Na
Albano Midelo
VISIWA viwili vya Mbambabay na Lundo katika ziwa Nyasa
mkoani Ruvuma ambavyo viliuzwa kinyume cha sheria kwa mwekezaji kutoka nje ya
nchi kati ya mwaka 2004 na 2005 vimerejeshwa serikalini.
![]() |
| Kisiwa cha Lundo ambacho kiliuzwa kimerejeshwa serikalini |
Mwandishi wa makala haya mwaka 2014 na 2015 aliandika kuhusu uuzaji wa visiwa hivyo kinyume cha sheria kwenye mitandao ya kijamii pamoja na gazetini.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Jabir Shekimweri alisema viongozi wa vijiji
waliuza visiwa hivyo kwa malipo ya shilingi kati ya milioni nne hadi tano na
kwamba baada ya kubaini kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria
uongozi wa Halmashauri ulimwita
mwekezaji huyo ambaye alikiri kununua
visiwa hivyo kinyume cha sheria.
Awali mwekezaji huyo
akiwa na mwanasheria wake alidai kuwa amenunua visiwa hivyo kwa mikataba halali
na viongozi wa vijiji hata hivyo mwishone ilibainika kuwa sheria haimruhusu
mwezezaji kumilikishwa visiwa.
Afisa ardhi wa
Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Christopher Komba ambaye pia ni mwanasheria
anabainisha kuwa Halmashauri ya kijiji cha Mbambabay iliuza kisiwa cha Zambia
kilichopo katika kijiji hicho na Halmashauri ya kijiji cha Lundo iliuza kisiwa
cha Lundo kati ya mwaka 2004 na 2005.
“Viongozi hao waliuza
visiwa hivyo kwa mzungu mmoja aliyefahamika kwa jina la John Tinny ambaye
alilipa kati ya shilingi milioni tano na kila mwaka alikuwa analipa kodi lakini
baadaye baada ya Halmashauri ya Mbinga kugawanywa kuwa na Halmashauri ya Nyasa
ndipo ufuatiliaji wa kina ulifanyika na serikali kufanikiwa kuvirejesha visiwa
hivyo’’,alisisitiza Komba.
![]() |
| Kisiwa cha Zambia kilichopo Mbambabay ambacho kiliuzwa |
Kwa mujibu wa Komba
visiwa hivyo vipo katika maeneo nyeti ambayo kimsingi hairuhusiwi kumilikishwa na kwamba visiwa vinasimamiwa na mamlaka
nyingine na sio Halmashauri ya vijiji kwa mujibu wa sera ya Taifa ya ardhi ya
mwaka 1995,sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 pamoja na sheria ya
uvuvi.
Akizungumzia kodi
ambayo alikuwa anadai analipa mwekezaji huyo katika Halmashauri ya kijiji kila
mwaka,Komba amebainisha kuwa mwekezaji huyo kulipa kodi hiyo alikuwa anafanya
makosa kwa kuwa kodi hiyo ilitakiwa kupangwa na waziri wa ardhi na maendeleo ya
makazi na sio Halmashauri ya kijiji kwa kuwa kisiwa sio sehemu ya kijiji.
Diwani wa kata ya
Lipingo Cathbert Ngwata ambaye kisiwa hicho kipo katika kata yake amekiri
Kisiwa maarufu kilichopo mpakani mwa vijiji vya Lundo na Ngindo kiliuzwa kwa raia mmoja wa
kigeni kinyume cha sheria za nchi.
Michael Milinga afisa
mtendaji wa kata ya Lipingo yenye vijiji vitatu ambavyo ni Ngindo,Lundo na
Lipingo anasema kisiwa hicho kina maliasili za kuvutia zikiwemo
wanyama,ndege,wadudu pamoja na mimea ya aina mbalimbali.
Kwa mujibu wa afisa
mtendaji huyo toka ufukweni hadi ndani
ya kisiwa hicho ni mwendo wa nusu saa kwa mtumbwi na kwamba raia huyo wa kigeni
ambaye aliuziwa kisiwa hicho aliwatumia viongozi wenyeji wa vijiji kuendesha
mchakato mzima wa kuuziwa kisiwa hicho.
