![]() |
| Sehemu ya jiji la Johannasburg nchini Afrika ya kusini |
Na Albano Midelo
HIVI karibuni
nimemaliza mafunzo maalum ya uhifadhi nchini Afrika ya kusini ambako nimeweza
kutembelea maeneo karibu yote muhimu katika nchi hiyo inayotajwa kuwa na
maendeleo makubwa hata kuzidi baadhi ya nchi za Ulaya.
Takwimu za uchumi duniani zinaonyesha kuwa nchi ya kwanza kwa uchumi mzuri ni Marekani ikifuatiwa na nchi ya China ambapo nchi ya Afrika ya kusini inashika nafasi ya tatu kiuchumi duniani.Hata hivyo nchi ya China inadaiwa mwaka 2050 itakuwa nchi ya kwanza kwa uchumi bora duniani ambayo inatarajia kuizidi Marekani mara mbili.
Katika makala haya
nitayaweka wazi baadhi ya mambo ambayo mimi binafsi yamenifurahisha kiasi
kwamba endapo nchi yetu inaweza kuiga baadhi ya mambo basi tunaweza kupiga hatua
katika maendeleo ya kijamii,kiuchumi na kisiasa.Wananchi wa Afrika ya
kusini sasa wanachapa kazi kwa bidii huku uzalendo
wa kweli katika nchi yao wakiwa wameuweka mbele kuliko kitu chochote.
Jambo la kwanza
ambalo limenifurahisha katika nchi ya Afrika ya kusini ni serikali ya nchi hiyo
kuwajali wananchi wake kwa kutambua kuwa mwananchi ndiyo mwajiri mkuu wa
viongozi wote serikalini kuanzia ngazi ya chini hadi Rais wa nchi.
![]() |
| Moja ya barabara za Afrika ya kusini zenye viwango vy |
Katika nchi ya Afrika
ya kusini kila mwananchi anaruhusiwa kuingia eneo la Ikulu ya nchi hiyo iliyopo
Pretoria kuanzia asubuhi hadi saa 12 jioni ambako anaweza kufanya lolote ikiwa
ni pamoja na kupiga picha na kufanya mazoezi ndani ya viwanja vya Ikulu bila kuomba
kibali serikali.
Hapa nchini jambo
hilo ni ndoto kwani Ikulu ya Dar es salaam huwezi kuingia bila
kibali,watanzania wanaogopa eneo la Ikulu kwa kuwa ni makazi ya Rais,lakini
nchini Afrika ya kusini wananchi wanaingia Ikulu kama nyumbani kwao unaweza kupiga
picha na kufanya lolote hakuna mtu anayekuuliza kwanini Tanzania tusiige jambo
hili ili watu waweze kuingia Ikulu bila mizengwe.
Jambo la pili ambalo
limenifurahisha nchini Afrika ya kusini ni utaratibu mzuri waliouweka kuhusu
askari wa barabarani ambao wamedhibitiwa kiasi kwamba hawana nafasi ya kuchukua
rushwa kutoka katika vyombo vya moto vya usafiri kama ilivyo hapa Tanzania.
Katika nchi ya Afrika
ya kusini kila mtu anafahamika mtaa na namba ya nyumba anayoishi,hata kama
nyumba hiyo ni ya chumba kimoja imepewa namba.Pia kila mwenye chombo cha
usafiri anafahamika endapo amefanya kosa la barabarani ,wenzetu wameweka kamera
maalum ambazo zinapiga picha makosa yote yanayotokea barabarani.
Iwapo dereva amefanya
kosa barabarani kwa mfano kwenda mwendo kasi anapigwa picha na siku inayofuata
analetewa faini nyumbani kwake ili aweze kulipa kulingana na kosa lake hivyo
askari wa barabarani hawana nafasi ya kuomba rushwa kama ilivyo hapa Tanzania
ambapo askari wa barabarani kuomba rushwa kwa madereva imekuwa ni kitega uchumi
chao kwa kuwa wanaomba rushwa bila aibu.
Nadhani utaratibu
kama wa Afrika ya kusini ungefanyika hapa nchini rushwa kwa askari wa
barabarani ingemalizika na pesa nyingi ingeingia serikalini,utaratibu huu
ungepunguza makosa ya barabarani kama ilivyo nchini Afrika ya kusini ambako
hata ajali zinatokea mara chache ,madereva wapo makini kuhofia kufanya makosa
ambayo yangedhibitiwa.
Katika usafiri wa
abiria wa daladala nchini Afrika ya kusini wenzetu wamepiga hatua kubwa kwa kuwa wameweka
utaratibu mzuri ambapo daladala zinabeba watu wanaokuwa wamekaa kwenye
viti,tena katika daladala hizo hakuna kondakta,abiria waliopo wakiwa tayari
abiria mmoja anamkusanyia dereva pesa na kumkabidhi kisha gari linaondoka. Hapa
Tanzania daladala zetu kila mmoja anajua kero iliyopo.
Jambo la tatu ambalo
limenifurahisha sana ni wananchi wa Afrika ya kusini kuwa na uzalendo wa kweli
katika nchi yao.Serikali ya Afrika ya kusini ni mfano wa kuigwa kutokana na
kumpatia heshima kubwa Rais mstaafu Nelson Mandela ambapo nyumbani kwake SOWETO
wameanzisha makumbusho maalum ya Nelson Mandela.
Makumbusho hiyo ina
kila kitu cha Rais mstaafu Mandela ikiwemo Nyumba yake,vitu mbalimbali
alivyotumia kama vile kitanda alichokuwa analalia,mkanda wa ngumi alioshinda
wakati anacheza mchezo wa ngumi,viatu vyake,samani mbalimbali alizotumia,barua
alizokuwa anaandika akiwa gerezani,miti aliyopanda pamoja na vivutio vingine
vingi ambavyo vinawavutia wengi wanaotembelea SOWETO katika nyumba ya Mandela.
Unapofika katika
nyumba ya Mandela muda wote unakutana na watalii kutoka nchi mbalimbali duniani
ambao wanalipa fedha nyingi kuangalia vivutio na kupata habari za Rais mstaafu
Nelson Mandela.
Makumbusho ya Nelson
Mandela ya SOWETO imeanzishwa mara baada ya kustaafu kwa Rais huyo kipenzi cha
watu wa Afrika ya kusini.Watanzania tumeshindwa kuanzisha makumbusho ya mwalimu
Nyerere licha ya kwamba amefanya mengi katika nchi hii.
Hata hivyo
hatujachelewa serikali inaweza kuanzisha makumbusho ya mwalimu Nyerere na
kuweka vitu vyote alivyofanya kabla ya kuwa Rais,baada ya kuwa na Rais na mara
baada ya kustaafu kama wenzetu Afrika ya kusini wanavyomuenzi Rais wao kila
kona ya nchi yao ambako wameweka picha yake na maeneo mengine wameweka video
yake ambayo inaonyesha kazi alizokuwa anafanya kwa ajili ya Afrika ya kusini.
Mzee Mandela ingawa
hivi sasa anaumwa yupo mahututi katika hospitali ya Medical Clinic mjini
Pretoria,bado serikali ya nchi hiyo inauzalendo wa hali ya juu kwa kuwa
kutokana na nafasi ya mzee Mandela katika nchi hiyo angeweza kwenda kutibiwa
katika nchi za Ulaya na Marekani ambazo zinaaminika
kuwa na hospitali zenye huduma bora zaidi,hata hivyo serikali inayoongozwa na
Rais Zuma imeamua kumtibu mzee Mandela ndani ya nchi yao huu ni uzalendo unaofaa
kuigwa na nchi nyingine kama Tanzania ambayo viongozi wake wengi wakiugua
wanakwenda kutibiwa nje ya nchi.
Jambo jingine ambalo
watanzania tunatakiwa kujifunza kutoka Afrika ya kusini ni uzalendo walionao
katika maliasili za Taifa ambapo idadi ya wananchi wanaofanya utalii wa ndani
ni kubwa kuliko watalii wanaotoka nje. Hapa Tanzania ni tofauti tunategemea
zaidi watalii wa kutoka nje ya nchi hivyo endapo watalii wa nje wanapungua
sekta ya utalii inaathirika kwa kuwa watanzania hatuna utamaduni wa kufanya utalii
wa ndani.
Hata hivyo hali hiyo
inachangiwa na serikali kwa mfano sekta ya utalii nchini Afrika ya kusini kila
mwaka inatengewa bilioni 200 wakati hapa Tanzania inadaiwa serikali inatenga
shilingi bilioni sita tu kwa ajili ya utalii.
Vivutio vya utalii
vilivyopo nchini Afrika ya kusini kama vile hifadhi ya Taifa ya Kluger ambayo
inatajwa kuwa kubwa kuliko zote barani Afrika haina wanyama wengi kama zilivyo
hifadhi za Taifa za Tanzania za Serengeti,Ziwa Manyara,Mikumi,Ruaha na
nyinginezo ambazo zina wanyama wengi wa aina mbalimbali ambao wanapatikana
kirahisi.
Katika hifadhi ya
Kluger wanyama ni wa kutafuta,anapatikana mmoja mmoja lakini kwa kuwa serikali
ya nchi hiyo imewekeza kikamilifu katika sekta ya utalii kwa kuitangaza hifadhi
hiyo,watalii wengi wa ndani na nje ya nchi wanaitembelea hifadhi hiyo kila siku
na serikali kuingiza fedha nyingi ambazo zinaimarisha uchumi wa nchi ya Afrika
ya kusini hivyo basi serikali ya Tanzania inatakiwa kubadilika na kuongeza
bajeti kwa ajili ya matangazo ya vivutio kwenye sekta ya utalii ili kupata
mafanikio makubwa katika sekta hiyo.
Sio hayo tu katika
nchi ya Afrika ya kusini sio jambo rahisi kwa wafanyabiashara wakubwa na
wananchi wa kawaida kukwepa kulipa kodi kutokana na utaratibu mzuri ambao
umewekwa na nchi hiyo unapoingiza bidhaa toka nje,kununua na kuuza ambapo
serikali inapata kodi yake kikamilifu na hakuna ukwepaji kodi kama unaofanyika
hapa nchini.Bidhaa za ndani ya nchi hiyo zimepewa kipaumbele na hakuna bidhaa
feki zinazoingizwa nchini Afrika ya kusini tofauti na hapa nyumbani Tanzania
ambako ni jalala la bidhaa feki.
Wenzetu katika
utunzaji wa mazingira wamepiga hatua kubwa kwa mfano ukitembelea katika mitaa
ya jiji la Johannesburg huwezi kuona takataka ambazo zimezagaa ovyo kama ilivyo
katika jiji letu la Dar es salaam,ukiangalia barabara za jiji la Johanasburg
zinavyovutia unaweza usitamani kuondoka katika jiji hilo.
Magari yaliopo katika
jiji la Johansberg yanatajwa kuwa ni mengi zaidi ukilinganisha na idadi ya
magari yaliopo katika jiji la Dar es salaam,hata hivyo kutokana barabara bora
zilizojengwa chini,katikati na juu zinasababisha jiji hilo kutokuwa na foleni
ya magari kama iliyopo jijini Dar es salaam ambako foleni imekuwa kero kubwa
kwa wakazi wa jiji hilo.
Kuna mengi ambayo
tunaweza kujifunza kutoka nchini Afrika ya kusini,kinachotakiwa ni kubadilika
kifkra na kimawazo kuanzia viongozi wetu waliopo madarakani hadi wananchi.Natambua
kuwa kutokana na maendeleo makubwa iliyonayo nchi ya Afrika ya kusini,tunaweza
kukata tamaa na kusema kuwa hatuwezi kujilinganisha na nchi hiyo badala yake labda
tuendelee kujilinganisha na nchi za Afrika Mashariki zikiwemo Kenya,
Uganda,Rwanda na Burundi.
Waswahili walisema Roma haikujengwa kwa siku
moja,tukiamua kujenga nchi yetu tunaweza lakini watanzania tunabomoa nchi yetu
kutokana na mambo mbalimbali yaliokithiri ikiwemo rushwa,ufisadi,ukosefu wa
viongozi bora na wenye uzalendo na ukosefu wa uwajibikaji na uaminifu.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129



No comments:
Post a Comment