Na
Albano Midelo
Inakuzalazimu kusafiri zaidi ya kilometa 170 kutoka Songea makao makuu
ya mkoa wa Ruvuma hadi kulifikia jiwe la kihistoria la Pomonda lenye ukubwa wa
nusu hekari ambalo lipo meta takribani 300 ndani ya ziwa Nyasa kutoka bandari ya Liuli.
Wajerumani walilipa jina la Pomonda
jina la sphinxhaven kutokana na kuwa
na vivutio vya utalii lukuki.
Utalii
wa kihistoria ni aina ya kwanza ya utalii ambayo inapatikana katika jiwe hilo
ambapo tangu vita vya kwanza vya dunia mwaka 1914 hadi 1918 pamoja na vita vya
pili vya dunia mwaka 1939 hadi 1945 wakoloni wa kijerumani na wakiingereza
walitumia pango kubwa lililopo katika jiwe hilo kama sehemu ya kujificha wakati
wa mapambano.
Jiwe la Pomonda linaweza kuhifadhi
watu kati ya 200 hadi 250 ambapo kilele chake kina urefu wa takribani meta 40
kwenda juu ipo taa maalum kubwa yenye
rangi nyekundu ambayo ilikuwa itatumiwa
na nchi tatu za Tanzania,Malawi na Msumbuji wakati wa wakoloni wa
kijerumani,kireno na waingereza kwa ajili ya alama ya kuongozea meli katika
ziwa Nyasa ili wasiweze kupotea
wanapotaka kutia nanga kwenye bandari ya Liuli,taa hiyo iliwawezesha
kuiona bandari ya Liuli hata wakiwa
katika nchi za Malawi na Msumbiji.
Kivutio kingine cha utalii ambacho
kinapatikana katika eneo la jiwe hilo ni mawe matatu makubwa ambayo wakazi wa
eneo hilo wanaamini yamepangwa na mwenyezi Mungu ,huku mpangilio wake ukiwa ni
kivutio cha ajabu utadhani yamejengwa na mafundi ujenzi huku yakiwa yameacha
njia maalum ambayo unaweza kupita kutokea upande wa pili hali ambayo
inawashangaza na kuwavutia wengi.
Jiwe la kihistoria la Pomonda pia ni sehemu
muhimu ambayo inafaa kufanya utalii wa kupiga mbizi pamoja kuwepo utalii wa kuruka toka juu ya jiwe la Pomonda hadi ziwani
umbali wa karibu mita 30 hali ambayo
inawavutia watalii wengi wa ndani na wa kutoka nje ya nchi kwenda mara kwa mara
katika jiwe hilo na kujisikie kana kwamba wapo katika nchi zao ambazo zina
maeneo ambayo wameyatengeneza tofauti na
eneo hilo la jiwe la Pomonda ambalo ni la asili.
Katika eneo lote linalozunguka jiwe la
Pomonda kuna aina zaidi ya 150 wa samaki
wa mapambo hivyo mtalii akifika katika jiwe hilo kuna eneo maalumu ambalo
anaweza kufanya utalii wa kuvua samaki
hao yeye mwenyewe pia anaweza kupika au kupikiwa ugali wa asili wa mhogo ambao ni chakula maalum kwa wakazi wa mwambao
mwa ziwa Nyasa.
Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa
kuna makampuni ambayo wanaendelea kuwavua samaki hao wa mapambo katika eneo
hilo kama shamba la bibi na kwenda
kuwauza Ulaya na Marekani kwa bei kubwa huku
wenyeji wa kata ya Liuli na maeneo mengine ambako samaki hao wanavuliwa
wakibakia mikono mitupu pia serikali inapoteza ushuru halali wa kodi ya samaki
hao ambao inakadiriwa wanauzwa ulaya kwa bei ya kati ya shilingi za kitanzania
80,000 hadi 100,000 kwa samaki mmoja.
Jiwe la Pomonda ni eneo ambalo linafaa kwa ajili ya kufanyia
picnic kwa kuwa lina ukumbi mkubwa ambao umefunikwa vizuri kwa mawe na mwenyezi
Mungu tangu kuumbwa kwa dunia hata wakati wa mvua mtalii anaweza kukaa na kuwa
salama,pia kuna eneo maalum ambalo linafaa kwa kupigia picha huku mtalii
akipata upepo mwananana wa ziwa Nyasa pamoja na kufanya utalii wa kuzunguka
maeneo yote ya jiwe hilo kwa kutumia boti maalum.
