Afisa wa bonde la maji la Rukwa  Idris Msuya anasema  kuwa  maelfu ya mifugo  ambayo inaishi, kula na kunywa  maji  ziwa Rukwa kwenye fukwe za kijiji cha Totowe  inatishia uwepo wa ziwa hilo.

 Hata hivyo Msuya alikiri kina cha maji cha ziwa Rukwa kinaendelea kupungua kwa kasi mwaka hadi mwaka kutokana na uharibifu wa mazingira unaochangiwa  na idadi kubwa ya ng’ombe katika wilaya zinazozunguka ziwa Rukwa ambazo alizitaja kuwa ni Chunya, Mbeya, Sumbawanga, Mpanda, Mbozi na Nkasi.

Kulingana na Msuya, Ziwa Rukwa hivi sasa lina wastani wa kina cha juu cha maji cha mita tisa tu  kiasi ambacho kitaalamu ni mbaya na kwamba kina cha chini ni mita nne , eneo la maji la ziwa hilo ni  kati ya kilometa 800 hadi 2300 kutegemeana na kiasi cha  mvua inayonyesha na kwamba utafiti umebaini kuwa katika kipindi cha mwaka  1970 hadi 2006 Ziwa Rukwa limepungua kwa kiasi cha zaidi ya kilomita saba.
Mto Songwe,mto pekee unaomwaga maji ziwa Rukwa kwa mwaka mzima

Waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe ametahadharisha kuwa kuna hatari kubwa ya Ziwa Rukwa kukauka katika kipindi cha miaka kumi ijayo endapo uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa vyanzo vya maji unaofanywa na wakazi wa maeneo yanayozunguka ziwa hilo hautadhibitiwa haraka.


 Profesa Maghembe ametoa rai kwa mamlaka zinazohusika  kujipanga vizuri ili kukabiliana na uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo kutumia sheria ndogo ndogo zilizopo kila Halmashauri nchini ili kudhibiti uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi ya watu  katika vyanzo vya maji.


Kulingana na Prof. Maghembe Sheria ndogo ndogo zilizotungwa na Halmashauri hazinabudi kuanza kutumika ili kudhibiti tabia iliyojitokeza hivi sasa ya baadhi ya watu kulima katika vyanzo vya maji.


Utafiti ambao ulifanywa katika Ziwa Rukwa kata za Ivuna na Kamsamba wilayani Momba umebaini viumbe hai wakiwemo ndege maarufu aina ya  nyange nyange na bata maji wapo katika hatari ya kutoweka kutokana na fukwe nyingi kukauka na ziwa kujaa tope.

 
Waziri mkuu, Mizengo Pinda amesema kuwa Ziwa Rukwa lipo hatarini kukauka, kutokana na kina chake cha maji kushuka. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Sumbawanga ng’ara kinachohusu masuala ya udhibiti wa mazingira, Pinda alisema katika kipindi cha miaka 50 ijayo ziwa hilo litakuwa limekauka.


Kufuatia kuwepo kwa hali hiyo waziri mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (mazingira) kuhakikisha wanalifanyia kazi suala hilo ili kulinusuru ziwa hilo.



 Wataalamu wa mazingira wanazitaja baadhi ya athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira duniani kuwa  ni pamoja na kupungua kwa mvua, majira kubadilika na kuongezeka kwa vipindi vya ukame, kupungua kwa kasi ya theluji katika ncha ya kaskazini na kusini na kwenye vilele vya milima kote dunia  ukiwemo mlima Kilimanjaro.



Athari nyingine ni  kupungua kwa kina cha maji katika maziwa mbali mbali na katika nchi yetu maziwa yanayoathirika ni Ziwa Tanganyika, Victoria na Ziwa Rukwa, kuongezeka kwa kina cha bahari na kuathiri maeneo ya nchi kavu baadhi yake yamezama na mengine yako hatarini kuzama ambapo hapa Tanzania kisiwa cha Maziwe kilichopo katika Bahari ya Hindi kimezama.







No comments:

Post a Comment