Na Albano Midelo
Uchumi endelevu
hauwezi kujengwa na Taifa lenye watu wagonjwa,kwa kuwa watatumia muda mwingi
kulala bila kuzalisha mali hali ambayo itachangia kuongezeka kwa umaskini.
Watanzania wengi
wanakabiliwa na adui maradhi yanayosababisha kuugua magonjwa mbalimbali na
kupoteza maisha kila mwaka kutokana na kuwepo kwa idadi ndogo ya madaktari ambao hawakidhi idadi ya
watanzania wanaofikia milioni 45.
Shirika la afya
Duniani WHO linaitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye madaktari wachache
sana ambapo uwiano wa daktari mmoja ni kuhudumia wagonjwa 30,000,wakati WHO
inapendekeza daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 1000.
Takwimu zinaonesha
kuwa katika nchi nzima kuna madaktari wasiozidi 2000 kati ya hao asilimia 32 tu
wanafanyakazi katika jiji la Dar es salaam,asilimia tisa wanafanyakazi katika
mikoa ya Mbeya,Arusha,Mwanza na Kilimanjaro,asilimia 19 wanafanyakazi katika
mikoa mingine ya Tanzania na asilimia 40 ya madaktari hao hawafanyi kabisa kazi
ya utabibu licha ya kuwa na taaluma ya utabibu.
Kutokana na takwimu
hizo asilimia 80 ya watanzania hawana madaktari, kwa hiyo kuna idadi kubwa ya
watanzania hasa katika maeneo ya vijijini ambao wanaugua magonjwa mbalimbali na
wengine wanapoteza maisha kwa sababu ya kukosa huduma ya utabibu hali hiyo
inachangia kuzorotesha uchumi kwa kuwa kuna nguvukazi kubwa inapotea au kuugua
na kushindwa kufanyakazi.
Hali hiyo ndiyo
iliyolisukuma Baraza la Maaskofu Tanzania kuanzisha shahada ya kwanza ya
udaktari katika chuo kikuu kishiriki cha SAUT tawi la Songea ambacho
kinajulikana kwa jina la Archbishop James University College (AJUCO) kampasi ya
udaktari Peramiho jimbo kuu katoliki la Songea.
Kutokana na
changamoto kubwa ya madaktari nchini hasa vijijini chuo cha AJUCO kupitia
kampasi yake ya udaktari Peramiho
inaandaa mfumo maalum wa madaktari watakaohitimu kufanyakazi vijijini
ambako kuna idadi kubwa ya watanzania wanaokosa huduma ya utabibu.
Mfumo wa kuwaandaa
madaktari kupenda kufanyakazi vijijini umefanikiwa katika nchi za Canada na
Brazil na kwamba AJUCO ina matarajio
makubwa ya kufanikisha mfumo huo katika
kozi ya madaktari ambayo ilianza mwaka juzi ikiwa na na jumla ya wanafunzi 257
kozi hiyo itachukua miaka mitano.
Kwa
mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania inatumia kati ya dola za
kimarekani 40,000 hadi 60,000 kusomesha daktari mmoja ambapo inakadiriwa
madaktari wanne kati ya kumi wanaomaliza elimu ya utabibu wanaacha fani ya
utabibu muda mfupi baada ya kuhitimu masomo yao.
Utafiti unaonesha kuwa katika mikoa ya
pembezoni kama Kigoma daktari mmoja anahudumia watu 308,000,Mara watu 167,000,
Tabora daktari mmoja anahudumia watu 132,000,Pwani watu 32,000,Arusha watu 22,000 na jiji la Dare s
salaam watu 24,000.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa pamoja na
eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara kubeba asilimia 24 ya mzigo wa magonjwa
duniani, kuna asilimia tatu tu ya nguvukazi katika sekta ya afya na asilimia
moja tu ya rasilimali fedha duniani.
Hata hivyo kitendo
cha chuo kikuu kishiriki cha SAUT kampasi ya udaktari Peramiho kuanzisha mfumo
maalum wa kuwaandaa madaktari kufanya kazi vijijini huenda kutasaidia
kukabiliana na tatizo la uhaba mkubwa wa madaktari hasa katika maeneo ya vijijini.
Chama
cha Madaktari Tanzania (MAT), kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali
la SIKIKA, vimefanya utafiti ambao umeonyesha kwamba asilimia 39.6 ya madaktari
nchini hawafanyi kazi ya kutoa huduma za kitabibu wala za kiutawala katika
Sekta ya Afya, badala yake wanafanya shughuli nyingine tofauti kabisa na fani
ya utabibu.
Utafiti
huo ulioshirikisha madaktari 2,246 waliohitimu shahada zao nchini,
unabainisha kuwa madaktari 890 kati ya 2,246 sawa na asilimia
39.6 ya wataalamu hao wa utabibu nchini hawafanyi kazi ya kitabibu licha ya
kusomea hali ambayo inazorotesha sekta hiyo muhimu kwa uhai wa binadamu na
maendeleo ya uchumi.
Kulingana na matokeo ya utafiti huo ni
madaktari 964 tu kati ya 2,246 ndio wanaofanya kazi katika hospitali na vituo
vya huduma za afya hapa nchini wengi wao wakifanya kazi katika majiji na miji
mikubwa na kwamba kuna madaktari 184 wa kitanzania ambao wanafanyakazi nje ya
nchi.
Hata hivyo kuna sababu nyingi ambazo zinatajwa
na madaktari hao zinazowasukuma kuacha kufanyakazi waliosomea au wengine
kukimbilia maeneo ya mijini au nje ya nchi zikiwemo za uhaba wa
vitendeakazi,nyumba bora za kuishi,mishahara ambayo hailingani na ugumu wa
kazi,posho na masilahi mengine.
albano.midelo@gmail.com

No comments:
Post a Comment