Saturday, September 7, 2013

'Pendekezo la serikali tatu lipite'



Na Albano Midelo
Baadhi ya wadau wa asasi za kiraia mkoani Ruvuma
ASASI za kiraia kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma wameridhia mapendekezo ya Tume ya  rasimu ya katiba ya Jamuhuri ya Muungano iundwe  shirikisho lenye serikali tatu.


Viongozi wa asasi hizo zaidi ya 50 wamekubali mapendekezo ya Tume ya rasimu ya katibu   katika mkutano wa jukwaa la kujadili Rasimu ya katiba mpya ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ulioandaliwa  na mtandao wa mazingira mkoa wa Ruvuma (RUNEA) kwa ufadhili wa shirika la The Foundation For Civil Society.

 Wakizungumza kwenye mkutano huo wa siku tatu katika ukumbi wa Songea Klabu,viongozi hao wamesema serikali ijayo ni muhimu kuundwa na shirikisho la serikali tatu ambazo ni serikali ya Jamuhuri ya Muungano,serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Tanganyika.
Akichangia mjadala huo Nathaniel Luoga ambaye ni kiongozi wa asasi ya Mwangaza Foundation alisema kuundwa kwa serikali tatu kutaimarisha muungano na kuwezesha sasa serikali ya Tanganyika kuwa na Rais wake kama ilivyo kwa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.
Kuhusu uendeshaji wa serikali tatu Luoga alipendekeza serikali ya Jamhuri ya muungano inapaswa kuchangiwa na serikali mbili za mapinduzi Zanzibar na Tanganyika ili kuendesha shughuli zake za  muungano hatimaye iweze kutekeleza kazi zake kuanzia mwaka 2015.
Vitalis Nkomera  mwanamazingira kutoka manispaa ya Songea akichangia kuhusu muundo wa serikali tatu ameseme wanaridhia uwepo wa serikali tatu  na kusisitiza kuwa  serikali ya Jamuhuri ya muungano itakuwa ndiyo mlezi mkuu wa serikali mbili za Zanzibar na Tanganyika .
‘‘Kazi kubwa ya serikali ya Jamuhuri ya Muungano iwe ni kusimamia na kuwa mwangalizi wa  kulinda mambo yote muhimu yanayohusiana na muungano,napendekeza kuwa serikali mbili za Zanzibar na Tanganyika ndiyo zijihusishe na ukusanyaji wa mapato yanayotokana na ushuru na tozo mbalimbali,serikali ya Jamuhuri ya muungano isihusike na kutoza ushuru wala ukusanyaji mapato yenyewe itapewa gawio tu toka serikali mbili’’,alisema.
Nkomera alipendekeza serikali ya Jamhuri ya muungano kuendeshwa kama ilivyo jumuiya ya Afrika ya mashariki ambayo inaundwa na nchi  zenye serikali kamili ambazo zimekuwa zinaichangia jumuiya hiyo bila kujali kama nchi hiyo ni kubwa au ndogo na kwamba muungano  ndiyo unatakiwa kuchangiwa na wote bila kujali uwezo wa serikali husika.
Regnad Mapunda akitoa mapendekezo yake kuhusu serikali tatu ameshauri serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kuruhusiwa kutafuta vyanzo vyake vingine vya mapato bila kuingilia vyanzo vya serikali mbili zinazounda serikali ya muungano .
Mapunda pia ameshauri sehemu ya kwanza ibara ya pili katika rasimu ya katiba eneo la Jamhuri ya muungano,liondolewe eneo lote la Tanzania bara badala yake liandikwe eneo lote la Tanganyika na kuongeza kuwa rasimali zote ikiwemo bahari, maziwa, mito, milima na raslimali nyingine zilizopo zitajwe bayana katika serikali zote.
Viongozi hao wa asasi za kiraia wametaja baadhi ya faida za serikali tatu kuwa ni pamoja na kila serikali kuwa na Rais wake,katiba yake,Bunge lake na kwamba kila serikali itasimamia uchumi katika serikali yake pia serikali ya jamhuri ya muungano ambayo itasimamia mambo yote ya muungano.
Wamesema serikali tatu itawezesha kuwepo uhuru katika maamuzi katika kila serikali,migogoro ya ukusanyaji wa mapato haitakuwepo,kila serikali itakuwa na mamlaka yake kiutendaji, hata hivyo wamependekeza kuwepo na jeshi moja tu la wananchi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania na polisi na pasiwepo na jeshi kwa kila serikali.
