Na
Albano Midelo
HIFADHI ya Taifa ya
Serengeti inayopita katika mikoa ya Arusha,Mwanza,Mara na Shinyanga ni eneo
pekee duniani lenye kundi kubwa la wanyama wanaohama katika mfumo mzima wa
mlishano.
Inasemekena neno
Serengeti linatokana na neno la kimasai la sirenget lenye maana ya uwanda mpana wa nyasi fupi,malisho mengi na
maji ya kutosha pengine ndiyo maana hifadhi hiyo inapewa majina mengi kama vile
lulu,bustani ya Afrika na Edeni ya Afrika kutokana na utajiri wa maliasili
uliopo ndani ya hifadhi hii.hifadhi ya Taifa ya
Serengeti yenye ukubwa wa kilometa za
mraba 14,763 ilianzishwa mwaka 1951, ni Hifadhi ya Taifa ya pili kwa ukubwa
nchini ikitanguliwa na hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye ukubwa wa kilometa za
mraba 20,226.
Umaarufu wa hifadhi
ya Taifa ya Serengeti unatokana na kuwa
na misururu mirefu ya nyumbu wanaohama kwa makundi na kuvuka hata mpaka wa Tanzania hadi hifadhi
ya wanyama pori ya Maasai Mara nchini Kenya ambapo takwimu za TANAPA
zinaonyesha kuwa kila mwaka zaidi ya nyumbu milioni moja,pundamilia 200,000,
swala tomi zaidi ya 300,000 na pofu 12,000 huunga misafara ya kutafuta malisho
na maji.
Mhifadhi John Makunga
anasema Kila mwaka katikati ya mwezi Julai tukio lisilokuwa na kawaida na lenye
mvuto wa kipekee hutokea katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kundi kubwa
la nyumbu wakikimbia kutoka upande wa
kusini mwa hifadhi hiyo na inapofika mwezi Mei wanyama hao huanza kukumbwa na
ukame hivyo kuondoka kuelekea kaskazini mwa hifadhi kwa kufuata malisho mazuri.
“Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti huchukuliwa kama moja ya maajabu ya dunia kutokana na tendo la
uhamaji wa nyumbu kutoka kusini hadi kaskazini na kurudi, tendo ambalo
linafanyika mara moja tu kwa mwaka tendo hilo linaifanya hifadhi hii kuwa Eden
ya Afrika na kupendwa kutembelewa na watu wengi ulimwenguni kote’’,alisema.
Licha ya nyumbu
wanyama wengine maarufu walao nyama katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni
chui na simba ambapo utafiti umebaini kuwa ukubwa wa hifadhi hii umesaidia
kudumisha uhai wa wanyama waliokuwa katika hatari ya kutoweka kama vile faru
weusi na duma.
![]() |
| Nyumbu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakelekea Kenya |
Wanasayansi wanaeleza kuwa wanyama aina nyumbu ambao ni
wengi katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti wameumbwa na vijinasaba ambavyo
huwafanya wahame katika mfumo mzima wa mlishano wa Serengeti kwa kufuata nyasi
fupi za Seronera kwenda kusini katika ukanda wa miti michache na nyasi ndani ya
hifadhi ya Serengeti maeneo ambayo ndiyo mazalio ya nyumbu.
Mhifadhi Daniel Gumbo
anasema maeneo hayo yana asili ya udongo wa volkano uliotokana na milipuko iliyotokea katika mlima mkubwa wa
Ngorongoro miaka mingi iliyopita na kwamba asili ya udongo huo huwezesha
wanyama aina ya nyumbu kutoa maziwa kwa wingi kwa ajili ya kunyonyesha ndama wa
nyumbu na kuwawezesha kukua kwa muda mfupi.
Mhifadhi huyo
anabainisha kuwa mara baada ya nyumbu kuzaliana,katika maeneo ya tambarare ya
Seronera huanza safari kuelekea hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande wa
magharibi na kuvuka mpaka kuingia hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya na baada
ya muda mfupi wanarudi Tanzania kupitia Loliondo pamoja na Ngorongoro na
kukamilisha mzunguko mzima.
Tafiti zinaonyesha
kuwa katika hifadhi ya Taifa ya
Serengeti kuna idadi ya nyumbu inayokadiriwa kuwa milioni moja na nusu ambao
hutembea eneo la kilometa za mraba 40,000 katika mfumo mzima wa mlishano wa
Serengeti ambapo nyumbu na wafuasi wao
wakiwemo pundamilia,swalatomi na pofu hukumbwa na vifo kutokana na kuchoka njiani
kwa sababu ya safari ndefu,umri mkubwa na magonjwa.
Kutokana na sababu
hizo wanyama ambao ni maadui wakubwa wa nyumbu ambao ni simba,fisi na mbweha
wanakuwa washiriki katika msafara huo wa nyumbu wanaohama katika mfumo wa
mlishano hivyo kufaidi mizoga ya wanyama
hao au kuwawinda wanyama wagonjwa na waliochoka.
