Saturday, September 14, 2013

Vyuo vikuu vya kanisa havina ubaguzi


B aadhi ya wanachuo wa shahada  St.Joseph Songea
 Na Albano Midelo
VYUO vikuu vya kanisa katoliki nchini vinapokea wanafunzi kutoka imani zote na hata wanafunzi wasiokuwa na imani za dini lengo likiwa ni kujenga  umoja wa Taifa na maelewano baina ya watanzania.
Hayo yalisemwa na askofu wa jimbo katoliki la Mbinga mhashamu John Ndimbo  kwa niaba ya Askofu mkuu wa jimbo kuu la Songea katika mahafali ya nne ya chuo kikuu cha mtakatifu Joseph kampasi ya Songea yaliofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho vilivyopo Ruhuwiko mjini hapa.
Mhashamu Ndimbo kwa namna ya pekee ameipongeza serikali kutokana na kutoa ushirikiano wa kutosha na kutambua mchango wa madhehebu ya dini  katika huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu.

“Hatuna budi kuishukuru serikali pale inapotoa sera na miongozo mizuri inayowezesha mashirika ya dini kushiriki kuilea jamii hususani huduma za elimu,tunayofuraha kuwepo kwa sera ya elimu ya  kanisa katoliki ya Tanzania ya mwaka  2005 na 2008 inayotaka vyuo  vikuu vyote vya kanisa kupokea wanafunzi kutoka imani zote na hata wale wasiokuwa na imani za dini lengo ni kujenga maelewano baina na watanzania wote’’,alisisitiza.
Katika mahafali hayo ambayo mgeni rasmi alikuwa waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi Dk.Shukuru Kawambwa jumla ya wanachuo 97 wametunukiwa vyeti vya kuhitimu stashahada na shahada katika chuo kikuu cha teknolijia ya habari cha mtakatifu Joseph kampasi ya Songea kinachomilikiwa na watawa wa katoliki wa Daughters Of Mary Immaculate (DMI).
Akizungumza katika mahafali ya nne ya  chuo kikuu hicho,mkuu wa chuo kikuu cha mtakatifu Joseph cha Tanzania  padre Dk. Arul Raj alisema kati ya wahitimu hao wanachuo 58 ni wenye shahada(degree) ya kompyuta ya sayansi  na wanachuo 39 wenye stashahada (diploma) ya sayansi ya kompyuta.
‘‘Leo tunapofanya mahafali ya nne ni muda muafaka wa kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kukiwezesha chuo chetu kupata mafanikio makubwa kitaaluma kwa kuzalisha wataalamu wengi katika fani ya teknolojia ya habari na uhandisi,pia kutokana na kupanua matawi ya chuo chetu ambapo hivi sasa katika Tanzania kuna matawi matano katika mikoa ya Ruvuma,Njombe,Dar es salaam na Arusha’’,alisema.
Ameyataja malengo ya baadaye ya chuo kikuu hicho kuwa ni kufungua tawi katika mkoa wa Tanga, katika kuhakikisha mpango huo unatekelezwa chuo kimetenga bajeti ya shilingi bilioni moja na tayari kimenunua ekari saba katika jiji la Tanga.
Aliongeza kuwa hivi sasa chuo kikuu cha mtakatifu Joseph cha Tanzania kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1350 wanaosoma katika fani za uhandisi na teknolojia ya habari na kwamba chuo hicho kutokana na kutoa elimu bora kimekuwa ni chagua la watanzania wengi ambao wanafanikiwa kutimiza ndoto zao.
Kwa upande wake makamu mkuu wa chuo kikuu cha mtakatifu Joseph Songea Sr.Julian Rani alisema kuwa chuo hicho hivi sasa kinajulikana ndani na nje ya nchi kutokana na kuzalisha wataalamu bora katika uandisi na teknolojia ya habari na kwamba kutokana na kuungwa mkono na serikali baada ya muda mfupi chuo kikuu hicho kitafahamika ulimwenguni na hivyo kuwa chuo kikuu cha kimataifa.
Alisema chuo kikuu cha mtakatifu Joseph Songea kilianza mwaka 2004 kikiwa na wanachuo wachache ambapo hivi sasa chuo hicho kina idadi kubwa ya wanachuo ambao ni 685 kati yao wanaume ni 558 na wanawake 127 ambao wanasoma stashahada na shahada katika Sayansi ya kompyuta.
Hata hivyo alisema kuanzia mwaka wa masomo uliopita chuo kimeanza kutoa  masomo ya shahada ya Sayansi ya elimu ambapo tayari kuna wanachuo 205 wanaosoma kozi hiyo na kwamba katika chuo hicho kampasi ya Songea tangu mwaka 2010  kinatoa masomo ya shahada ya kilimo  ambapo tayari kuna wanachuo 173 kati yao wanaume ni 119 na wanawake 54.
