Na Albano
Midelo
Utumikishaji
watoto wadogo bado unaendelea nchini Tanzania licha ya serikali kuweka sheria
ya kumlinda mtoto mwenye umri usiozidi miaka 18.
Nimepita
katika baadhi ya maeneo mjini Songea na kubaini idadi kubwa ya watoto wenye
umri kati ya miaka tisa na 12 ambao wanazunguka kuuza bidhaa ndogo ndogo na
wengine wanaombaomba.
Said Ally ni
mtoto anayesoma darasa la pili katika shule moja mjini Songea ambaye anafanya
biashara ya kuuza karanga za kukaanga.
“Nimeanza
biashara hii tangu darasa la kwanza
nikitoka shuleni saa tano nafika mjini kuuza karanga katika maeneo
mbalimbali yakiwemo ya klabu za pombe,
hadi kufika saa tisa nakuwa nimemaliza
kuuza karanga ambapo kwa siku Napata shilingi 5000’’,anasema.
Anadai pesa
anayopata inamsaidia yeye na familia yake kuendesha maisha kila siku,ingawa
amekiri kuwa inamwathiri katika masomo yake kwa kuwa hapati muda wa kutosha
kushiriki katika masomo.
Uchunguzi
ambao nimeufanya katika viunga mbalimbali vya mjini Songea majira ya usiku wa
kuanzia saa mbili hadi saa tano usiku nimeshuhudia makundi ya watoto wadogo
wakifanyabiashara hatarishi kutokana na mazingira.
Tatizo la kuwatumikisha watoto wadogo
kazi halifanyiki kwa ajili ya biashara
pekee bali pia watoto wameonekana wakifanyishwa kazi katika maeneo mengine kama
vile maeneo ya machimbo,kazi za ndani na uvuvi.
Kwa mfano katika machimbo ya Tanzanite
Mirereni mkoani Manyara watoto wadogo wanatumikishwa kuingia katika mashimo madogo yenye kipenyo
kidogo kwenda chini ardhini kwa kutumia ngazi au kamba jambo ambalo ni hatari
kwa watoto kiafya.
Mwambao mwa ziwa Nyasa mkoani Ruvuma
kuna idadi kubwa ya watoto ambao wameacha shule na kufanyakazi ya uvuvi wa
samaki licha ya kulipwa ujira mdogo.
Sheria ya haki za mtoto ya mwaka 2009 inabainisha wazi kuwa mtu
hataruhusiwa kumuajiri au kumshughulisha mtoto katika aina yoyote ya kazi
itakayomnyonya mtoto.
Kwa mujibu wa sheria hiyo,mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya kutengwa
au matendo yoyote yanayoweza kuwa na athari mbaya kwake kwa kuzingatia umri na
uwezo wake.
Sheria inabainisha kuwa,kazi itakuwa ni ya kinyonyaji kwa mtoto iwapo
inamnyima mtoto kuwa na afya njema au maendeleo,haifai kwa umri wake au mtoto
hapati malipo ya kutosha.
Mtu yeyote anayevunja sheria katika kifungu hicho,sheria inaelekeza
wazi kuwa atakuwa anatenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini
isiyopungua shilingi laki moja au kutumikia kifungo kwa muda wa miezi mitatu au
vyote kwa pamoja.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 174
zilizoridhia Azimio la umoja wa mataifa namba 182 la kukomesha utumikishaji
watoto chini ya umri wa miaka 18.
Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa
pamoja na jitihada za serikali za kupiga vita utumikishaji watoto bado watoto
wamekuwa wakitumikishwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa visingizio
mbalimbali ambavyo havina msingi wowote.
Shirika la Kuteteta
Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, watoto wa maeneo ya
migodi nchini Tanzania wanakabiliwa na mazingira magumu.
Ripoti inabainisha
inataja idadi kubwa ya watoto wameathirika kiafya kutokana na kufanyishwa kazi
ngumu zikiwemo za kwenye migodi.
Kulingana na ripoti hiyo,kuna vitendo vya dhuluma na ukatili wa
kingono unaofanywa dhidi ya watoto hao na kwamba watoto wapo katika hatari ya
kupata magonjwa mbalimbali kutokana na vumbi la madini.
Umoja wa Mataifa ulipitisha mkataba wa haki za
watoto ili kumlinda mtoto asinyanyaswe na kukoseshwa haki zake za msingi kama
vile kupata elimu, matunzo na kadhalika.
Ajira ya watoto ni tatizo sugu ambalo
halijapatiwa ufumbuzi katika nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania,huku
sababu kubwa ikitajwa kuwa ni ujinga,maradhi,vita na umaskini.
Kupitia katika vyombo mbalimbali vya
habari tumeshuhudia watoto wakilazimika kufanya kazi ngumu ya kuponda kokoto
ili kuweza kupata fedha za kuendeshea maisha ya familia hivyo kuathiri taaluma.
Ruvuma,Mwanza,Arusha,Mbeya,Dar es salaam na Morogoro
ni miongoni mwa mikoa ya Tanzania yenye idadi kubwa ya watoto walioacha shule
na kugeuka kuwa watoto wanaofanya biashara ndogondogo na wengine wamegeuka
ombaomba.
Ukitembea katika miji hiyo ni jambo la kawaida kukutana na watoto ambao walitakiwa kuwa shuleni badala yake wamekuwa watoro,wakifanya biashara ndogondogo ili waweze kujikomboa kiuchumi.
Utafiti umebaini kuwa baadhi ya watoto hulala katika veranda za maduka makubwa yaliyopo katika miji na wengine hulala katika maeneo ya vituo vya mabasi.
Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2014
alishtushwa na kiwango kikubwa cha wanafunzi wa shule za msingi katika mkoa wa
Ruvuma kushindwa kuhudhuria na kumaliza shule kwa sababu mbalimbali, ukiwemo
utoro.
Changamoto ya utoro ni kubwa hapa nchini kwa mfano katika mkoa wa
Ruvuma,takwimu za utoro zinaonesha kuwa kati ya watoto 41,801 walioanza shule
ya msingi mwaka 2007 ni watoto 30,698 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya
msingi mwaka 2013.
Takwimu
za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonesha kuwa, tangu mwaka 2004 hadi
2008, wanafunzi wa kike 28,600 walishindwa kuendelea na masomo huku sababu
nyinginezo ikiwa ni utoro,ajira na mimba za utotoni.
Kuendelea kuwepo watoto wanaoacha masomo kutokana na sababu mbalimbali, kunaipa serikali changamoto kubwa ikizingatiwa wadau wa elimu wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kuhimiza usawa wa kijinsia katika elimu.
Tathmini ya ripoti ya malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs) inaonesha kwamba serikali ilidhamiria kuhakikisha ifikapo mwaka huu 2015, hakuna mwanafunzi wa shule ya msingi anayekatiza masomo,jambo ambalo limeshindikana kwa sababu idadi ya watoto wanaoacha shule kwa sababu mbalimbali inaongezeka badala ya kupungua.
albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917


No comments:
Post a Comment