Saturday, May 7, 2016

Beatrice anahitaji msaada amekatwa miguu yote



Ama kweli hujafa hujaumbika
Na Kwirinus Mapunda

“Nisingekatwa miguu yote miwili ningekufa siku nyingi kwa kuwa madaktari walisema mifupa ya miguu yote imeathirika dawa pekee ni kukatwa miguu yote ili niweze kuendelea kuishi’’,anasema Beatrice Ndomba kwa masikitiko makubwa.
Beatrice baada ya kukatwa miguu

Mtawa anayefahamika kwa jina moja la Sr.Lucy  kutoka shirika la watawa wa mtakatifu Vincent jimbo katoliki la Mbinga ambaye anahusika na idara ya wenye ulemavu wa viungo ndiye aliyemchunguza na kubaini miguu yake imeathirika ndipo alimfadhili nauli na fedha za matibabu katika hospitali ya Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe.

“Baada ya kufika katika hospitali hiyo nilipigwa X RAY,na kubaini kuwa wadudu wa hatari walikuwa wameshaingia hadi katika mifupa,madaktari walinishauri kuwa iwapo mguu huo hautakatwa wadudu hao wataathiri katika maeneo  muhimu hadi kwenye moyo na kunisababishia kifo hivyo nilikubali kukatwa mguu wangu wa pili
hivyo kubakia bila miguu lakini nikiwa mzima wa afya’’,alisema.

Hata hivyo anasema tangu amekatwa mguu wa pili maumivu yote yamekwisha isipokuwa sasa amekuwa tayari mlemavu wa viungo na kwamba anamshukuru Sr.Lucy kwa utaalamu wake pamoja na kumpatia misaada mbalimbali ya fedha na baiskeli ya wenye ulemavu ambayo anaitumia hivi sasa.

Beatrice anahitaji msaada wa miguu ya bandia  hivyo mfadhili yeyote ambaye anaweza kumsaidia gharama za viungo hivyo bandia atakuwa ametoa mchango mkubwa kwa Beatrice.



Beatrice mwenye umri wa miaka 23 alizaliwa mwaka 1992 ,hivi sasa ni mlemavu wa viungo baada ya kukatwa miguu yake yote miwili,anaishi katika mtaa wa Ruhuwiko kanisani manispaa ya Songea mkoani Ruvuma anapatikana kwa namba ya simu 0766642634 au 0673054535 unaweza kuwasiliana naye.

Anabainisha kuwa mguu wake wa kwanza alikatwa  mwezi Agosti,2012 katika hospitali ya Rufaa ya Peramiho iliyopo kilometa 24 kutoka mjini Songea  na mguu wake wa pili alikatwa  Julai 2014 katika hospitali ya Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe.

Anasema alizaliwa salama kabisa wala hakutarajia kwamba siku moja atakuwa mlemavu,amesoma darasa la kwanza shule ya msingi Ruhuwiko manispaa ya Songea,kisha kuendelea na darasa la pili hadi la saba jijini Mbeya ambako alikuwa anaishi na wazazi wake.

 Alijiunga na elimu ya sekondari ya Forest iliyopo jijini Mbeya ambako alisoma kuanzia kidato cha kwanza hadi kufanikiwa kumaliza kidato cha nne mwaka 2010  akiwa hana ulemavu wowote.

Hata hivyo anasema mwaka 2012 tatizo lililosababisha kupata ulemavu wa viungo lilianza akiwa amejiunga kwa ajili ya masomo stashada ya uhasibu katika chuo cha Uhasibu jijini Mbeya mwaka wa kwanza ndipo alianza kupata maumivu makali katika mguu wake mmoja hali iliyomsababishia kushindwa kuendelea na masomo na kurudi Songea kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Homa ilianza kwa kujisikia kama dalili za ugonjwa wa malaria hivyo nilipewa dawa aina ya SP ambayo haikuweza kunisaidia ndipo nilipelekwa hospitali ya Songea ambapo nilitundikiwa dripu la kwinini ambayo pia haikusaidia, homa iliendelea kwa kasi huku nikipata maumivu makali  kwenye miguu ambayo ilikuwa kama inawaka moto’’,alisema.

Kutokana na kutopata nafuu siku iliyofuata asubuhi  alipelekwa katika hospitali ya Rufaa ya misheni Peramiho ambapo madaktari walijitahidi kumuhudumia.
Beatrice kabla hajakatwa miguu

Hata hivyo anasema maumivu ya miguu yaliendelea huku miguu ikianza kuvimba na kuwa na rangi nyeusi na kutoa malengelenge ambayo yanafanana na mtu aliyeungua moto ambapo madaktari walishauriana na kuamua kuichubua ngozi na kutibu kama vidonda.