Dk.Txa Ananth ambaye ni Rais wa baraza la vyuo vikuu vya mtakatifu Joseph Afrika vinavyomilikiwa na watawa wa DMI  akitoa ripoti ya vyuo hivyo kwenye mahafali hayo alisema jamii ya watawa wa DMI ilianzishwa nchini India mwaka 1984 kwa lengo la kuhudumia masikini ambapo hivi sasa DMI inahudumia wanawake  zaidi ya 500,000,wanafunzi wahandisi 21,000 na watoto 35,000.
“Chuo kikuu cha mtakatifu Joseph kinamilikiwa na kanisa katoliki chini ya watawa wa DMI kinafanya kazi zake zote kwa kumtanguliza mwenyezi Mungu mbele, hata hivyo tunatoa huduma kwa watu wote bila ubaguzi wa dini,kabila wala rangi’’,alisisitiza.
Kwa mujibu wa Rais huyo wa watawa wa DMI Afrika,shirika hilo limeenea katika nchi sita za Afrika ambazo alizitaja kuwa ni Tanzania,Zambia,Malawi,Ethiopia,Sieraleone,Sudan kusini na nchi ya Brazil katika Amerika ya kusini ambapo hapa Tanzania DMI ilianza rasmi mwaka 2003.
Katika hatua nyingine serikali mkoani Ruvuma imekubali ombi la kutoa  ekari  zaidi ya 2000 kwa chuo kikuu cha mtakatifu Joseph Songea ili kiweze kujipanua katika sekta ya elimu,maombi hayo pia yameungwa mkono na waziri wa elimu Dk.Shukuru Kawambwa ambaye ameahidi kushughulikia ombi hilo haraka iwezekavyo.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma,mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti alisema serikali imekubali ombi hilo itaanza mara moja mchakato wa kuhakikisha ekari hizo zinapatikana ili kupanua uwezo wa chuo hicho ambacho tayari kina kampasi mbili katika wilaya ya Songea.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi Dk.Shukuru Kawambwa amelipongeza shirika la watawa wa DMI kwa kutoa taaluma bora ya elimu ya juu katika fani za uhandisi na teknolojia ya habari,wataalamu ambao alisema ni muhimu katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia.
Hata hivyo alisema serikali katika kipindi hiki cha miaka mitatu imejikita kuboresha elimu ili kuleta mabadiliko makubwa sasa (Big Results Now) kuanzia elimu ya awali,msingi na sekondari na kwamba hakuna muda wa kusubiri licha ya changamoto zilizopo.
Alisema matokeo makubwa sasa yakifanikiwa katika elimu ya awali,msingi na sekondari  utakuwa mwanzo wa matokeo makubwa katika elimu ya juu kutokana na uhusiano uliopo kati ya elimu ya msingi,sekondari na elimu ya juu.
Kuhusu serikali kuanza kutoka mikopo kwa wanafunzi wanaosoma stashahada,waziri Dk.Kawambwa amesema serikali itaangalia uwezekano wa kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashada ingawa lisisitiza kuwa ni kazi nzito kwa kuwa hata mikopo inayotolewa kwa wanafunzi wa shahada haitoshelezi kwa wote kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma elimu ya juu.
Hata hivyo alisema serikali inajitahidi kila mwaka kuongeza kiwango cha mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambapo mwaka 2005 jumla ya shilingi bilioni 56 zilitengwa katika bajeti kwa ajili ya mikopo na kwamba mwaka huu serikali imetenga shilingi bilioni 326 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu.
“Tangu serikali imeanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu zimetolewa jumla ya trilioni moja  na bilioni mia nne na hamsini,pesa zilizorudishwa kutoka kwa wanachuo ni bilioni 35 tu,wengi waliochukua mikopo wameingia mitini licha ya kupata kazi nzuri, natoa wito kwa wanachuo waliopata mikopo waanze kuirejesha ili wengine waweze kukopeshwa’’,alisisitiza.
Alibainisha kuwa idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu inaongezeka kwa kasi kubwa ukilinganisha na idadi ya wanafunzi 13 ndiyo waliojiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam mwaka 1961 na kwamba idadi imekuwa inaongezeka ambapo takwimu za mwaka 2005 zinaonyesha kuwa wanafunzi waliojiunga na vyuo vikuu ilikuwa ni 42,000 na mwaka huu idadi ya wanachuo katika vyuo vikuu na vyuo imefika 170,000.




No comments:

Post a Comment