![]() |
| Dawa za kulevya |
Na Albano Midelo
Idadi ya vijana
wanaoingia nchini Afrika ya kusini kutokea Tanzania kinyume cha sheria kwa
lengo ya kutafuta maisha bora imesababisha wengi wao kujiingiza katika biashara
ya dawa za kulevya baada ya kukosa kazi.
Uchunguzi ambao umefanyika
katika mitaa ya jiji la Johannesburg pekee umebaini kuwepo idadi kubwa ya
vijana wa kitanzania ambao wamekuwa wanazurura na wanauza na kutumia dawa za
kulevya na kujihusisha na kazi za ujambazi wa kutumia silaha kwa lengo la
kujipatia kipato.
Balozi wa Tanzania
nchini Afrika ya kusini Radhia Msuya amekiri kuwepo kwa vijana wengi wa
kitanzania ambao wanaingia kinyume cha sheria na kwamba ofisi yake inaingia
gharama kubwa ambapo kila mwezi vijana wazururaji zaidi ya 200 walioingia
kinyume cha sheria wanarudishwa
Tanzania.
Alibainisha kuwa
vijana wengi wanaamini kuwa nchini Afrika ya kusini ni kama peponi kwa kuwa
kuna maisha bora hivyo wengi wanakimbilia kuja kutafuta maisha kwa kutumia njia
ambazo sio halali ikiwemo kufika bila hati za kusafiria.
![]() |
| Radhia Msuya Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya kusini |
‘‘Ni kweli nchini
Afrika ya kusini kuna maisha bora,lakini maisha hayo hayapatikani hivi hivi tu,
kwa kudhani ukifika hapa unachupa pesa kutoka kwenye miti,watu hapa wanachapa
kazi kwa bidii’’,alisisitiza.
Alisema kutokana na
vijana hao kukosa kazi za maana ambazo hazikidhi kipato baadhi ya vijana wamejiigiza katika biashara haramu
ya matumizi ya dawa za kulevya hali ambayo imesababisha wengine kuwa wakabaji.
Peter Masika mkurugenzi
wa kampuni ya utalii ya Monsoon Transfers and tours ni mtanzania ambaye ameishi
nchini Afrika ya kusini kwa miaka 15,anasema anapokuwa anazunguka katika baadhi
ya mitaa Johannesburg na Pretoria amekuwa anakutana na watanzania wengi ambao
wamegeuka ombamba kwa kukosa kazi ya maana.
‘‘Wengi wananifahamu
hivyo wakiona gari langu wamekuwa wanalizunguka na kuomba fedha kwa kuwa nimekuwa
nawasaidia lakini wengi hivi sasa ni
waharifu wanauza na kutumia dawa za kulevya na kujiingiza katika vitendo vya uharifu
’’,alisisitiza.
Maxmillian Bushoke ni
mtangazaji wa idhaa ya Kiswahili ya Channel Afrika ambaye yupo nchini Afrika ya
kusini tangu mwaka 1994 amekiri kuwa jamii ya watu wanaofanya biashara ya dawa
za kulevya imezuka na kuwashirikisha vijana wengi wanaotoka Tanzania na Nigeria
.
Kulingana na Bushoke
ambaye pia ni mwanamuziki maarufu wa zamani nchini Tanzania alidai kuwa hata
baadhi ya wamamuziki ambao wanaingia nchini Afrika ya kusini,wanajitumbukiza
katika biashara ya unga baada ya kukutana na vijana wenzao wanaotumia madawa
hayo hivyo kujiletea matatizo makubwa yanayosababisha kufungwa na hata kupoteza
maisha.
Nina mfano hai uliotokea
hivi karibuni kwa mtoto wetu mwanamuziki wa kizazi kipya Mangwea ambaye alifika
hapa Afrika ya kusini alifanya maonyesho kadhaa ya muziki kisha aliamua kwenda
kuwatembelea wenzake ambao ni watumiaji wakubwa wa madawa hayo ambayo aliamua
kubwia na kusababisha kifo chake’’,alidai Bushoke.
Hata hivyo Bushoke
alidai kuwa vijana wa kitanzania wanaotumia madawa ya kulevya nchini Afrika ya
kusini,walianza kutumia madawa hayo tangu walipokuwa Tanzania isipokuwa katika
nchi ya Afrika ya kusini matumizi ya madawa hayo ni makubwa zaidi kuliko
Tanzania.
Bushoke alisema
utafiti walioufanya katika jiji la Johannesburg mwaka huu wamebaini vijana
wanaoongoza kwa matumizi ya madawa ya kulevya ni wale wanaotoka katika nchi ya
Nigeria wakifuatiwa na Tanzania ambao wanatumiwa na matajiri wakubwa katika
biashara hiyo haramu.
Ripoti
kutoka Afrika Kusini zinasema wanawake wawili wamekamatwa katika uwanja wa
ndege wa kimataifa OR. Tambo nchini Afrika Kusini wakitokea Tanzania, wakiwa na
madawa ya kulevya yenye thamani ya Rand million 42.6 kiasi ambacho ni kikubwa
zaidi kuwahi kukamatwa katika mpaka wowote wa nchi hiyo.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na shirika la habari la Africa Kusini SABC,
wanawake hao hivi karibuni waliwasili na ndege kutoka Tanzania, walikutwa na
mabegi 6 makubwa yaliyojaa madawa (crystal meth) yenye thamani ya Rand 42.6
millioni ambayo ni sawa na zaidi ya billioni 6 ya Tanzania.
Takwimu kutoka wizara ya mambo ya ndani za mwaka 2005 pekee zinaonyesha kuwa kiasi
cha dawa za kulevya kilichokamatwa kilikuwa ni kilo 150,000 za bangi, kilo 1206
za mirungi, kilo 10 za heroin,
kilo 78 za bangi iliyosindikwa, gramu 362 za cocaine
na kilo 1.4 za dawa ya hospitali aina ya morphine na kwamba
ukamataji wa dawa hizo uliambatana na kukamatwa kwa watuhumiwa 4,532 ambapo
jumla ya kesi 3,368 zilifunguliwa mahakamani.
Kwa mujibu wa
ripoti ya Mwaka 2006, vyombo vya dola vilikamata kilo 91. 5 za heroin, kilo 4.13 za
cocaine, kilo 37 za morphine, kilo 11 za mirungi na kilo 225,229 za bangi.
Katika
nchi ya China sheria ipo wazi kuwa mtu anapokamatwa na dawa za kulevya
anahukumiwa kifo ambapo takwimu kutoka nchini China zinaonyesha kuwa katika
kipindi cha mwaka mmoja uliopita inadaiwa watanzania 200 walinyongwa katika
nchi hiyo baada ya kukutwa na hatia ya dawa za kulevya.
Wataalamu
wa afya wanasema matumizi ya madawa za kulevya yana madhara mengi kwa watumiaji
kama vile uharibifu wa mfumo wa fahamu ambao husababisha mtu kupata mabadiliko
ya kihisia, kimtizamo na kitabia. Mabadiliko hayo humsababishia mtumiaji tabia
zisizokuwa za kawaida kwa mwanadamu na hata kupungukiwa uwezo wa kufikiri
vizuri.
Kwa
mujibu wa wataalamu mtumiaji wa muda mrefu wa dawa za kulevya husababisha
magonjwa ya akili, ini, mapafu na wakati mwingine hata kifo.Wataalamu
wanasisitiza kuwa ni rahisi kwa
watumiaji wa dawa za kulevya kuambukizwa Ukimwi kutokana na kushirikiana
kujidunga sindano na kufanya ngono zembe.
albano.midelo@gmail.com


No comments:
Post a Comment