Uchunguzi zaidi uliofanywa na madaktari  wa hospitali ya Peramiho ulibaini kuwa mguu mmoja uliharibika kabisa hivyo waliamua kuukata jirani ya goti hali iliyomsababishia kupata ulemavu kwa kubakiwa na mguu moja ambao bado ulikuwa na kidonda ambacho kiliendelea kumsumbua.

Beatrice anadai kuwa madaktari hao walimweleza chanzo cha tatizo la miguu yake kuathirika lilitokana na athari za dawa ya SP na dripu la kwanini ambayo alikunywa na kutundukiwa kwa lengo la kutibu ugonjwa wa malaria.

Anasema kidonda ambacho kilikuwepo katika mguu mmoja kiliendelea kumsumbua kuanzia mwaka 2012 hadi 2014 na kumsababishia gharama kubwa ya nauli na matibabu ya kwenda Peramiho kila baada ya siku moja  madaktari walimtaka kufungia kidonda.

Kutokana na kushindwa kumudu gharama ndipo bibi yake aliamua kwenda kuomba msaada kwa mhasibu wa nyumba ya watawa wa kanisa katoliki wa Vincent Ruhuwiko mjini Songea Sr.Lea Haule ambaye alimsaidia nauli ya watu wawili na gharama za kufungia kidonda kila baada ya siku moja.

Hata hivyo Sr.Lea alimtafuta Sr Lucy ambaye anahusika na kitengo cha walemavu wa viungo mjini Mbinga mkoani Ruvuma ili aone uwezekano wa kumtengenezea mguu wa bandia Beatrice .

Hata hivyo Sr.Lucy mtaalam wa watu wenye ulemavu wa viungo alipomchunguzwa  kwa makini alibaini kuwa kumtengenezea mguu wa bandia bado haitasaidia kwa kuwa mguu wake mmoja aliubaini una matatizo makubwa ambayo yanatakiwa kwanza kufanyiwa uchunguzi  wa kudumu katika hospitali nyingine.

Hatimaye Sr.Lucy mwezi Julai 2014 alimsaidia Beatrice na mtu wa kumuuguza nauli na fedha za matibabu na matumizi kwenda katika hospitali ya misheni ya Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe ambayo inatajwa kuwa na madaktari bingwa wa matatizo ya viungo vya binadamu ambako aliweza kutibiwa baada ya kukatwa mguu wake wa pili.

Hata hivyo anasema ndoto zake za kusomea uhasibu zimeyeyuka kwa kuwa kutokana na ulemavu alionao hawezi tena kuwa mhasibu badala yake hivi sasa anapenda kujifunza lugha ya  kiingereza ,kusomea kompyuta pamoja na kujifunza ufundi wa kushona nguo na kudalizi vitambaa.

“Ndoto zangu hivi sasa ni kufungua kiwanda cha ushonaji kwa kuanzia nikipata mashine mbili za kushonea nitaweza kujitegemea mwenyewe,nawaomba watanzania wanaoweza kunisaidia mashine hizo pamoja na misaada mingine nitashukuru kwa kuwa mimi tayari ni mlemavu nikiwezeshwa naweza’’,alisisitiza.

Beatrice ambaye ni yatima ndiye mtoto wa kwanza kuzaliwa  katika familia ya watoto tisa  anahitaji msaada wa hali na mali katika kipindi hiki ambacho hana ajira zaidi ya kutegemea misaada ya wahisani mbalimbali.

Hata hivyo anasema yeye pamoja na wadogo zake  hawana sehemu maalum ya kuishi,kwa sababu wamefadhiliwa katika nyumba moja katika eneo la Ruhuwiko na kwamba anatamani kuishi na kujitegemea ili aweze kuwalea wadogo zake ambao wanamtegemea.

Watu wenye ulemavu kama sehemu ya jamii ya Tanzania,ni watu muhimu na wanastahili kupata haki zao kama watu wengine wasiokuwa na ulemavu.



Kwa kutambua umuhimu huo, Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania lilipitisha rasmi Sheria namba 9 ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010. Adhima kuu ya sheria hii ni kutoa haki na fursa mbalimbali kwa watu wenye ulemavu. Pia inakataza aina zote za ubaguzi dhidi yao.



Kwa mujibu wa sheria hiyo mwenye ulemavu ana Haki ya kutambuliwa na kuheshimiwa, Haki ya  kuwezeshwa na kuwekewa miundombinu ya kuyafikia na kuyatumia majengo ya umma,Haki ya kupata nyenzo za kujimudu mfano, fimbo nyeupe kwa wasioona, kiti cha magurudumu matatu kwa wenye ulemavu wa viungo na Haki ya kufanya kazi na kupata ajira.



No comments:

Post a Comment