![]() |
| Ndege aina ya Tandawalamachaka katika hifadhi ya Taifa Kitulo |
Na Albano Midelo
HIFADHI ya Taifa Kitulo ndilo eneo
pekee Tanzania lenye ndege aina ya tandawala machaka(Denhams Bustard) wenye
uwezo wa kuruka toka bara moja hadi jingine, wameweka makazi yao.
Hifadhi ya
Taifa Kitulo inayopita katika mikoa ya Mbeya na Njombe ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa mwaka
2005 ikijumuisha sehemu ya eneo la shamba la mifugo,msitu wa Livingstone na bonde la Numbi.
Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba
442 ndani ya mwinuko wa kati ya mita 2100 hadi 3000,awali ilijulikana kama
Elton Plateau baada ya Mvumbuzi Fredirick Elton kupita eneo hili
mnamo mwaka 1870. Mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo(FAO) lilichukua eneo
hili kwa ajili ya ukulima wa ngano na ufugaji wa kondoo.
Kutokana na umuhimu wa eneo hili wadau
mbalimbali wa mazingira walipendekeza eneo hili litangazwe kuwa hifadhi ya Taifa
ili kulinda umaridadi wa maua,ndege na mimea adimu inayopatikana ndani ya eneo
hili.
Dk.Ezekiel Dembe kaimu mkurugenzi wa
mipango ya maendeleo na huduma za utalii anasisitiza kuwa ndege aina ya
tandawili machaka hawapatikani sehemu nyingine yeyote hapa Tanzania,watalii na
watafiti wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani wanafika katika hifadhi ya
Taifa ya Kitulo kwa ajili ya kuwaona ndege hawa ambao wanasafiri umbali mrefu
wa kutoka bara moja kwenda bara jingine.
Anasema ndege hao adimu wanapendwa na watalii wengi
duniani na kwamba hifadhi hiyo ndiyo
eneo pekee ambako ndege hao wanataga
mayai na kuzaliana kwa wingi kabla ya kuruka na kwenda katika mabara mengine.
“Utafiti unaonyesha kuwa kuna ndege
aina ya tandawili machaka ambao waliwekwa alama walipokuwa katika hifadhi ya
Taifa ya Kitulo,ndege hao walionekana na alama zao katika hifadhi moja barani
Australia,utafiti huu ndiyo uliothibitisha kuwa ndege aina hiyo wanasafiri kwa
kuruka toka bara moja kwenda bara jingine’’,alisema mhifadhi huyo.
Hata hivyo alisema ndege hao wamekuwa
na tabia katika msimu Fulani kuruka na kufika katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo
kwa ajili ya kutaga mayai na kuangua vifaranga kutokana na mazingira ya hifadhi
hiyo kuonekana kuwa ni mahali pekee duniani penye mazingira rafiki ndege hao
kuzaliana hivyo mara baada ya kutaga mayai,kuangua vifaranga na ndege kukua,wanaruka na kwenda katika mabara
mengine duniani.
Utafiti umebaini kuwa Katika hifadhi ya
Taifa ya Kitulo ndege wa aina ya abdims
stock,denhams(tandawili machaka) na blue swallow ambao wametoka Afrika ya
kaskazini,Afrika ya kusini,Australia na Ulaya wanaitumia hifadhi ya Taifa ya Kitulo kama
makazi yao katika misimu tofauti.
Ndege
wengine adimu na wanaovutia ambao wanapatikana katika hifadhi hiyo ni mpasua
mbegu mweusi(Kipengere seed eater), lesser kestrel,pallid harrier, Njombe
cristicola, na Uhehe fiscal pia kuna
aina mbalimbali za ndege maji wanaopatikana katika ziwa Nzambe ndani ya
hifadhi hiyo wakiwemo yellow billed duck,white fwced whistling ducks,common
teal,open billed stock,red knobbed coot na uncommon forest magpie manikin .
Andrew Ngunangwa ambaye anaishi kijiji
cha Matamba wilayani Makete kilichopo jirani na hifadhi ya Kitulo anasema ndege
hao wanaruka na kuingia katika makundi makubwa msimu wao wa kutaga hali ambayo
inawavutia watalii na kusisitiza kuwa
hifadhi hiyo ikitangazwa kikamilifu ndani na nje ya nchi inaweza kuvutia
watalii wengi kuja kuangalia mazalia ya ndege hao adimu hivyo kuliingizia taifa
pesa nyingi za kigeni na kufungua milango ya utalii kusini mwa Tanzania.
Watalii wakiwa ndani ya hifadhi ya
Taifa ya Kitulo wanaweza kuangalia ndege adimu
katika ziwa Zambwe na misitu,kuweka kambi kwa ajili ya malengo
mbalimbali, utalii wa kutembea kwa miguu,kupanda farasi,michezo ya gofu na
kukwea milima.
Unapoingia katika hifadhi hiyo msimu wa
maua kuchanua inakuwa kama vile unga umeanikwa katika miinuko ya hifadhi hiyo
hali ambayo inaongeza mvuto kwa kila mmoja ambaye anakuwa amebahatika kuingia
ndani ya hifadhi hiyo.
