Hakuna shaka kwamba umewahi kusafiri nje ya nchi
yako na kutakiwa kupata chanjo.Kwa wengine, chanjo hiyo ikiwamo ya homa ya ini
imeonekana kama usumbufu na udhia mtupu. Hata hivyo, wapo wengine ambao
hawaufahamu ugonjwa huu.
Kwa wanaoujua, wanahofia kuwa ugonjwa huu una
madhara makubwa pengine kuliko saratani na Ukimwi.Homa hiyo au Hepatitis
B inapewa uzito mdogo licha ya kuwa ni ya hatari kubwa.Wataalamu
wanaeleza kuwa Hepatitis B au homa ya ini ni ugonjwa unaoambukizwa kwa urahisi,
wenye madhara makubwa na wenye uwezo wa kuambukiza kwa wepesi kuliko Ukimwi.
Kitaalamu, ugonjwa huu, husababishwa na virusi
vya Hepatitis B (HBV) ambavyo huathiri mfumo wa utoaji wa sumu mwilini.
Inaelezwa kuwa robo tatu ya watu ulimwenguni wameathiriwa kwa muda na homa ya
ini na wengine milioni 350 wameathirika moja kwa moja.
Takwimu zinaonyesha kuwa homa ya ini huua watu
600,000 kila mwaka katika sehemu mbalimbali, idadi ya watu inayolingana na wale
wanaokufa kutokana na malaria.Maradhi haya ya ini yanaelezwa kuwa yanaweza
kusababishwa na kunywa kileo kupita kiasi au sumu inapoingia mwilini.Hata
hivyo, mara nyingi ugonjwa huu husababishwa na virusi.
Wanasayansi kwa upande mwingine wamegundua virusi
vitano vinavyosababisha ugonjwa huu na wanasema kwamba huenda kuna vingine
vitatu.Matokeo yake, sheria zimewekwa katika nchi mbalimbali ambazo
zinamtaka kila raia mgeni anayetaka kuingia katika nchi husika, kupata chanjo
ya ugonjwa huu ili kuepusha maambukizi.Kila anayechanjwa hupewa kadi
maalum itakayomwezesha kuingia katika nchi husika ili kuthibitisha kuwa
amechanjwa.
Hata hivyo, ujanja mwingi umekuwa
ukifanyika katika baadhi ya nchi ikiwamo Tanzania ambapo watu hujipatia kadi za
homa ya manjano kwa kutoa rushwa na kukwepa kuchoma chanjo hiyo pindi
wanapotaka kusafiri nje ya nchi bila kujua madhara ya kutopata chanjo
hiyo. Vilevile, chanjo hiyo iliwahi kukosekana nchini kwa zaidi ya mwezi
mmoja kutokana na sababu ambazo haziwekwi wazi na mamlaka zinazohusika.
Hatari kubwa ya ugonjwa huu inatajwa ni namna ya
uambukizaji wake ambapo, unaposhika damu au majimaji ya mwilini ikiwemo mbegu
za uzazi huweza kuambukizwa. Wataalamu wanaeleza ubaya wake ni kuwa
unaweza kuambukizwa kwa kufanya ngono na hata kwa kushika majimaji ya mwili wa
mtu aliyeathirika ikiwemo damu, mate, machozi na mkojo.
Taarifa za Shirika la Afya Duniani(WHO) zinaeleza
kuwa kirusi cha homa ya ini kinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu kwa
siku saba na kwa wakati huu, kirusi hiki kinaweza kusababisha maambukizi iwapo
mtu hajapata chanjo ya kuuzuia.Watanzania wengi bila kujua wamekuwa wakiugua
maradhi mbalimbali yanayosababishwa na homa ya ini na bila kufahamu ini
limekuwa likiathirika taratibu.
Dk Yuki Mark wa Hospitali ya Parktown North,
Johanesburg, nchini Afrika Kusini anasema kuwa homa ya ini aina ya B inaweza
kuua kimyakimya bila kuonyesha dalili zozote.“Huenda dalili zikaonekana
waziwazi miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa. Zinapoonekana, huenda tayari ini
limenyauka au lina saratani na magonjwa hayo huua asilimia 25 ya watu walio na
virusi vya HBV,” anasema Dk Mark.
Aidha, mtaalamu huyo anasema, dalili kuu
zinazojulisha kuwa mtu ana homa ya ini ni kutapika, kuchoka kupita kiasi,
kuathirika kwa ini, homa na mkojo kuwa wenye rangi ya njano iliyokolea
sana.“Unaweza kuharisha na kutapika au kupata maumivu katika eneo fulani la
tumbo lako, macho na ngozi kuwa vya njano,” anaeleza.
Homa ya ini aina ya B, inaweza kuingia mwilini
mwa mtu kwa njia ya ngono, kama ilivyo Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa.
Hivyo basi, majimaji katika mwili wa mwanadamu yanaweza kuwa chanzo
cha maambukizi.
“Watu wengi wanaendelea kuambukizwa kwa
kutiwa damu yenye virusi hivyo, hasa katika nchi ambako hakuna vifaa bora vya
kuchunguza virusi hivyo katika damu. Virusi vya HBV vina uwezo mkubwa zaidi wa
kuambukiza kwa kulinganishwa na virusi vya Ukimwi,” anasema Dk Mark
Anaongeza: “Hata kiasi kidogo cha damu yenye
virusi hivyo kama ile inayobaki kwenye wembe, inaweza kupitisha virusi hivyo na
tone la damu iliyokauka kwa juma moja au hata zaidi inaweza kumwambukiza mtu
virusi hivyo.”Dk Mark anasema, madhara mengi huweza kumkumba mtu aliyepata
maambukizi ya homa ya ini, kwani anaweza kupata shinikizo la damu, anaweza
kuathirika ubongo au hata kupooza sehemu ya mwili wake.
Angalizo ambalo mtaalamu huyo anaeleza ni kuwa
baada ya mtu kuambukizwa homa hiyo, hawezi kupona, kwani dawa kuu ya ugonjwa
huu ni chanjo ya kuzuia homa ya manjano (yellow fever vaccination).
CHANZO NI GAZETI LA MWANANCHI

No comments:
Post a Comment