Peramiho ni eneo maarufu ndani na
nje ya Tanzania ambalo linapatikana kilometa 24 tu kutoka mjini Songea mkoani
Ruvuma.
Kata ya Peramiho yenye wakazi zaidi ya 14,000 kwa mujibu wa sense ya
watu na makazi ya mwaka 2012 ipo katika
Halmashauri ya wilaya ya Songea,kata hiyo inaundwa na vijiji vinne ambavyo ni
Peramiho A,Peramiho B,Lundusi na kijiji cha nguvumoja .
Afisa mtendaji wa kata ya Peramiho Salma Kipande anasema ili kuhakikisha
kuwa wananchi wa kata hiyo wanatekeleza kauli mbiu ya Rais John Magufuli kwa
Vitendo ya Hapa kazi tu kuna mipango kabambe ya maendeleo ambayo wameipanga
katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 inatekelezwa katika vijiji vyote vinne
ambayo vinaunda kata hiyo ambayo ndiyo kioo cha Halmashauri ya wilaya ya
Songea.
Katika kuhakikisha kuwa kauli ya hapa kazi tu inatekelezwa kwa vitendo
katika kata hiyo,afisa mtendaji wa kata hiyo , Salma Kipande anasisitiza kuwa
katika kikao cha kamati ya maendeleo ya kata hiyo kilichofanyika hivi karibuni,moja
ya mambo ambayo yalipitishwa na wajumbe wote ni pamoja na kuwa na benki ya
tofali ambapo kila kijiji kimeweka mkakati wa kufyatua tofali laki tatu.
“Tofali hizo zitafyatuliwa kuanzia mwezi Juni na kuchomwa mwezi Julai ,
vijijini vinne vinahusika ambavyo ni Peramiho A,Peramiho B,Lundusi na Nguvumoja
ambapo jumla tutakuwa na tofali milioni moja na laki mbili ambazo zitatumika
katika miradi mbalimbali ya ujenzi zikiwemo ofisi,vyumba vya madarasa,zahanati
pamoja na shughuli nyingine ambazo zinahitaji tofali’’,alisisitiza.
Kwa upande wake kaimu mratibu elimu kata ya Peramiho Rashid Pilly
amesema kata hiyo ina jumla ya shule za msingi sita pamoja na shule mbili za
sekondari ambazo zinamilikiwa na serikali na kwamba kuna shule moja ya
sekondari ambayo inamilikiwa na Abasia ya Peramiho.
Hata hivyo amesema kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi kata hiyo
inafanya sensa ya wanafunzi pamoja na kupima eneo ambalo limepangwa kujengwa
shule mpya ya msingi ya Ukombozi katika eneo la Njunde Peramiho linalokadiriwa
kuwa na hekari 10 na kwamba kinachosubiriwa ni ramani kutoka Halmashauri ya
wilaya ya Songea vijijini ili kazi ya ujenzi iweze kuanza mapema mwaka huu.
Hata hivyo kaimu mratibu elimu kata huyo ambaye pia ni mwalimu mkuu
msaidizi shule ya msingi Peramiho A ameitaja changamoto kubwa ambayo inaikabili
shule hiyo ni kuoza kwa vigae vilivyotumika kuezeka shule hiyo ambapo msimu
wote wa mvua wanafunzi wanashindwa kusoma kutokana na vyumba viwili vya
madarasa kuvuja hivyo kuathiri tendo la ufundishaji.
“Vigae vyote vilivyotumika kuezekea shule hiyo vimeoza vinatakiwa
kuondolewa ni vya muda mrefu badala yake shule iezekwe upya kwa kutumia bati
ili kudhibiti kuvuja kwa vyumba vya shule na kuathiri ujifunzaji na
ufundishaji’’, alisisitiza Pilly.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha Nguvumoja ambaye ni kaimu diwani wa kata
ya Peramiho Joseph Ngonyani amesema kata ya Peramiho imedhamiria kusonga mbele
katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, mazingira, mapato,michezo na kuboresha
huduma zote muhimu za kijamii kwa wananchi.