Watafiti wa wanyama
hao wanautaja muda mzuri ambao wanyama hao wanasafiri ni usiku kutokana na muda
huo kuwa na hali ya hewa isiyokuwa na joto ambayo huwawezesha kukimbia kwa muda
mrefu na kwamba wanyama hao mara nyingi hukimbia katika mstari mmoja na
wanapofika kwenye malisho au mapumziko wanatawanyika.
Wanasayansi
waliowafanyia tafiti nyumbu wanadai kuwa inapotokea nyumbu wanazaa wakati mvua
zinanyesha huweza kuchelewa tendo la
kuzaa kwa wiki mbili hadi tatu na mvua zinapowahi nyumbu huweza kuzaa mapema
wiki mbili au tatu kabla ya muda wake .
Kwa mujibu wa
wataalamu hao wa wanyama, baada ya kuzaliwa ndama wa nyumbu huweza kusimama na
kukimbia na mama yake baada ya dakika chache na kwamba baada ya siku moja tu
ndama wa nyumbu huweza kukimbia na kundi zima la nyumbu na baada ya siku kumi
huweza kula nyasi huku akiendelea kunyonya kwa miezi sita lakini anaendelea
kubaki na mama yake hadi ndama mwingine atakapozaliwa.
Watalii wanaotembelea
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kutokana
na makundi makubwa ya nyumbu wameifanya hifadhi hiyo kuwa maarufu Afrika
mashariki na ulimwenguni kote hali iliyosababisha shirika la Umoja wa Mataifa
la Elimu na Sayansi UNESCO kuitangaza
Serengeti kuwa eneo la urithi wa Dunia kwa kuwa ndiyo eneo pekee ulimwenguni
lililosalia kundi kubwa la wanyama wahamao.
![]() |
| Nyumbu wa hifadhi ya Taifa Serengeti |
Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti inatambulika kama Edeni ya Afrika kwa kuwa ni moja ya maajabu ya
dunia hivyo kuvutia hisia za watu wengi kupenda kutembelea hifadhi hii ambapo
tafiti mbalimbali za kisanyasi kuhusiana na hifadhi hii zimefanyika na makala
nyingi za kisayansi zimeandikwa.
Mwanasayansi kutoka nchini Ujerumani anayefahamika kwa jina
la Gyzmeck Gyzmeck alifanya utafiti wa kisayansi katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti kisha kuandika kitabu
kilichoitwa ‘‘Serengeti shall never die”
ikiwa na maana Serengeti haitakufa .
Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti ipo umbali wa kilometa 335 kutoka Arusha ikiambaa kaskazini katika
mpaka na nchi ya Kenya,kwa upande wa magharibi inapakana na na ziwa
Viktoria,hifadhi hii inafikika kwa kukodi ndege kutokea jijini Dar es
salaam,Mwanza,Kilimanjaro na Arusha pia kwa barabara kutokea Arusha,Musoma na
Mwanza,wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ili kuona uhamaji wa nyumbu ni
kuanzia mwezi Desemba hadi Julai.
Mkurugenzi
wa Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA Allan Kijazi anasema utalii katika hifadhi 16 za Taifa ni moja ya
vyanzo vikuu vya fedha za kigeni katika Taifa na kwamba juhudi za kuzitangaza
hifadhi kimataifa zimesababisha idadi ya watalii kutoka nje ya nchi kuendelea
kuongezeka na kwamba TANAPA inafanya juhudi za kuwawezesha watanzania kufanya utalii
wa ndani badala ya kutegemea wageni .
Takwimu
zinaonyesha kuwa TANAPA imeingiza mapato ya zaidi ya sh. bilioni 549.8 hadi kufikia kipindi cha mwaka wa fedha wa
2011/2012 ikiwa ni mapato yaliyotokana na watalii waliotembelea Hifadhi za
Taifa zilizoko chini ya shirika hilo na kwamba katika kipindi hicho jumla ya
watalii milioni 5.730,181 walitembelea hifadhi hizo za Taifa.
Balozi
Khamis Kagasheki ni waziri wa maliasili na utalii, anasema sekta ya utalii hapa
nchini ni ya pili kwa ukubwa katika kuchangia pato la Taifa ambayo inachangia
asilimia 17 na kwamba Kutokana na mapato
makubwa ya sekta ya utalii waziri Kagasheki anasisitiza kuwa Serikali
imekusudia kuongeza mchango wa utalii katika pato la Taifa.
Mkakati mmoja wapo unaotumika kuboresha sekta
ya utalii kama ulivyoainishwa katika Sera ya Utalii ya mwaka 1999 ni kupanua wigo wa utaliii ikiwa ni pamoja na
kufungua maeneo mapya ya utalii na kuendeleza mazao mapya ya utalii hivyo
kuongeza muda wa mtalii kukaa nchini na kufanya matumizi zaidi hatimaye Taifa
kupata mapato zaidi.
Sekta
ya utalii ni muhimu sio kwa Tanzania pekee bali pia duniani kote kutokana na takwimu za kimataifa
kuonyesha kuwa Mapato yatokanayo na utalii duniani yalifikia dola za Marekani
milioni 919 mwaka 2010 ukilinganisha na mwaka 2009 ambapo mapato hayo yalikuwa dola za Marekani milioni 851 sawa na ongezeko la asilimia 4.7
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129



No comments:
Post a Comment