BARAZA la madiwani
katika Halmashauri ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma limewatumbua majipu
watumishi wanne akiwemo afisa utumishi
mkuu kutokana na makosa mbalimbali ya kiutumishi.
![]() |
| Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Alto Komba |
Watumishi waliotumbuliwa majipu katika kikao cha Baraza la madiwani ya Halmashauri hiyo
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Bay live mjini Mbambabay ni pamoja na
Ephrem Kawonga aliyekuwa afisa utumishi mkuu ambaye sasa
ameshushwa cheo baada ya
kutuhumiwa kuhujumu mfumo wa utumishi.
Watumishi wengine
waliotumbuliwa ni pamoja na aliyekuwa afisa mifugo wa Halmashauri hiyo Kalistus
Kisela ambaye amefukuzwa kazi kutokana na kutumia vyeti feki pamoja na watumishi wawili kutoka idara
ya afya ambao ni Pawabu Shaban na Selastine Haule ambao hawakuwepo katika kituo
cha kazi kwa muda mrefu.
Katika kikao hicho
cha Baraza la madiwani kimeridhia taarifa ya mapendekezo ya majina ya watumishi
159 kwa katibu wa Tume ya utumishi wa walimu ya Februari mosi,2016 pamoja na majina
42 ya watumishi wasiokuwa walimu ambapo wamejadili na kukubali watumishi hao
kupandishwa vyeo.
Katika hatua nyingine
Baraza hilo limethibitisha wakuu wa
idara sita walioteuliwa Septemba 2015,kuwa wakuu wa idara kamili baada ya
kuridhishwa na utendaji wao wa kazi kwa mujibu wa masharti ya barua zao za
uteuzi.
Mapendekezo ya
kuwathibitisha katika vyeo hivyo ni kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma
namba nane ya mwaka 2002 ambayo imefanyiwa marekebisho kwa sheria namba 18 ya
mwaka 2007 na kanuni zake za mwaka 2003.
Kikao hicho cha
Baraza la madiwani katika Halmashauri ya Nyasa kilihudhuriwa madiwani 27,wakuu
wa idara,wataalam mbalimbali pamoja na mbunge wa jimbo la Nyasa ambaye pia ni
Naibu waziri wa Elimu,Sayansi,Teknolojia na mafunzo ya ufundi Injinia Stella
Manyanya.
mapundakwirinus@yahoo.com

No comments:
Post a Comment