Saturday, August 24, 2013

Bunge labaini Ufisadi wa kutisha hazina


           Na mwandishi wetu
Waziri wa fedha Dk.William Mgimwa
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imebaini mtandano wa baadhi ya maofisi wa Hazina ambao kwa kushirikiana na halmashauri wanachote fedha za serikali kwa njia ya kuzidisha viwango vinavyokuwa vimeombwa.
Akizungumza na waandishi wa habari  katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mohamed Mbarouk, alisema kupitia mtandao huo wa kifisadi zaidi ya sh bilioni moja zimetoroshwa kutoka Hazina kupitia halmashauri mbalimbali nchini.Alisema mchezo huo umefanywa na baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu na kuzitaja baadhi ya halmashauri za wilaya hizo kuwa ni Mbarali ambako waliingiziwa sh milioni 700 na hazina badala ya sh milioni 70 zilizokuwa zimeombwa.Mbarouk aliitaja pia halmashauri ya wilaya ya Korogwe mjini kuwa iliingiziwa milioni 500 wakati ile ya Mvomero nayo ikingiziwa sh milioni 89 zaidi ya mahitaji yao.

Alisema mtandao huo wa walanguzi baada ya kutekeleza azma yao hiyo huzitakatisha fedha hizo kwa kuzirudisha kwa ajili ya maslahi yao binafsi na hivyo kuitia hasara serikali.
“Tulichogundua ni utoroshaji wa fedha nyingi za serikari kutoka hazina kwenda kwenye njia haramu jambo lililotushangaza,” alisema.
Akizungumzia hati za hesabu zisizoridhisha za halmashauri nchini, Mbarouk alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita, zimepungua ikiliganishwa na kipindi cha nyuma.
Alisema kiumjumla bado yapo matatizo ya watendaji wa halmashauri hizo kutokuwa na nidhamu ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi.
“Halmashauri nyingi zimekutwa na matumizi ya fedha za miradi huku baadhi ya watendaji wakishindwa kutoa maelezo ya jinsi zilivyotumika jambo ambalo linatia shaka wakati wote,” alisema.
Mbarouk alisema kamati imewaagiza wakurugenzi wote wahakikishe kila tofauti iliyojitokeza kipindi hiki inasawazishwa na isitokee tena.
Wakati huohuo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imekataa kupitisha ripoti ya hesabu ya mwaka 2011/12 za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutokana na dosari ikiwemo kufanya matumizi ya sh bilioni tisa kwa ajili ya kulipana posho za vikao vya mabaraza ya wafanyakazi.
Mbali na hilo ripoti hiyo imebaini mamlaka hiyo kufanya manunuzi yao kiholela bila kuzingatia sheria ya manunuzi ya umma ambapo walitumia sh bilioni 30 kwa manunuzi ya vifaa bila kuwa na kibali cha Wizara ya Fedha na Uchumi.
Akizungumza jana na watendaji wa mamlaka hiyo walioambatana na Mwenyekiti wa Bodi wa Bandari, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe, alisema kuwa kamati imeikataa ripoti hiyo na wanamuandikia barua Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ili kufanya ukaguzi maalum katika maeneo yenye dosari.
Filikunjombe alisema kuwa CAG atalazimika kupitia upya maeneo hayo ambayo hesabu zake zina utata ikiwemo matumizi ya sh bilioni 6.2 yaliyofanywa na mamlaka hiyo kwa ajili ya kugharamia matangazo.
“Huu ni uzembe na ni lazima hili lifanyiwe ukaguzi. Hivi unaposema mmetumia sh bilioni 6.2 kwa ajili ya matangazo ina maana leo kila Mtanzania ukimuuliza shughuli mnazofanya atakuwa anazifahamu?” alihoji.
Aliongeza kuwa taarifa za matangazo hayo zinaonekana tofauti katika ripoti hiyo wakati ni kitu kimoja.
“Unaposema katika ripoti umefanya publicity na advertisement kwa gharama tofauti hapo unamaanisha nini, hicho si ni kitu kimoja jamani au nakosea,” alisema.
Kiukweli ni kuwa publicity hailipiwi isipokuwa advertisement.
Alisema kuwa Utouh anatakiwa kufanya ukaguzi pia katika eneo la safari za watendaji wa mamlaka hiyo ambao wametumia sh bilioni 10 kwa ajili ya posho za safari pekee.
Filikunjombe aliwataka watendaji hao kuwa wazi iwapo matumizi hayo yamekuwa yakihusisha na wizara ya uchukuzi.
“Labda mkurugenzi utueleze kama fedha hizo zinagharamia na watu wa wizara yenu maana kuna maeneo mengine tumepata malalamiko hayo ya mamlaka kuombwa fedha.”
Alisema kuwa katika ripoti hiyo kwa mara nne mfululizo imeonyesha jinsi mamlaka hiyo inavyoshindwa kuzingatia manunuzi ya umma hatua iliyosababisha kufanya manunuzi yao kiholela ya kununua vifaa vya sh bilioni 30 bila kibali.
Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa (CCM), alisema kuwa mamlaka imetumia sh bilioni 3.2 kwa ajili ya kulipa matibabu ya wafanyakazi na kutaka kuanzia sasa mamlaka hiyo ijiunge na Mfuko wa Bima ya Afya ili kuepuka upotevu wa fedha za serikali.
“Yaani kuna wizi unaofanyika huwezi kusema umejaza magari mafuta ya lita 100; ni gari lipi hilo lazima tuangalie hilo na CAG afanye ukaguzi upya na tutakutana nanyi Desemba mwaka huu,” alisema.
Naye mjumbe wa kamati hiyo, Esther Matiku (CHADEMA), alihoji hatua ya mamlaka hiyo kumpatia zabuni ya ujenzi wa mnara wa Bandari ya Mtwara mzabuni ambaye hakushinda huku akiachwa aliyeshinda na ambaye ana vigezo.
Alishangazwa na mamlaka hiyo kuamua kuunganisha kwa pamoja thamani ya ardhi na majengo yao jambo ambalo limewasababishia kupata hati chafu.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), alihoji sh milioni 100 zilizotolewa kwa mkandarasi wa bandari ya Tanga ambaye hakufanya kazi hiyo na badala yake alitokomea kusikojulikana.
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Madeni Kipande, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa kazi hiyo ilikuwa ifanyike kwa sh milioni 500 lakini walitoa fedha za kuanza kazi sh milioni 100.
CHANZO GAZETI LA TANZANIA DAIMA


No comments:

Post a Comment