Sunday, May 1, 2016

Diwani awalipa wenyeviti wa vijiji posho kila mwezi


Na Kwirinus Mapunda
Katika hali isiyokuwa ya kawaida  diwani wa kata ya Linga wilayani Nyasa mkoani Ruvuma Edmund Magendo ameamua kuanza kuwalipa posho ya kila mwezi wenyeviti wa  vijiji  vilivyopo katika kata yake.
Diwani wa kata ya Linga Edmund Magendo kushoto
Akizungumza na mwandishi wa habari hizo mjini hapa diwani huyo kijana amesema ameamua kuwalipa posho kila mwezi kwa kutambua mchango wa maendeleo kwa wenyeviti wa vijiji katika kata yake hivyo ili kuwatia moyo ameamua kuanza kuwalipa posho viongozi wa vijiji vitatu vya Ngingama,Litumbakuhamba na Lukali vinavyounda kata mpya ya Linga ambayo imemegwa kutoka kata ya Lituhi.


Diwani huyo pia amewalipia kadi za mfuko wa afya ya jamii CHF kwa wenyeviti wote wa vitongoji  12 vilivyopo katika kata hiyo ili waweze kupata huduma za afya  kwa urahisi wao na familia zao hali ambayo itawaongezea motisha ya kufanyakazi zaidi ili kwenda sanjari ya kauli mbiu ya Rais ya hapa kazi tu.
“Kwa mwaka kila mwenyekiti wa kijiji atapata fedha ya posho zisizozidi laki moja na nusu hivyo katika bajeti yangu kwa mwaka nimetenga karibu shilingi laki tano kwa ajili ya posho kwa wenyeviti wangu watatu wa vijiji,nawalipa kila baada ya miezi mitatu,sina uwezo mkubwa natarajia kuwalipa katika kipindi changu chote cha miaka mitano ya udiwani’’,alisisitiza.
Kutokana na serikali  kutokuwa na bajeti ya kuwalipa posho wenyeviti wa mitaa,vijiji na vitongoji,diwani huyo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi ametoa wito kwa Rais John Magufuli kuangalia uwezekano wa kuanza kuwalipa posho wenyeviti hao kama zinavyotolewa kwa madiwani kwa kuwa viongozi hao ni msingi wa kuchochea na kuhamasisha maendeleo kuanzia ngazi ya chini.
Mwanasheria mahiri nchini Dk.Nshala Rugemeleza alisema katika sheria ya ardhi ya mwaka 1999 inaonesha kuwa asilimia 70 ya ardhi  ipo chini ya  serikali ya kijiji hivyo serikali ya kijiji ina nguvu ya kisheria na anashangaa kwanini mwenyekiti wa serikali ya kijiji halipwi mshahara wakati ana majukumu mazito ya kiserikali.
Diwani huyo pia amefungua mfuko wa kukopeshana kwa gharama nafuu katika vijiji vya kata yake ambao unamwezesha mwananchi yeyote kukopa fedha na kurudisha ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kata yake.
Kwa mujibu wa Magendo,kata ya Linga ina watu karibu 5000 hivi sasa na kwamba kata hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa kituo cha afya hali inayosababisha watu kusafiri zaidi ya kilometa 30 hadi 40 kufuata huduma za afya ambapo waathirika wakubwa ni wanawake wajawazito na watoto.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa ofisi mbalimbali ikiwemo ofisi ya afisa mtendaji wa kata,ukosefu wa shule ya msingi katika kijiji cha Ngingama,ukosefu wa chumba za kuhifadhia dawa katika zahanati ya Ngingama pamoja na ukosefu wa wodi ya wajawazito katika zahanati ya kijiji cha Ngingama.
Pamoja na changamoto hizo diwani Magendo anaitaja miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa katika vijiji vya kata  hiyo kuwa ni pamoja na ukarabati wa zahanati  na ujenzi wa nyumba za watumishi katika kijiji cha Litumbakuhamba.
“Miradi mingine ni kilimo cha umwagiliaji katika kijiji cha Ngingama,ujenzi wa ofisi ya kijiji cha Ngingama,kwa ujumla katika kata yangu shughuli za kiuchumi zilizopo ni kilimo,uvuvi,ufugaji na biashara ndogo ndogo’’,alisisitiza.
Mwisho

No comments:

Post a Comment