Kana kwamba haitoshi Hifadhi hii
imebarikiwa na mwenyezi Mungu kwa kuwa na aina zaidi ya 350 za mimea jamii ya
flora.Miongoni mwa mimea maarufu ndani ya hifadhi hii ni jamii ya viazi vya
asili vinavyoitwa vikanda ambavyo hutumika kutengeneza chikanda ambavyo
vinatajwa kuwa na bei kubwa katika nchi jirani ikiwemo Zambia na Zimbabwe.
Mhifadhi Godwel Ole Meing’ataki mratibu
wa miradi, mipango ya maendeleo na uboreshaji huduma vivutio vya utalii
kusini(SPANEST) anasema utafiti umebaini kuwa mimea aina ya vikanda vinavyopatikana
ndani ya hifadhi ya Taifa ya Kituro vina soko kubwa katika nchi za Zambia na Zimbabwe
ambapo debe moja la vikanda hivyo huuzwa kati ya shilingi 80,000 hadi 100,000.
Hata hivyo alisema kabla ya baadhi ya
vijiji kuingizwa katika eneo la hifadhi wananchi wanaozunguka eneo hilo walikuwa
wanaingia na kuchimba vikanda hivyo na kwamba hivi sasa hawaruhusiwi kuchimba
viazi vya asili ndani ya hifadhi hiyo kwa kuwa eneo hilo limetengwa na kwamba kufanya
shughuli zozote ndani ya hifadhi ni ujangili.
“Katika hifadhi nyingine kuna ujangili
wa wanyamapori lakini ndani ya hifadhi ya Taifa ya Kitulo kuna ujangili wa viazi vya asili (vikanda) ambavyo huchimbwa
na kuuzwa katika nchi za nje kwa bei kubwa’’,alisema.
Yapo mengi ya kujivunia katika Hifadhi
ya Taifa ya Kitulo ukiwemo uwanda wa
tambarare, mabonde,vilima na maporomoko ya maji kama Numbi ambapo ndani ya
msitu kuna miti ya aina ya cidar yenye urefu wa zaidi ya mita 50 na inakadiriwa
kuwa ndiyo miti mirefu kuliko yote duniani.
Hifadhi ya Taifa ya Kitulo inafikika
kwa gari kutoka Chimala,kilometa 78
Mashariki mwa mji wa Mbeya unapanda
milima yenye kona 68 ambazo pia ni kivutio hadi katika mji wa Matamba wilayani Makete mkoa wa Njombe.
Reli ya TAZARA hupita karibu na
hifadhi ya Taifa ya kitulo.Pia unaweza kufika ndani ya hifadhi hiyo ukitokea
Zambia kupitia Tunduma ni wastani wa kilometa 170 au Malawi kupitia wilaya ya
Karonga mkoa wa Mzuzu kwa barabara ni wastani wa kilometa 135.
Kutokea jijini Dar es salaam kupitia Makambako, Njombe,Makete hadi Kitulo
ni wastani wa kilometa 963 na kutoka Dar es salaam,Chimala, Matamba hadi Kitulo
ni wastani wa kilometa 836.
Huduma
za hoteli na malazi zinapatikana kwa urahisi ambapo katika jiji la Mbeya kuna
hoteli kadhaa zenye hadhi ya kitalii,pia katika mji wa Matamba ambao upo jirani
na hifadhi hii kuna nyumba za wageni.
Hata hivyo kutokuwapo kwa juhudi za kutosha katika kuhamasisha wananchi
kutembelea hifadhi hiyo kumechangia vivutio vingi vya utalii kutofahamika hata
kwa baadhi ya wenyeji.
Abed
Chaula afisa Utalii Maliasili na Mali kale mkoa wa Njombe amekiri kuwa
licha ya mkoa huo kuwa na vivutio adimu ikiwemo hifadhi ya Taifa ya Kitulo bado
wakazi wake hawana mwamko wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hali
ambayo inachangia kutofahamika kwa vivutio hivyo.
“Wananchi
walio wengi wanadhani wanaostahili kutembelea vivutio hivyo ni watalii kutoka
nje ya nchi pekee, lakini wengine wako hapa mkoani hawajui vivutio vya utalii
vilivyopo mkoani hapa wakiamini kuwa fursa ya utalii ipo katika mikoa ya kuskazini
pekee kwenye hifadhi za Taifa maarufu za wanyamapori,” alisema Chaula.
Chaula
alisema ofisi yake inajitahidi kufanya juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa
vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Njombe na hasa hifadhi ya Taifa ya Kitulo
vinatangazwa pamoja na kutoa hamasa ya kutosha kwa wananchi wa mkoa wa Njombe kutembelea vivutio hivyo.
Mkurugenzi
mkuu wa shirika la Hifadhi za Taifa
Tanzania TANAPA Allan Kijazi akizungumzia hifadhi za Taifa kwa ujumla alisema
hadi sasa shirika lake linasimamia hifadhi 15
za Taifa pamoja na hifadhi ya kisiwa cha Saanane iliyopo mkoani Mwanza ambayo ipo katika mchakato wa
kuanzishwa.
Pamoja na mafanikio
yaliyopatikana katika hifadhi za Taifa, Kijazi amezitaja changamoto
zinazozikabili hifadhi za Taifa kuwa ni pamoja na ujangili unaotokana na
biashara za kujikimu,upungufu wa maji katika baadhi ya hifadhi wakati wa
kiangazi,migogoro ya mipaka katika baadhi ya hifadhi na muingiliano kati ya
wanyamapori na binadamu.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment