Na Albano Midelo
TANGU mwaka 1961 hadi 1970 bonde la
Songwe wilayani Chunya mkoani Mbeya lilikuwa ni ardhi oevu,yenye uoto wa
kijani na msitu mnene wenye miti mbalimbali ya asili.
![]() |
| Shughuli za kibinadamu zinavyoharibu mazingira na kuuwa ardhi |
Wakati huo wakulima
waliweza kuzalisha mazao ya chakula kwa wingi kutokana na bonde kuwa na ardhi
oevu yenye maji yaliokuwa yanatiririka kutoka mto Songwe ambao unaanzia milima
ya Umalila Mbeya na kumwaga maji yake ziwa Rukwa .
Bonde la Songwe
ambalo linaundwa na kata za Totowe, Galula,Namkukwe,Kanga
na Mbuyuni wakati huo lilikuwa linavutia maisha ya viumbehai wakiwemo
binadamu, wanyamapori na ndege wa aina mbalimbali.
Katika bonde la Songwe wakulima waliweza kulima mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, alizeti, ufuta, mtama,viazi vitamu na mpunga.
Katika bonde la Songwe wakulima waliweza kulima mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, alizeti, ufuta, mtama,viazi vitamu na mpunga.
Mtu ambaye alifika
kwenye bonde la Songwe miaka ya 1970 akitembelea leo kwenye bonde hilo hawezi
kuamini kwa kile ambacho atakiona kutokana na mabadiliko makubwa ya
kimazingira ambayo yamejitokeza,hivi sasa bonde hilo linakabiliwa na njaa kila mwaka kutokana
na ukame unaotokana na bonde kukosa mvua za uhakika.
Siku za nyuma hayati Baba wa Taifa mwl.Julius
Nyerere alitahadharisha kuwa ardhi ndiyo msingi wa uhai wetu,ardhi ikiwa na afya
tutakuwa na afya,ardhi ikiugua tutaugua na ardhi ikifa viumbe wote
tunafutika katika uso wa dunia.
Maneno hayo ya Baba wa Taifa yameanza
kutimia katika maeneo mbalimbali nchini likiwemo bonde la Songwe ambapo hivi sasa katika bonde
hilo miti imetoweka,ardhi imebaki uchi,miti karibu yote iliyokuwa kivutio
katika bonde la Songwe haipo tena,bonde limejaa makorongo makubwa ambayo
yanatokana na mmomonyoko wa ardhi,vumbi zito na vimbunga vya mara kwa
mara limekuwa ni jambo la kawaida katika bonde hili.
![]() |
| Ufyekaji ovyo misitu unamaliza miti na kuharibu mazingira |
Unapofika kwenye bonde hili kuanzia
mwezi wa Aprili hadi Novemba utaona upepo wenye vumbi zito ambao unaweza
kudhani mvua inataka kunyesha,vumbi hilo huwa zito kiasi kwamba huwezi kumuona
mtu aliye mbele yako.Hali hii inawafanya wakazi wa Bonde hilo kujifungia ndani
ya nyumba zao kuepukana na vumbi hilo.
Athari hizo za kimazingira
zinachangiwa na idadi kubwa ya mifugo ambayo inaendelea kuongezeka
kwa kasi kubwa kwenye bonde la Songwe huku wafugaji hao wahamiaji kutoka kanda
ya ziwa wakifanya uharibifu wa mazingira kwa kufyeka miti ovyo kwa lengo la
kujipatia kuni,mkaa na mashamba.
Afisa mifugo,kilimo na ushirika
katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya Adamu Mbale anasema idadi ya
ng,ombe katika bonde zima kati ya mwaka 1961 hadi 1970 ilikuwa ni 800 tu hali
iliyosababisha mazingira katika bonde hilo kuwa ya kuvutia.
Kwa mujibu wa Mbale idadi ya
ng’ombe kwenye bonde hilo iliongezeka kwa kasi na kuathiri mazingira
katika kipindi cha kuanzia mwaka 1981 hadi 1990 ng’ombe walifikia
173,681,mwaka 2000 ng’ombe walifikia 186,800 na hadi kufikia mwaka 2010 idadi
ya ng’ombe ilifikia 286,800.
Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus
Kinawiro amekiri kuwa bonde la Songwe na wilaya ya Chunya kwa ujumla wake
inapita katika kipindi kigumu sana cha uharibifu wa mazingira ambacho
hakijawahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwa wilaya hiyo.
“Kimsingi hali ya uharibifu wa
mazingira katika wilaya yetu ni mbaya sana na kama hatutachukua hatua za
haraka hali inaweza kuwa mbaya zaidi
miaka michache ijayo,ni jukumu letu sisi viongozi wa serikali kushirikiana na
viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji,kijiji,kata na tarafa kuokoa hali hii
inayotishia ustawi wa maisha ya watu endapo kutatokea jangwa kwa kuwa dalili
zake hasa katika bonde la Songwe zimeanza kujitokeza’’,alisema.
Kinawiro alisema misitu mingi ya asili
na iliyotengwa kwa ajili ya hifadhi
katika wilaya ya Chunya imevamiwa licha ya serikali kupiga marufuku kuendesha
shughuli zote za kibinadamu kama vile kulima na kufuga na kwamba ndani ya
misitu hiyo kuna wafugaji wengi ambao wanakata miti ovyo bila kuangalia athari
za kimazingira.
“Kwa mtu ambaye unapenda mazingira
ukifika katika misitu ya hifadhi ya wilaya ya Chunya unaweza kulia kwani misitu
imebakia vibara vitupu,watu wamekata miti ya asili ambayo imekuwa kwa zaidi ya
miaka 100,kibaya zaidi mara baada ya kuikata anaichoma moto inakuwa majivu na
kuacha eneo hilo kuwa kama uwanja wa mpira tena ambao hauna nyasi’’,alisema.
Alisisitiza kuwa bila miti hakuna mvua
ndiyo maana katika bonde la Songwe ambalo karibu miti yote imekatwa linakabiliwa
na ukame ambao unasababisha njaa kila mwaka
hali inayoleta matatizo kwa serikali kila mwaka kupeleka chakula cha
msaada kwa wakazi wa bonde hilo ambao eneo lao ni nusu jangwa.
Alisema mwezi Juni
mwaka huu imefanyika operesheni maalum katika kata ya Totowe bonde la Songwe
kuwaondoa watu waliovamia maeneo ya misitu ya hifadhi na kwamba wanatarajia
kwenda katika maeneo mengine yaliokithiri ambayo aliyataja kuwa ni Gua,Ngwala
na Kapalala ambako wanatarajia kwenda kuendesha operesheni hiyo ili kuhakikisha kuwa misitu ya hifadhi
inabakia kuwa endelevu.
Utafiti umebaini kuwa
Kuna baadhi ya maeneo hapa nchini yakiwemo katika mikoa ya Dodoma,Arusha,Manyara,Shinyanga
na Mbeya wameanza kuonja athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo kuna
wakati fulani wa mwaka kunatokea giza kubwa la upepo wa vumbi zito mfano wa wingu la mvua ambalo linaendelea kuuwa ardhi .
Wanasayansi wanatahadharisha kuwa Dunia hivi
sasa inapita katika tatizo kubwa la kubadilika kwa misimu ya mvua,kuongezeka
kwa joto,ukame,mafuriko,kuongezeka kwa baridi,kuyeyuka kwa barafu kwenye mlima
Kilimanjaro pamoja na sehemu nyingine kutokana na uharibifu mkubwa wa
mazingira.
Viumbehai wa kuvutia
kama ndege,mimea na wanyama kuna dalili kwamba siku moja wanaweza kufutika
katika uso wa dunia kutokana na uharibifu
mkubwa wa mazingira unaofanywa na binadamu ambao hivi sasa unatishia
mabadiliko ya tabia nchi.
![]() |
| Waziri wa mazingira Dk.Teresia Huvisa akitoa maagizo kukabiliana na Mazingira |
Waziri
wa nchi ofisi ya makamu wa Rais mazingira Dk.Teresia Huvisa hivi karibuni
amewaasa watanzania wote kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira ili
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yaliosababishwa na hewa ukaa angani na
kusisitiza kuwa uharibifu wa mazingira ni janga la duniani ambalo linaviweka
viumbehai njia panda.
“Mimi kama Rais wa
mazingira Afrika ambaye nilichaguliwa mwaka jana na mawaziri wote wa mazingira
barani Afrika nina wajibu wa kutoa tahadhari sio tu kwa watanzania bali Afrika
nzima na ulimwengu kote kwa ujumla,
dunia inaweza kuangamia kama sisi sote hatutafanya juhudi za makusudi
kupambana na mabadiliko ya tabianchi’’,alisisitiza.
Kulingana na waziri huyo,tangu
kuumbwa kwa dunia shughuli mbalimbali za kibinadamu zimesababisha dunia
kuharibika na kuongezeka kwa joto kwa kwa asilimia 0.7 na kusababisha madhara
yote yanayotokea sasa duniani yakiwemo ukame,mafuriko na mabadiliko ya
tabianchi kwa ujumla.
Hata hivyo
wanasayansi wanatahadharisha kuwa iwapo joto duniani litaongezeka hadi kufikia asilimia 1.5 ambalo ni ongezeko
la asilimia 0.8 viumbehai wote waliopo duniani hawataweza kumudu kuishi.
“Mwaka juzi
tulipokuwa nchini Afrika ya kusini
ongezeko la joto duniani lilikuwa 0.7,katika mkutano wa kidunia wa
mawaziri wa mazingira ambao tuliufanya mwaka jana jijini Doha nchini Quatar
kiwango cha joto kilifikia 0.8, mwaka huu tunafanya mkutano mwingine nchini
Poland hatujui joto litafikia kiwango gani linawezekana kufikia 0.9,kupambana
na hali hii inatakiwa kupanda miti ya kutosha na sio vinginevyo’’,alisisitiza
waziri Dk.Huvisa.
Kwa mujibu wa sera ya
Taifa ya misitu ya mwaka 1998, Tanzania ina karibu hekta milioni 33.5 za misitu
ambapo theluthi mbili ya hekta hizo ipo
mashakani kutokana na ukosefu wa usimamizi mzuri hali inayosababisha watu
kuvamia na kuharibu misitu kwa ajili ya kilimo,malisho ya mifugo,moto,uchimbaji
madini,ujenzi na shughuli nyingine.
Licha ya kwamba
hakuna takwimu za kuaminika kuhusu kasi ya kutoweka kwa misitu,inakadiriwa kuwa
hapa nchini ni kati ya hekta 130,000 hadi 500,000 za misitu zinafyekwa kila
mwaka hali inayokatisha tamaa jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi ambayo yanahitaji miti ili kupunguza hewa ukaa .
Mwanadamu ndiyo mtaji
mkubwa katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira hivyo wananchi watambua
kuwa mabadiliko ya tabia ya nchi yameanza kutuathiri inatakiwa kupanda miti
kila mwaka na kuitunza ili kupunguza matatizo haya yanayoiweka dunia njia panda.
albano.midelo@gmail.com



No comments:
Post a Comment