Hata hivyo aliitaja changamoto ya
maji katika vijiji vya kata ya Peramiho imekuwa kero kubwa katika vijiji
vyote vinavyounda kata ya Peramiho na kusisitiza kuwa katika kijiji cha
Peramiho B kuna upungufu mkubwa wa maji safi na salama ambapo katika vijiji vya
Nguvumoja,Peramiho A na Lundusi maji yanapatikana kwa gharama kubwa.
Amesema kuwa katika vijiji vya Peramiho A na Nguvumoja umeanzishwa mradi
wa maji ya bomba ambao unafahamika kwa kifupi cha majina ya vijiji viwili yaani
PENGU ambao ni mradi wa maji ya bomba unaoendeshwa kwa umeme wa jenerata kutoka
chanzo cha maji cha mto Namihoro.
“Wananchi wengi wanashindwa kulipia bili za maji katika mradi huu ambapo
gharama kwa mwezi inafikia hadi shilingi 50,000 na ndoo moja inatozwa shilingi
50 hali ambayo inasababisha wananchi kushindwa kumudu kulipa hivyo kubakia kuwa
changamoto kwa wananchi masikini’’,alisema mwenyekiti wa kijiji cha Peramiho A
David Kapinga.
Hata hivyo utafiti ambao ulifanywa na waandisi wa maji wa Halmashauri ya
wilaya ya Songea katika vyanzo vya kata hiyo umebaini kuwa vyanzo vyote vya
maji vilivyopo vina maji ya kutosha kinachotakiwa ni serikali kuwawezesha umeme
wa TANESCO ili kupunguza gharama za kutumia jenereta za mafuta ambazo zina
gharama kubwa katika uendeshaji wake.
Kamati ya maendeleo ya kata ya Peramiho imependekeza kwa kauli moja
kuchimba kisima cha maji ili kutatua tatizo la maji katika shule ya msingi
kijiji cha Mnyonga yenye wanafunzi 200 kati yao wanafunzi 20 ni wenye ulemavu
wa akili.
Shule hiyo inatumia vyoo vya kisasa ambavyo vinahitaji maji mengi ambapo
hivi sasa kutokana na gharama kubwa ya kulipia maji inayotozwa katika mradi wa
PENGU,shule hiyo ina kosa maji hali ambayo inahatarisha wanafunzi hao kupata
magonjwa ya maambukizi hasa katika kipindi cha kiangazi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Peramiho A Jommo Mbilinyi alisema kijiji chake
kinaendelea kutekeleza kwa vitendo kauli ya Rais Magufuli kwa vitendo ambapo
tayari kijiji kimejenga zahanati ya kijiji ambayo imekamilika kwa asilimia 80
pamoja na ofisi ya serikali ya kijiji ya kisasa ambayo inatarajia kugharimu
shilingi milioni 60 hadi itakapokamilika .
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii kata ya Peramiho Pirmin
Mbilinyi amesema idara yake inafanya hamasa kubwa ya kuhakikisha kuwa vikundi
vya ujasirimali vilivyosajiriwa vinaundwa katika kata hiyo ambapo hadi sasa
katika kata nzima kuna vikundi vya ujasiriamali vilivyosajiriwa 20.
Mbilinyi anasisitiza kuwa
uhamasishaji mkubwa unafanywa na ofisi ya maendeleo ya jamii katika kata
hiyo kuhakikisha kuwa wananchi wake
wanakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kata inasonga mbele kiuchumi ili kila
mmoja afanye kazi kwa bidii kama kauli
mbiu ya hapa kazi ilivyoagiza.
Akizungumzia mahusiano kati ya serikali kata ya Peramiho na uongozi wa
kanisa katoliki Abasia ya Peramiho,afisa mtendaji wa kata hiyo Salma Kipande
amesisitiza kuwa kanisa katoliki katika Abasia hiyo linashirikiana vema na
serikali kwa miaka mingi na kwamba limekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo
ya kata hiyo hasa katika sekta ya afya na elimu.
