Wednesday, August 14, 2013

Ziwa Rukwa kufungwa kwa miezi sita



 Na Albano Midelo
Ziwa Rukwa upande wa wilaya ya Chunya mkoani Mbeya linatarajiwa kila mwaka kufungwa kwa miezi sita kwa lengo la kutoa fursa kwa samaki kuzaliana na kukua

Katibu tawala wa wilaya hiyo akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro alisema serikali imeamua kuchukua hatua hiyo kufuatia kasi ya kutoweka kwa samaki katika ziwa hilo  ambapo hivi sasa wavuvi wanavua samaki wachanga mfano wa dagaa ambao hawafai kwa kitoweo. Ziwa Rukwa tangu uhuru limetoa ajira katika sekta ya uvuvi ambapo wavuvi wameweza kusomesha watoto wao,kujipatia kipato kwa kuuza samaki na kupata kitoweo ambacho kinajenga afya kutokana na samaki wanaopatikana kwenye ziwa hilo.

Kinawiro alisema kutokana na uharibifu wa mazingira katika ziwa Rukwa upande wa wilaya ya chunya umesababisha mazalia muhimu ya samaki ndani ya ziwa hilo kuharibika kutokana na shughuli za kibinadamu zinazotokana na uingizaji wa mifugo mingi pamoja na uvuvi wa kutumia kokoro ambao umesababisha samaki wengi kutoweka na kubakia samaki wachanga pekee.
“Kutokana na kasi ya kutoweka kwa samaki ziwa Rukwa sisi kama serikali ya wilaya ya Chunya tumeamua kuchukua maamuzi magumu ikiwemo kufunga shughuli zote za kibinadamu katika ziwa Rukwa kwa miezi sita kila mwaka ili kutoa nafasi kwa samaki kuzaliana ’’,alisisitiza.
Alibainisha kuwa serikali tayari imeandaa na kukamilisha utaratibu ambao kila baada ya miezi sita shughuli zote za uvuvi katika ziwa hilo zitasimamishwa na miezi sita baadaye wananchi wataruhusiwa kuendelea na  uvuvi katika ziwa hilo na kwamba kinachosubiriwa hivi sasa ni idara ya maliasili na uvuvi kupata pesa kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi kuhusiana na mpango huo wa serikali kulifunga ziwa hilo kila baada ya miezi sita.
Alisema idara hiyo itatoa elimu kwa wananchi kufanya shughuli mbadala ambazo zitawaingizia kipato katika kipindi cha miezi sita ambayo ziwa litakuwa limefungwa ili maisha ya wananchi waliokuwa wanategemea shughuli ya uvuvi pekee yaweze kuendelea.
Uchunguzi ambao ulifanywa na mwandishi wa makala haya mwaka 2011 katika ziwa Rukwa upande wa wilaya ya Chunya katika fukwe saba za kata ya Totowe na kata za Ivuna na Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya ulibaini kutoweka kwa samaki wa aina mbalimbali maarufu katika ziwa hilo.
 Mvuvi Stanley Rwamba(65) mkazi wa kijiji cha Totowe ziwa Rukwa wilayani Chunya  aliwataja  jamii ya Samaki ambao wapo katika hatari ya kutoweka katika ziwa Rukwa  ni ngogo,shibe na kachinga ambao walikuwa wanapatikana kwa wingi wakati wa mvua miaka kumi iliyopita.
Uvuvi  wa kutumia  kokoro unaofanyika katika fukwe za ziwa Rukwa katika kata za Totowe, Ivuna na Kamsamba mkoani Mbeya  umechangia kusababisha samaki katika ziwa hilo kupungua kwa kasi.   

Wavuvi kwenye fukwe hizo wamebainika kutumia nyavu za kokoro kuvulia samaki licha ya kwamba nyavu hizo haziruhusiwi kisheria kwa kuwa zinaharibu  mazalia ya samaki pamoja na kuvua samaki wadogo.

Fukwe ambazo uvuvi wa kutumia kokoro umekithiri katika kata ya Totowe  ni  Handeni, Ihovyo, Mtanda, Kambipotea, Kwaboko, Mchangani na Kisiwani.Mwandishi wa makala haya alishuhudia wavuvi  wanavua bila kuwa na hofu ya kukamatwa na maofisa uvuvi ambao wanadaiwa kuchangia hali hiyo kuendelea kwa kuwa hawaonekani katika sehemu zao za kazi.

Staniley Rwamba mvuvi mkongwe katika ziwa Rukwa anasema wavuvi wameamua kutumia kokoro ambazo haziruhusiwi kisheria   kutokana na samaki wanaoruhisiwa kuvuliwa kisheria katika ziwa hilo kuanza kutoweka.
Hata hivyo wavuvi ambao walikuwa wanavua  katika ziwa hilo kila mahali walionekana kukosa samaki ,ambapo wavuvi wanadai hali hiyo inachangiwa na idadi kubwa ya ng’ombe ambao wametia kambi kwenye fukwe za ziwa Rukwa ambao hula malisho ambayo ni mazalia ya samaki ndani ya ziwa hilo.

Bonifasi Yamlinga ni mvuvi katika fukwe ya Mchangani anasema maelfu ya ng’ombe kila siku wanaingizwa hadi mita 500 ndani ya ziwa Rukwa kula nyasi ambazo ni mazalia ya samaki .

