Licha ya kuwa ni siku ya huzuni kwa dunia nzima, hotuba ya Rais wa Marekani, Barack Obama imewagusa maelfu ya watu waliokuwa kwenye Uwanja wa FNB katika ibada ya kitaifa kumwaga Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Obama aliyetumia dakika 20 katika hotuba yake iliyokuwa ikikatizwa na
kelele za kumshangilia, aliwataka vijana wa Afrika na dunia nzima kuiga
maisha aliyoishi Mandela kama yeye alivyojifunza mambo mengi kutoka kwa
mzalendo huyo.
“Miaka 30 iliyopita nikiwa mwanafunzi, nilisoma Kitabu cha Mandela na
tangu siku hiyo nilijifunza, nikajenga roho ya uthabiti. Iliamsha
uwajibikaji kwa ajili yangu na kwa ajili ya watu wangu… hakika Mandela
amenifanya niwe hivi nilivyo leo. Michelle na mimi tumenufaika sana na
Mandela,” alisema Obama na kuongeza:
“Mandela alinifanya niwe mtu ninayesimama mbele yenu leo, alichangia
kunifanya kuwa kiongozi bora. Nitaendelea kuiga mfano wake,”
Katika sherehe hizo, Obama alipokewa kwa shangwe na kushangiliwa kila
alipopita na kila alipozungumza tofauti na ilivyokuwa kwa Rais wa nchi
hiyo, Jacob Zuma ambaye alikuwa akizomewa.
Obama alimtaja Mandela kama kiongozi anayefaa kuigwa kwani pamoja na
kukaa gerezani kwa miaka 27 akipigania uhuru, hakutaka kung’ang’ania
madaraka na badala yake alistaafu kwa hiari yake, tofauti na viongozi
wengi wa Afrika.
“Mandela alionyesha uongozi wa vitendo na kujaribu, alikuwa ni
mwanamume, binadamu wa kawaida, mume, baba na kiongozi shupavu,” alisema
Obama.
Pia Obama alisema, Mandela aliachiwa huru kama mfungwa, lakini kama
mwalimu ambaye alitumika kutuonyesha kuwa, ni lazima kuwaamini wenzako
ili nao wakuamini.
“Kufundisha upatanisho, hakuhitaji kudharau historia mbaya ya nyuma
bali ni kuikabili kwa umakini, ukweli na uhalisia wake. Mandela
alibadili sheria, lakini alibadili mioyo yetu pia,” alisema.
Katika risala hiyo, Obama alimtaja Mandela kama mwanamapinduzi mkubwa
wa karne ya 20 aliyeibadilisha mioyo ya watu wake, akaimarisha mapatano
na maelewano kwa wazungu na weusi.
“Amezaliwa kipindi cha Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, kijana aliyekuwa
akichunga ng’ombe na kuteswa na wakubwa zake wa kikabila, lakini
ameibuka na kuwa mwanamapinduzi mkuu wa karne ya 20,” alisema Obama.
Vilevile, Obama alimfananisha Mandela na Abraham Lincoln, Rais wa
zamani wa Marekani kwa kuiunganisha nchi yake pale ilipokuwa inataka
kuvurugika
Rais huyo aliufanya umati katika uwanja huo ulipuke zaidi kwa furaha
baada ya kuzungumza neno la Kizulu, ‘ubuntu’ linalomaanisha utu au
ubinadamu ambapo alisema Mandela ameimarisha utu na ubinadamu kwa
Waafrika Kusini.
“Alidumisha ‘utu’ miongoni mwetu. Utu ambao tunaweza kuupata kwa
kushirikiana na kuwajali wanaotuzunguka,” alisema Rais huyo ambaye
anatajwa kuwa Rais wa dunia. Obama alionyesha umahiri wake katika risala
hiyo na katika sehemu ya risala hiyo alisema ni wajibu wa kila mmoja
kuiga maisha aliyoishi Mandela.
“Ni lazima tujifunze kutoka kwake, kwa sababu Waafrika Kusini kwa jumla wao wameonyesha kuwa, tunaweza kubadilika.”
Obama alimtaja Mandela kama mtu asiyependa kujikweza bali
aliyeshiriki kuonyesha mawazo yake na hofu na uhalisia wake hasa kwa
kusema kuwa yeye si mtakatifu labda kama mtakatifu ni sawa na mwenye
dhambi ambaye hachoki kujaribu. Kiongozi huyo alimalizia hotuba hiyo kwa
nukuu muhimu za Mandela zinazosema kuwa, ‘Mimi ni kiongozi wa imani,
mustakabali wangu, na mimi ni nahodha wa roho yangu’ na kuwataka
Waafrika Kusini kuishi katika maneno hayo ya Mandela katika maisha yao.
“Hakika ilikuwa roho ya ajabu, tutamkumbuka sana. Mungu wabariki
Waafrika Kusini,” alimaliza Obama. Kabla ya hotuba hiyo, Obama alifanya
jambo la kihistoria kwa kupeana mikono na Rais wa Cuba, Raul Castro,
kama ishara ya mapatano baada ya migogoro iliyoko baina ya nchi hizo
mbili.
Kabla ya Obama kuzungumza, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki-Moon katika hotuba yake alisema kuwa, alijitoa muhanga kwa ajili ya
usalama, uhuru na demokrasia ya nchi yake.
“Sherehe hizi za kumbukumbu zinadhihirisha upinde wa mvua wa taifa.
Ninatumaini tutaweza kuuona upinde huo punde, kupitia mvua ya simanzi,”
alisema Ki-Moon. Ki-Moon alimtaja Mandela kuwa ni kiongozi aliyejiandaa
kupoteza kila kitu kwa ajili ya uhuru na demokrasia.
“Dunia imepoteza rafiki na mwalimu. Alikuwa ni zaidi ya viongozi
wakubwa wa nyakati zetu; mwalimu mkuu aliyetufundisha kwa mifano,”
alisema Ki-Moon.
Wakati huo huo, Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Jenerali Thanduxolo
Mandela kwa niaba ya familia ya Mandela alipata nafasi ya kutoa risala
yake kwa Rais huyo na alisema kuwa, familia hiyo ina bahati ya kuwa na
mzazi kama Mandela.
“Utakumbukwa daima, hatuwezi kuusahau mchango wako katika familia na katika maisha ya Waafrika Kusini wote,” alisema Thanduxolo.
Baada ya Thanduxolo, walikuja wajukuu na vitukuu wa Mandela kwa niaba
ya wajukuu wote, Pumla, Andile na Mbuso Mandela ambao walisema wana
mengi waliyojifunza kwa babu yao ambaye walimtaja kuwa kioo cha familia
na kuahidi kuwa wataishi na matendo yake.
Mandela atazikwa Jumapili

No comments:
Post a Comment