Kipande anasisitiza kuwa kanisa katoliki linatekeleza kwa vitendo kauli
mbiu ya hapa kazi tu kwa sababu katika Taasisi mbalimbali zilizopo katika
Abasia hiyo kanisa limetoa ajira kwa watanzania pamoja na kutoa huduma muhimu za afya na elimu
katika ngazi mbalimbali kwa maendeleo ya watanzania na Taifa kwa ujumla wake.
Abasia ya Peramiho ina seminari
kuu inayohudumia nchi nzima,hospitali ya misheni ya rufaa inayohudumia watanzania kutoka nchi
nzima,chuo cha uuguzi,kiwanda cha uchapaji yaani Peramiho printing press,chuo
cha ufundi seremala,magari na umeme na tawi la chuo kikuu cha madaktari
Bugando.
Utafiti umebaini kuwa
Peramiho inafahamika zaidi nje ya nchi pengine kuliko miji mingine
iliyopo kusini mwa Tanzania kutokana na mji huo kuwa na historia ya namna yake
kipekee.Peramiho
inaunganishwa
na wabenediktini wa kanisa katoliki kutoka St.Otilia nchini
Ujerumani,ambao waliamua kuweka makao makuu yao katika Abasia ya Peramiho.
Wabeneditine hao waliingia kwa
mara ya kwanza katika mji huo mkongwe mwaka
1898 wakiongozwa na Kasian Spiss.Tangu wakati huo wabenediktine hao
wamekuwa na wakifanya mambo mazuri na ya
kipekee katika eneo hilo hali iliyosababisha
kuutambua Peramiho kuwa ni eneo
linalokidhi vigezo kuwa na utalii wa
kihistoria na kitamaduni.
Mhifadhi kiongozi wa makumbusho
ya Taifa Philipo Maligisu anasema
wabenediktine wa Abasia ya Peramiho wametengeneza historia ya kipekee na
kuvutia katika nchi ya Tanzania ni pale walipoamua kujikita katika suala zima
la elimu na kuamua kuwekeza katika elimu zaidi ya miaka 100 iliyopita hadi
sasa.
Wabenediktine hao walizindua rasmi mji huo
Julai 31,1898 na tangu hapo waliendelea na shughuli zao wakiwa na mahusiano
mazuri wakati huo na utawala wa machifu katika eneo hilo.
Hadi sasa watanzania wengi hapa
nchini bado hawajatambua kuwa eneo la Peramiho lina historia ya kipekee
inayowaunganisha wananchi wa mkoa wa Ruvuma na sehemu nyingine duniani na hasa
nchi ya Ujerumani ambao wanaitambua sana Peramiho.
“Wananchi wa Ujerumani wanaijua sana Peramiho pengine kuliko hata
sisi watanzania,ndiyo maana kizazi na
kizazi wanasafiri kwa gharama kubwa hadi katika mji huo ili kufanya utalii wa
kihistoria kwa kutembelea katika maeneo mbalimbali ya kihistoria na kujifunza
mambo mbalimbali”,anasisitiza Maligisu.
Sera ya taifa ya utamaduni ya
mwaka 1997 ina tamka bayana kuwa eneo lolote la kihistoria linapokuwa
limetimiza miaka 100 moja kwa moja
linaingia katika urithi wa utamaduni wa
taifa.
Kutokana na hali hiyo
ukiangalia mji huo wa Peramiho tayari umekidhi vigezo na maeneo yake yote ya
kihistoria kuingia katika urithi wa utamaduni wa taifa kwa ajili ya kujifunza
elimu na utalii ndiyo maana makumbusho
ya taifa inafanya mchakato wa kuliingiza eneo la Peramiho katika urithi wa
utamaduni wa taifa.
Mawasiliano:mapundakwirinus@yahoo.com

No comments:
Post a Comment