Judith Erasto ameshauri katika rasmu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jeshi la mgambo kuingizwa katika katiba na kutambuliwa rasmi kuwa ni miongoni mwa majeshi muhimu kwa kuwa serikali kila mwaka inatoa mafunzo ya askari mgambo na mara baada ya kuhitimu wanaachwa hawafahamiki wanafanya nini.
‘‘Mgambo ni jeshi la akiba ambalo linapewa mafunzo ya kijeshi na wanajeshi wenyewe,katika rasimu ya katiba hakuna kipengele kinacholitambua jeshi la mgambo,unapowazalisha askari mgambo wengi kila mwaka bila kuwapa ajira,wale mgambo wanaweza kujiingiza hata katika vitendo vya uharifu,naomba katiba mpya ilitambue rasmi jeshi la mgambo baada ya mafunzo waweze kuajiriwa’’,alisisitiza.
Vinsent Kapinga kutoka Mbinga akichangia kuhusu serikali tatu amesisitiza kuwa  kasoro za muungano zinazojitokeza hivi sasa katika serikali mbili zitamalizika au kupungua sana mara baada ya kuwepo na serikali tatu kikatiba.
Amesema hakuna haja ya kuhofia gharama za uendeshaji kwa kuwa nchi ina rasilimali nyingi za kutosha ambazo zinaweza kusaidia katika uendeshaji wa serikali tatu ili mradi wapatikane viongozi wazalendo na wanaoweza kusimamia kikamilifu rasilimali za Taifa.
Pius Kayombo kutoka kikundi cha wenye ulemavu Peramiho anasema rasimu ya katiba ya Jamhuri ya muungano inakidhi malengo ya kuwa na serikali tatu isipokuwa amependekeza marekebisho yafanyike polepole na kwa uhakika kutokana na ukweli kuwa katiba ni kitu kigeni ambacho hakifahamiki na watanzania wengi.
‘‘Katiba ni kitu cha kudumu ikishaandikwa inaweza kutumika kwa miaka 50 hadi 100 ijayo, hivyo makosa yakifanyika leo yatawaumiza watanzania kwa miaka mingi,mchakato wa rasmu ya marekebisho ya katiba ya Jamhuri ya muungano naona unafanyika kwa haraka sana tunakimbilia wapi,watu wangepewa muda wa kutosha kuisoma na kuifanyia marekebisho kabla ya kuandikwa’’,alidai Kayombo.
Mchungaji Faustine Luoga amependekeza kuwa katika rasimu hiyo iwekwe wazi mambo yote ya maliasili za Taifa kama vile misitu,madini,maziwa na mengineyo kwa kuwa mazingira ndiyo maisha badala ya kuwekwa kwa ujumla kama ilivyo katika rasimu ya katiba hivi sasa.
Awali  mwenyekiti wa mtandao wamazingira mkoa wa Ruvuma (RUNEA) ambao ndiyo waandaaji wa mkutano huo Method Ngerangera aliyataja malengo ya kuendesha mabaraza ya katiba yanayoundwa na asasi za kiraia kuwa ni kutokana na umuhimu wa watanzania kuwa na katiba mpya ili washiriki wajadili na kutoa maoni yao juu ya vipengere vilivyopo kama vinakidhi au vifanyiwe marekebisho ili viingizwe kwenye katiba mpya ijayo.
‘‘Uendeshaji wa Baraza la  rasmu ya katiba unaangalia na kutoa haki sawa kwa wote katika kutoa mawazo au maoni ya kila mshiriki kwa kuwa lengo la Baraza hili ni kuwa hakuna mwalimu au mwanafunzi wa kutoa maelekezo yatakayotumiwa na mtu au kikundi Fulani kwa kutaka kuyakubali au kukataa maoni kwa lengo la kuwakilisha mtu,kikundi,taasisi,dini,kabila au chama Fulani kisiasa bali maoni hayo yawe na sura ya umoja’’,alisisitiza.
Naye mstahiki meya wa manispaa ya Songea Charles Mhagama akizungumza wakati anafungua mkutano huo aliwatahadharisha washiriki wote kuacha tofauti zao  zote kuhakikisha kuwa mapendekezo yote yatakayotolewa kwenye rasimu ya katiba  yawe kwa ajili ya Taifa letu la Tanzania.
Sura ya kwanza katika rasimu ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania sehemu ya kwanza,ibara ya kwanza  kifungu cha kwanza kinaonyesha Jamhuri ya muungano wa Tanzania ni shirikisho lenye mamlaka kamili ambayo imetokana na muungano wan chi mbili za Tanganyika na Zanzibar ambazo kabla ya hati ya makubaliano ya muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.
albano.midelo@gmail.com



No comments:

Post a Comment