![]() |
| Viongozi wa mtandao wa RUNEA wakiteta jambo |
Na Albano Midelo
ASASI za kiraia
mkoani Ruvuma zimependekeza eneo la wazee katika rasimu ya katiba ya
jamhuri ya muungano wa Tanzania liwe
wazi kwa kuhakikisha kuwa wazee wote nchini wanalipwa pensheni itakayowawezesha
kuishi.
Wawakilishi zaidi ya
50 kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma wametoa mapendekezo hayo kwenye mkutano wa jukwaa la kujadili rasimu
ya katiba mpya ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ulioandaliwa na mtandao wa mazingira mkoa wa Ruvuma
(RUNEA) kwa ufadhili wa shirika la The Foundation For Civil Society .
Aidan Challe
amependekeza rasimu ya katiba iweke wazi katika katiba kifungu ambacho kinasema bayana kuwa
wazee watalipwa pensheni ya asilimia 75 ya mshahara wa kima cha chini
serikalini na kufutwa kifungu ambacho
kimewekwa katika rasmu ya katiba kinachosema msaada kwa wazee huku kifungu
kikiwa hakionyeshi wazi wazee watapata msaada toka kwa nani na kiasi gani.
Challe alisisitiza
kuwa kifungu cha wazee kulipwa pensheni kikiwa wazi katika katiba mpya itakuwa
rahisi wazee kwenda kudai endapo serikali itashindwa kulipwa na kwamba kufungu
kilichowekwa kwenye rasmu ya katiba hivi sasa kimezungumzwa kwa ujumla bila
kuanisha wazi wazee wanastahili haki zipi na nani anawajibika kwa wazee.

Grasias Kipara
akichangia kifungu cha wazee katika rasmu alisema sera na sheria zilizopo
zinawanyima haki wazee wa Tanzania ambapo katika rasmu mpya ya katiba ameshauri
kila mzee wa Tanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 60 bila kujali alikuwa ameajiriwa
serikali au mkulima alipwe pensheni itakayomwezesha kumudu maisha hadi mwisho
wa maisha yake hapa ulimwenguni.
‘‘Sera ya wazee
imetaka wazi kuwa wazee wanatakiwa kupata matibabu bure,lakini wote ni
mashahidi ni wazee wangapi wanapata matibabu bure,hakuna hata mmoja tunaomba
katika rasimu hii mpya kifungu kiwekwe na kutamka bayana atakayehusika na haki
zote za wazee ili atakayekiuka atambue kuwa anafanya makosa kikatiba’’,alisema
Kipara.
Ally Jaibu
amependekeza katika rasimu ya katiba mpya kiongezwe kifungu ambacho kitaonyesha
wazi kuwa watu wote ambao wanawadharau wazee waweze kuadhibiwa kisheria tofauti
na hivi sasa wazee katika jamii wanaonekana ni balaa.
Jaibu pia
amependekeza katika rasimu ya katiba wazee wawe washauri wakuu katika taasisi
mbalimbali za umma na binafsi na kwamba kwa kazi hiyo serikali iweke bayana
posho ambazo watalipwa wazee hao.
Judith Erasto amesema
katika kipengere cha haki za binadamu wazee wameonekana wanakosa hali zao za
msingi,licha ya kwamba rasimu ya katiba ya jamhuri ya muungano ibara ya 47
kutamka wazi kuhusu haki za wazee zikiwemo kushiriki katika shughuli za
kijamii,kuendeleza maisha yao,kutambuliwa utu wao,kulelewa na kupata misaada
kutoka katika familia zao,jamii na mamlaka ya nchi.
Alisema wazee wa
Tanzania wanaishi katika mazingira magumu kutokana na serikali kuziweka haki
zao kisiasa zaidi kwa kuwa hakuna mtu anayewajibika moja kwa moja kwa wazee
ndiyo maana hata wakiugua licha ya kwamba serikali kupitia sera ya wazee
ilisema watapatiwa matibabu bure lakini katika hali halisi wazee wa Tanzania
hawatibiwi bure.
‘‘Napendekeza katika
rasimu hii ihakikishe kwa kutaja bayana haki zote wanazotakiwa kupata wazee na
mtu anayewajibika kuhakikisha haki hizo wanazipata,pia hatua za kuchukuliwa kwa
yeyote ambaye atashindwa kutimiza wajibu wake katika haki za wazee
kikatiba’’,alisisitiza.
Vinsent Kapinga
kuhusu haki za wazee kwenye rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ameshauri katiba mpya kujenga mfumo sawa
kwa wazee wote kuhakikisha wanapata haki zote za msingi kama ilivyo kwa wazee wa
nchi za Afrika ya kusini ambayo imeamua kila mwezi wazee kuwalipa pensheni ili
waweze kuendelea kuishi.
‘‘Katika katiba mpya
serikali lazima iweke kifungu ambacho kinasema imekusudia kuwatunza wazee kwa
kiwango Fulani cha pensheni ,wazee wa Tanzania wanahangaika na kugeuka ombaomba
kila mtu Mungu akimpa maisha kuanzia miaka 60 anaweza kuwa mzee hivyo ni vema
katiba ijayo itilie mkazo haki za wazee’’,alisema.
Amesisitiza kuwa
katika katiba kuwe na kifungu ambacho kinatamka wazi kuwa wazee wenye umri wa
kuanzia miaka 60 wana haki ya kupata matibabu bure badala ya kusema wazee wasaidiwe huku mtu
anayewajibika moja kwa moja wazee hao akiwa hafahamiki na kuleta matatizo makubwa kwa wazee.
Kuhusu kipengere cha
wazee kupata msaada katika familia zao kama kilivyowekwa kwenye rasimu ya
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nathaniel Lugongo ameshauri kipengele
hicho kuondolewa badala yake ieleze kuwa
mtoto ana haki ya kisheria kumtunza mzazi wake na sio msaada kutokana na ukweli
kuwa mzazi ndiye aliyemlea,kumtunza na kumsomesha mtoto huyo.
Takwimu zinaonesha
kuwa katika manispaa ya Songea inakadiriwa
kuwa na wazee wenye umri wa miaka zaidi
ya 60 kufikia zaidi ya 180,000, hapa nchini inakadiriwa wazee wa zaidi ya miaka
60 wapo zaidi ya milioni 1.4 na ifikapo
mwaka 2050 idadi ya wazee wa Tanzania inatarajia kufikia milioni 8.3 sawa na
asilimia 10 ya watanzania wote.
Kulingana na taarifa
za umoja wa Mataifa za mwaka 1999 zinaonyesha kuwa mwaka 1950 wazee wenye umri
wa miaka zaidi ya 50 duniani walikuwa 200,mwaka 1975 idadi hiyo iliongezeka na
kufikia wazee 350,mwaka 2005 idadi ya wazee duniani ilifikia milioni 625 na
mwaka 2050 wazee wenye umri wa zaidi ya
miaka 60 katika historia ya binadamu
inatarajia kuongezeka kuzidi idadi ya watoto na vijana wenye umri wa
miaka 24.
Katika bara la Afrika
pekee ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee inatarajia kuongezeka kutoka milioni 38
hadi kufikia milioni 212,ongezeko hilo la wazee ni changamoto kwa serikali
ikiwemo serikali ya Tanzania kuhakikisha
kuwa katika rasimu mpya ijayo inawatendea haki wazee ambao asilimia 75 wanaishi
vijijini katika maisha ya umaskini uliokithiri.
albano.midelo@gmail.com

No comments:
Post a Comment