Na Kwirinus Mapunda,Peramiho
Shule ya sekondari ya
Maposeni iliyopo katika Halmashauri ya wilaya
ya Songea mkoani Ruvuma inakabiliwa upungufu mkubwa wa vitanda hali
inayosababisha wanafunzi wawili wawili kulala katika kitanda kimoja.
Shule hiyo pia inakabiliwa
na uhaba wa mabweni ya kulala kufuatia idadi kubwa ya wanafunzi wanaoletwa kuanza kidato cha tano hali iliyosababisha
baadhi ya madarasa kubadilishwa matumizi na kuwa mahali pa kulala.
Risala ya wanafunzi wa
shule hiyo iliyosomwa na wanafunzi Ezekiel Kazeni na Prudensia Kitusi katika
mahafali ya saba ya kidato cha sita katika shule hiyo imezitaja changamoto
nyingine zinazoikabili shule hiyo kuwa ni kutokamilika kwa ukumbi wa
chakula,mikutano na mitihani yaani multipurpose hall.
Kwa mujibu wa risala
hiyo changamoto nyingine ni upungufu wa nyumba za watumishi ambazo zipo nane tu
kati ya nyumba 48 zinazohitajika hali iliyosababisha walimu wengi kupanga mbali
na eneo la shule.
Mkuu wa shule hiyo
Dismas Nchimbi alizitaja changamoto nyingine kuwa ni uchakavu wa majengo ya
shule,nyumba za watumishi,ofisi na vyumba vya madarasa kwa kuwa majengo hayo ni
ya zamani ambayo yalijengwa mwaka 1987 wakati shule hiyo inafunguliwa.
“Kukosekana kwa maji ya
uhakika ni changamoto kubwa ambapo shule hutegemea maji ya visima tu ambayo ni
ya msimu na hayakidhi mahitaji ya idadi ya wanafunzi 903 waliopo hivi sasa
kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita’’,alisema.
Pamoja na changamoto
hizo Nchimbi alisema shule hiyo imepata mafanikio makubwa katika kutekeleza
majukumu ya kutoa elimu bora kwa mujibu wa Matokeo Makubwa Sasa ambapo shule
hiyo imeweza kufaulisha wanafunzi wa
kidato cha sita kwa asilimia 100 kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015.
Mafanikio mengine
ameyataja kuwa ni shule imefanikiwa ujenzi wa bwalo la chakula ambalo
limeezekwa hata hivyo ametoa wito kwa wadau mbalimbali kusaidia kukamilisha
ujenzi huo na kwamba shule ina mradi wa ufyatuaji wa tofali zinazotumika katika
miradi ya ujenzi ambapo hadi sasa tayari tofali 105,000 zimefyatuliwa lengo
likiwa wanafunzi kuwafundisha elimu ya kujitegemea.
Katika mahafali hayo
jumla ya wahitimu 218 kati yao wavulana 131 na wasichana 87 walitunukiwa vyeti
vya kuhitimu.Shule ya sekondari ya Maposeni ilianza rasmi mwaka 1987 na kutoa
wahitimu wa kwanza wa kidato cha nne wapatao 53 mwaka 1990 ambapo kidato cha
tano kilianza rasmi mwaka 2008.
Mwisho
No comments:
Post a Comment