Licha ya mifugo kuharibu mazalia ya samaki katika ziwa Rukwa wataalamu wa mifugo wanabainisha kuwa ng’ombe mmoja ana uwezo wa kunywa maji zaidi ya lita 40 kwa mkupuo ambapo idadi ya zaidi ya ng’ombe 500,000 wanaoingia kunywa maji ziwa Rukwa kwa siku  katika fukwe za ziwa Rukwa wilayani Chunya  wanakunywa zaidi ya lita milioni 20.

 Takwimu zinaonyesha kuwa Halmashauri ya wilaya ya Chunya ilikuwa na mifugo zaidi ya 800,000 hadi kufikia Desemba 2010 mifugo mingi ikiwa  katika bonde la Songwe ambalo lina malisho ya kutosha na maji yanayopatikana kwa urahisi kutoka ziwa Rukwa na mito ya Lupa na Songwe.

Yamlinga anabainisha kuwa licha ya samaki wengi wanaovuliwa ziwa Rukwa upande wa Chunya kuwa ni wale ambao hawaruhusiwi kuvuliwa kisheria, amedai hakuna afisa samaki wa kata anayehoji uhalali wa kuvua samaki hao hali ambayo inasababisha wavuvi kuwa huru na kuendelea kufanya uvuvi haramu katika ziwa Rukwa.

Hata hivyo afisa uvuvi na maliasili wa Halmashauri ya wilaya Momba Agrey Ngalunga baada ya kuona samaki wengi wachanga wanaovuliwa ziwa Rukwa katika kata za Ivuna na Kamsamba alidai   serikali ya wilaya hiyo ilitoa ombi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ili wafunge shughuli za uvuvi kwa miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili kila mwaka  ili samaki waweze kuzaliana maombi ambayo bado hayajakubaliwa.
 Kulingana na Ngalunga  mwaka 2010 kamati ya ulinzi na usalama  wilaya ya Momba kwa kushirikiana na kikosi cha usimamizi wa raslimali uvuvi cha Tunduma waliweza kukamata  nyavu haramu kwenye maduka mjini Tunduma zipatazo 2236  zenye thamani zaidi ya shilingi milioni 137 ambazo ziliteketezwa hadharani kwa moto.

 Wavuvi kutoka fukwe za Kwaboko, Mtanda, Handeni na kisiwani ambao ni Peter Sasawata,Staniley Rwamba na John Sichalwe  wanadai kuwa kutoweka kwa  samaki  kunatokana na kina cha maji kupungua,uvuvi wa kutumia kokoro unaofanywa na baadhi ya wavuvi  katika ziwa hilo pamoja na mifugo mingi inayokula nyasi ambazo ni mazalia ya samaki.

Peter Sasawata mvuvi katika ziwa Rukwa anasema  kuwa kwa  wiki moja hadi mbili wavuvi wamekuwa wakivua si zaidi ya samaki watano   aina  ya kachinga ambapo miaka michache nyuma samaki hao walikuwa wanapatikana kwa wingi,ameshauri  juhudi za watalaamu  na serikali zinahitajika ili  kukabiliana na uharibifu wa mazalia ya samaki ili kuzinusuru aina mbalimbali za samaki.

“Kabla ya uharibifu katika ziwa hili, miaka ya nyuma ziwa hili lilikuwa linavutia, kulikuwa na wanyama kama viboko, mamba lakini hivi sasa wanyama hao wamekimbia, hata samaki wamepungua, unaweza kukaa mwezi mzima bila kula samaki,” alisema Elivathan Silwimba, Ofisa Uvuvi Kata ya Ivuna.

John Sichalwe amewataja samaki wengine ambao hivi sasa wameanza kutoweka kuwa ni magege na kapimoja na kwamba samaki aina ya  kambare bado wanapatikana kwa wingi kwa kuwa samaki hao wanapenda kuishi katika matope ambayo yapo mengi ndani ya ziwa Rukwa ambalo kina chake kimejaa tope na mchanga.

Utafiti uliofanywa kwenye fukwe katika ziwa Rukwa unaonyesha dhahiri serikali imeshindwa kusimamia sekta  ya uvuvi na kusababisha kuendelea kuvuliwa kwa samaki wachanga wanaotokana na tatizo la uvuvi haramu hivyo hatua ya serikali ya wilaya ya Chunya kuamua kuchukua maamuzi magumu ya kulifungia ziwa Rukwa kwa miezi sita pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya uvuvi haramu inafaa kuigwa katika maeneo mengine nchini .
 Sensa ya samaki ambayo ilifanywa mwaka 1999 katika ziwa Rukwa ilibaini kuwa   ziwa hilo linazalisha samaki tani 7000 kwa mwaka wakiwemo aina tatu za kambale ambazo ni kibonde,singa na poroko,aina nyingine ni magege, dagaa, kapimoja na kachinga.Wilaya zinazopitiwa na ziwa Rukwa ni pamoja na Chunya na Momba mkoani Mbeya, Sumbawanga na Nkasi mkoani Rukwa na  Mpanda mkoani Katavi.

 Hata hivyo Sera ya Taifa ya mazingira ya mwaka 1997 kuhusu sekta ya uvuvi kifungu cha 60 inaelekeza wazi kuwa uvuvi utaendelezwa  vema kwa kutumia vifaa vya uvuvi vinavyofaa na njia bora za kuendeleza bidhaa zinazotokana na uvuvi ambapo  njia zinazoharibu mazingira katika uvuvi zinadhibitiwa kwa sheria na kuhakikisha  unafuu wa upatikanaji wa vifaa bora vya uvuvi .





No comments:

Post a Comment