Martin Ndomba kutoka kikundi cha
Ntembo Tours Liuli anashauri watalaamu
kutoka wizara ya utalii na maliasili kutembelea katika jiwe la kihistoria la
Pomonda ili kufanya utafiti zaidi na kubaini vivutio vingine zaidi na hata umri
wa jiwe hilo
ambalo linafanana na lile lililopo ziwa Viktoria.
Serikali mkoani Ruvuma imesema vivutio vya utalii ambavyo
vimetambuliwa katika mwambao mwa ziwa Nyasa vitaingizwa kuwa miongoni mwa
vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa wa Ruvuma pamoja na kuviendeleza ili
hatimaye wananchi na serikali waanze kunufaika na vivutio hivyo ambavyo
vitafungua milango ya utalii katika ukanda wa kusini.
Mbunge wa jimbo la Nyasa ambaye pia ni
mjumbe wa Bodi ya utalii katika mkoa wa Ruvuma na Naibu waziri wa
Elimu,Sayansi,Teknolojia na ufundi Injinia Stella Manyanya anasema matangazo ya
vivutio mbalimbali vya utalii katika
vyombo mbalimbali vikiwemo vya ndani ya nchi na vyombo vya kimataifa
yatawezesha vivutio hivyo kufahamika kitaifa na kimataifa hivyo idadi ya
watalii kuendelea kuongezeka mwaka hadi
mwaka na kuliingizia taifa mapato makubwa.
Injinia Manyanya anasema tafiti zinaonesha
kuwa ni watanzania wachache ambao
wanaonekana kuwa na tabia ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo
nchini,mbali ya wanafunzi wa shule za msingi,sekondari na vyuo bado watu wengi
hawajaonesha kipaumbele katika sekta ya utalii.
Hata hivyo anasisitiza elimu sahihi kuhusu
utalii itawezesha kujenga mazoea ya
kutembelea vivutio hivyo na hatimaye kuifanya sekta ya utalii katika mikoa ya kusini kusimama kwa miguu
miwili huku ikipata uwezo wa kutimiza malengo yake hata bila ya kutumia nguvu kubwa
ya kujitangaza.
Anasema mkoa wa Ruvuma umebahatika
kuwa na ziwa Nyasa wilayani ambako
unaweza kufanya utalii wa aina mbalimbali kama vile fukwe za ziwa,samaki wa
mapambo wanaopatikana katika ziwa pamoja
na ngoma za asili na vyakula vya jadi ambavyo kinaweza kuwa kivutio cha kipekee
katika utalii .
Manyanya anabainisha zaidi kuwa licha ya kuwepo utalii wa kuona wanyama au
mambo ya kale, katika mkoa wa Ruvuma kuna utalii wa ngoma za asili na kwamba
mkoa wa Ruvuma una utajiri mkubwa wa ngoma hivyo kuna fursa ya kuutangaza
utalii wa ngoma na amezitaja baadhi ya ngoma hizo kuwa ni
lizombe,kioda,kitoto,mganda,ligihu pamoja na aina nyingine nyingi za ngoma za
jadi.
Ngwatura Ndunguru ni mbunge mstaafu wa jimbo
la Mbinga magharibi na afisa maliasili na utalii mstaafu anabainisha kuwa Moja
ya mambo ambayo yanaweza kuwa ni matunda ya sekta ya utalii katika ukanda wa
kusini ni uboreshaji wa miundombinu hususani ya mawasiliano ya barabara
,usafiri,hoteli za kisasa ili kukidhi
matakwa ya wageni wanaofika kusini kwa shughuli za kitalii.
Mataifa mengi duniani hivi sasa
yanatoka kwenye utalii wa kutegemea mbuga za wanyamapori na kuingia kwenye
utalii wa mambo ya kale,ngoma,hadithi na simulizi za kale hivyo fursa za utalii
katika mkoa wa Ruvuma ni nyingi na zikiibuliwa,zikiendelezwa na kutangazwa mkoa
unaweza kupiga hatua kubwa katika utalii.
albano.midelo@gmail.com
No comments:
Post a Comment