Monday, September 2, 2013

Mandela atolewa hospitalini Pretoria



Inayoonekana kwa mbali ni hospitali alikokuwa amelazwa mandela

 Na Mwandishi wetu

 

 Serikali ya Afrika Kusini imethibitisha kuwa Rais wa zamani, Nelson Mandela ametolewa hospitali ambako amekuwa akitibiwa matatizo ya mapafu tangu Juni mwaka huu.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa katika tovuti ya Rais wa Afrika Kusini imeeleza kuwa Mandela bado ni mahututi na hali yake wakati mwingine inabadilika.
Uthibitisho huo umetolewa siku moja baada ya maofisa wa Serikali ya nchi hiyo kukanusha taarifa kwamba Mandela (95) amerudishwa nyumbani kwake, Johannesburg juzi.
Taarifa zilieleza kwamba madaktari wake wanaamini akiwa nyumbani kwake atapata matibabu sawa na yale ya hospitali... “Wameweka sawa mazingira yake huko Houghton ili aweze kupata matibabu aliyokuwa akiyapata hospitali.”
Serikali imesema inamtakia mema wakati akiendelea na matibabu.
Juzi Serikali ya Afrika Kusini ilikanusha habari za baadhi ya vyombo vya habari zilizosema kwamba Mandela ameondolewa hospitali. Msemaji wa Rais wa Afrika Kusini, Mac Maharaj alisema, Mandela bado yuko hospitali anaendelea vizuri lakini hali yake bado ni mbaya.

Kauli hiyo imekuwa ikitumiwa na Serikali ya Afrika Kusini kuelezea hali yake Mandela tangu alipolazwa hospitali mwanzoni mwa Juni kutokana na ugonjwa wa mapafu.
Jumamosi iliyopita, Maharaj alisema mara kwa mara afya ya Mandela imekuwa ikizorota, lakini alifaulu kukabiliana na ugonjwa wake.  Taarifa zaidi zilieleza kwamba Mandela ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, alisafirishwa kutoka Hospitali ya MediClinic, Pretoria na kupelekwa nyumbani kwake Johannesburg.
Tangu alipolazwa, watu wamekuwa wakiendelea kumwombea na kuacha ujumbe wa kumtakia heri nje ya nyumba yake.
Ilielezwa kwamba matatizo ya mapafu yanayomwandama yalitokana na kuugua kifua kikuu alipokuwa jela akitumikia kifungo cha miaka 27.
Tangu kuanza kwa mwaka huu, Mandela amelazwa mara nne lakini safari hii amekaa hospitali kwa muda mrefu zaidi.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment