Tuesday, October 8, 2013

Tumbaku inaweza kusababisha jangwa


Zao la tumbaku
 Na Albano Midelo

UZALISHAJI wa tumbaku katika mikoa ambayo zao hilo linalimwa umekuwa hauendi sanjari na ongezeko la upandaji miti kwa ajili ya kuchomea tumbaku hali ambayo inachangia uharibifu mkubwa wa mazingira .
Ofisa kilimo wa wilaya ya Songea Kaswam Maswaga anasema hakuna juhudi za makusudi zinazofanywa na wakulima za kupanda miti kwa ajili ya kupata nishati ya kukaushia tumbaku hivyo ametoa wito kwa wakulima kuhakikisha juhudi za kupanua mashamba mapya ya tumbaku zisilete athari za kukata miti  kwa ajili ya kuchomea tumbaku. 
  Frank Komba ni mwanaharakati wa mazingira katika wilaya ya Namtumbo anasema mashamba ya tumbaku yanasababisha uharibifu mkubwa wa misitu  katika wilaya ya Namtumbo pamoja na mikoa mingine inayolima tumbaku kama Tabora kutokana na zao hilo kuhitaji kuni nyingi kwa ajili ya kuchomea tumbaku.


“Ukataji holela wa misitu ili kuchomea tumbaku umeleta athari kubwa ya mabadiliko ya tabia nchi katika kipindi cha miongo michache mkoani Tabora, na sasa mkoa umekuwa na ukame pamoja na ukataji miti unaofanyika mkoani Ruvuma bado mazingira yake ni nafuu tuchukue hatua’’,anasisitiza Komba.

Hata hivyo Komba anadai kuwa jitihada za kushawishi wakulima kuacha kulima tumbaku na kuanza kuzalisha mazao mbadala zimekuwa ni ngumu kwa kuwa wakulima wanaamini zao hilo lina faida kubwa ukilinganisha na mazao mengine ya biashara.

“Ukataji miti ovyo unaoendelea kufanyika kila mwaka karibu wilaya nzima ya Namtumbo, umechangia sana uharibifu wa vyanzo vya maji wilayani Namtumbo ,huku kiwango cha mvua kikiendelea kupungua mwaka hadi mwaka’’,alisema John Nilahi mkazi wa Namtumbo.

 Amosi Luambano ni mkulima mdogo wa tumbaku katika kijiji cha Mbimbi wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma amekuwa akilima tumbaku tangu miaka ya 1980 ambapo Kwa miaka kadhaa amekuwa akishuhudia msitu uliokuwa umezunguka katika kijiji chake ukitoweka huku ardhi ikibakia uchi kwa kukosa miti.

Zao la tumbaku linateketeza maelfu ya tani za kuni kila mwaka zinazotumika kwa ajili ya kukaushia tumbaku kwa mfano inakadiriwa katika mkoa wa Tabora kila mwaka kuni zinazotumika ni zaidi ya meta za ujazo 124,389 za miti hukatwa.

Utafiti uliofanywa kwa kuwahoji baadhi ya wanavijiji   wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, unaonyesha kwamba wakulima wengi hawajui madhara ya zao la tumbaku katika mazingira licha ya kwamba athari zinazotokana na ukataji miti ovyo kwa ajili ya kukaushia tumbaku zimeanza kujitokeza katika vijiji vingi.

Hata hivyo utafiti  uliochapishwa na Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine ambao ulifanyika mkoani Tabora Machi 2012, unaonyesha kuwa Tanzania inapoteza zaidi ya ekari 61,000 za misitu kila mwaka kutokana na zao la tumbaku hali ambayo inaliweka zao hilo mashakani kwa kuwa linaweza kuleta jangwa.

Utafiti huo unasema zao la tumbaku lina mahitaji makubwa ya kuni yanayosababisha miti mbalimbali ya asili  kufyekwa hususani  miyombo. Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 75 ya wakazi wa wilaya za Tabora ni wakulima wa tumbaku, wanalima wastani wa ekari 1.3 za tumbaku kwa mkulima kila msimu, zinazohitaji meta za ujazo 23 za kuni kuchoma majani ya tumbaku.

Mtafiti Mkuu katika utafiti huo, Mwita Mangora, anasema masalia ya misitu mkoani Tabora yaliopo sasa hayana uwezo wa kukidhi matumizi makubwa ya kuni za kuchomea  majani ya tumbaku yanayoongezeka kila mwaka.
Tumbaku hukaushwa kwa kutumia nishati ya kuni, hali ambayo husababisha ukataji mkubwa wa miti kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo, hivyo kuchangia kutoweka kwa misitu ambayo ni vyanzo vikuu vya maji kwa ajili ya binadamu na viumbe hai wengine.

Pamoja na kujulikana kwa uwazi kabisa juu ya madhara ya matumizi ya tumbaku kwa kiwango hicho, bado serikali na jamii kwa ujumla wake imeendelea kuchukulia tumbaku kama moja ya zao muhimu ya kiuchumi katika nchi yetu.

Kulingana na taarifa za benki kuu ya Tanzania(BOT), mchango wa zao la tumbaku kwenye uchumi wa taifa ni mkubwa, kutokana na zao hilo kila mwaka katika mauzo ya tumbaku kuchangia zaidi ya dola za kimarekani milioni 150.
Wakulima wakubwa kwa wadogo wanalima tumbaku, serikali nyingi duniani ikiwamo ya Tanzania zinapata kodi kubwa kutoka kwenye mazao ya tumbaku kama sigara na nyinginezo, hivyo inakuwa vigumu kwa bajeti ya serikali Kupangwa bila tumbaku kuguswa kama chanzo cha mapato.
Sera na mikakati mbalimbali ya kilimo imekuwa ikitazama tumbaku kama mkombozi kwa wakulima na serikali kwa ujumla. Sigara ni biashara ya makampuni makubwa ya kimataifa yakiwa yametawanya mitandao yao katika mataifa mbalimbali ulimwenguni,ikiwemo hapa nchini.
Licha ya kwamba biashara ya tumbaku inaingiza fedha nyingi, ikitazamwa kwa darubini kali, faida yake haina maana sana kwani serikali kwa kuwa inajikuta inaingia katika athari za kiafya kwa wananchi na uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na ukataji wa miti zinazotumika kukaushia tumbaku.
Uchunguzi umebaini kuwa madhara ya tumbaku ni makubwa zaidi kuliko faida, kwani wakati sasa dunia inalia kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, na juhudi kubwa zikielekezwa katika shughuli za uzalishaji mali na utunzaji bora wa mazingira, kilimo cha tumbaku kinabakia kuwa moja ya shughuli yenye madhara zaidi kwa uchumi  na kimazingira.
Maeneo yanayolima zao la tumbaku hapa nchini ikiwemo mkoa wa Morogoro,Tabora,Chunya mkoani Mbeya na Namtumbo mkoani Ruvuma hali ya mazingira ni mbaya kwa kuwa wakulima wanafyeka misitu ya asili ili kupata kuni za kuchomea majani ya tumbaku na kuacha maeneo hayo kuwa wazi na kukaribisha jangwa jambo ambalo ni hatari.
Kutokana na madhara makubwa ambayo yanaletwa na zao la tumbaku kimazingira na kiafya ni vema sasa jamii katika maeneo ambayo yanazalisha tumbaku ikaanza kujipanga kutafuta mbinu endelevu za kuachana na shughuli ya kilimo cha tumbaku na kuanza kuzalisha mazao mbadala.







                

 






No comments:

Post a Comment