Wanaidai serikali sh. bilioni sita
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT),
kimetoa mwezi mmoja kwa serikali kulipa malimbikizo yao ya madeni ya walimu
yanayofikia bilioni 33.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam, rais wa chama hicho, Greisoni Mukoba, alisema wamechoka
kupewa ahadi hewa na serikali ndio maana wamefikia hatua hiyo.
‘Tumetoa mwezi huu wa tisa uwe wa
mwisho kuililia serikali, baada ya hapo tutaamua hatua gani tufanye, maana
tumekutana na makatibu wakuu wa wizara zinazowahudumia walimu lakini bado
tunaishia kupewa ahadi hewa,” alisema Mukoba.
Mukoba aliongeza kuwa Agosti 14, mwaka
huu, walikutana na makatibu wakuu wanaowahudumia walimu pamoja na Katibu Mkuu
ofisi ya Rais Menejimenti ya Umma, wakatakiwa kuwasilisha madai yao yote.
“Tulikutana na makatibu, katika kikao
hicho, tuliwafahamisha kuwa walimu wanaidai serikali zaidi ya sh bilioni 33 na
mwisho wa kikao hicho tulikubaliana CWT iwakilishe madai hayo ndani ya wiki mbili,”
aliongeza Mukoba.
Mukoba alisema wiki mbili zilipofika,
walienda kuonana tena na Katibu Mkuu, ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na kuwasilisha vitabu vyenye madai mbalimbali ya walimu.
“Madai hayo tuliyaambatanisha kwenye
barua Na CWT/004/UTMS/VOL.11/94 na madai hayo sasa yamefikia sh bilioni sita,”
alisema Mukoba.
Mukoba aliishangaa serikali kuanzisha
Mpango wa Matokeo Makubwa sasa “Big Result Now”, huko walimu ambao ndio
watekelezaji wakubwa wa mpango huo, wana maisha magumu kutokana na mishahara
kuwa midogo na kuzidi kwa malikimbizo ya madeni yao.
“Walimu ambao ndiyo watelekezaji wakuu
wa mpango huu japo hawaelewi au hawajapewa semina elekezi, lakini ndio
watekelezaji wakubwa.
Naishangaa serikali kuwadharau walimu
na nakuhakikishia mpango huo hautafanikiwa kama walimu hawapati haki zao,”
alisema Mukoba.
Mukoba aliionya serikali ikamilishe
madai ya walimu ili wafanye kazi kwa moyo tofauti na sasa ambapo wengi wamekata
tamaa.
‘‘Walimu wa nchi hii wamekata tamaa.
Mioyo yao imekufa ganzi kwa sababu serikali imekataa kuwalipa malimbizo yao.
Kwa nini serikali
imeamua kuwatendea jeuri walimu kiasi hiki?” alihoji Mukoba.
CHANZO GAZETI LA
TANZANIA DAIMA

No comments:
Post a Comment