“kuna raia mmoja wa kigeni
alifika kuomba kumilikishwa kisiwa cha Lundo ili aweze kuwekeza mwanzoni
makubaliano na uongozi wa kijiji ilikuwa anafanya malipo katika kijiji kwa
miaka mitano na baadaye aliomba kwa miaka kumi’’,alidai Milinga.
Uchunguzi unaonesha kuwa baadhi ya viongozi wa
vijiji waliingia mkataba wa kumuuzia
raia wa kigeni kisiwa hicho bila kuwashirikisha wananchi wote licha ya kwamba
kisiwa hicho sio sehemu ya kijiji kwa kuwa kipo ndani ya ziwa Nyasa.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wameipongeza
hatua ya uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa kumnyang’anya visiwa hivyo
mwekezaji na kwamba tangu awali walikuwa hawaungi mkono hatua ya viongozi wao
wa vijiji kumuuzia mgeni kisiwa hicho kwa kuwa kina manufaa makubwa kwa wavuvi
ambao wamekuwa wanakitumia kupumzika na
kujihifadhi ziwa linapokuwa na dhoroba kali.
“Iwapo raia huyo wa
kigeni angemilikishwa kisiwa hicho angeweza kuweka masharti magumu yakiwemo
kutoruhusu sisi wavuvi kupumzika katika eneo hilo la kisiwa hali ambayo ingehatarisha
maisha yetu kwa sababu ziwa Nyasa ni moja ya maziwa yenye dhoruba
kali’’,alisisitiza mvuvi John Challe. .
Kisiwa hicho kinachokadiriwa
kuwa na ekari kati ya 60 hadi 70 kinadaiwa kuanza
mchakato wa kuuzwa tangu mwaka 2004 na
kwamba mwekezaji anadaiwa mara baada ya
kununua kila mwezi alikuwa analipa
ushuru wa shilingi 400,000 katika kijiji cha Lundo.
![]() |
| Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Jabir Shekimweri |
Afisa maliasili wa Halmashauri
ya wilaya ya Nyasa Bugingo Bugingo anasema sheria za nchi haziruhusu mtu
binafsi kumilikishwa fukwe,mlima au kisiwa na kusisitiza kuwa ni kosa kubwa
kummilikisha mtu binafsi na hasa raia wa kigeni eneo ambalo linatambulika
kisheria kuwa ni hifadhi.
“kulingana na sheria za
Tanzania kisiwa chochote kilichopo ndani ya bahari au ziwa hairuhusiwi
kummilikisha mtu yeyote ispokuwa sheria inaruhusu kuwekeza’’,anasisitiza mtaalam
huyo wa mazingira.
Dk.Rugemeleza Nshala
ni mwanasheria na mkurugenzi wa chama
cha wanasheria watetezi wa mazingira Tanzania (LEAT) anabainisha kuwa kisheria
mtu binafsi anaruhusiwa kumiliki ardhi lakini haruhusiwi kumiliki visiwa
vidogo,fukwe,vilele vya milima,kingo za mito,maeneo yote oevu au chepechepe
pamoja na njia za asili za wanyamapori.
Hata hivyo amesema
watu ambao tayari wametwaa fukwe na visiwa na kuwazuia watu wengine au
kuwalipisha pesa wanakiuka kanuni ya msingi ya matumizi ya raslimali za pamoja
na kwamba ni jukumu la kila mwananchi
kupinga kubinafsishwa kwa visiwa au fukwe ambazo ni zawadi tuliopewa na Mungu.
Mbunge wa jimbo la
Nyasa Injinia Stella Manyanya ambaye pia ni Naibu waziri wa
elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi, ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya
utalii mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kuwa
wanayalinda maeneo yote yaliohifadhiwa hasa mwambao mwa ziwa Nyasa ambako kuna
rasilimali muhimu zinazoweza kufungua sekta ya utalii.
Tangu serikali ilipotangaza kufunguliwa kwa
Mtwara korido pamoja na kutangazwa kwa wilaya ya Nyasa
wawekezaji wengi wamekuwa wanajitokeza kutafuta maeneo ya uwekezaji
mwambao mwa ziwa Nyasa huku baadhi yao wakipata maeneo kwa njia haramu ikiwemo kuwatumia viongozi wa vijiji bila kuwahusisha wananchi.
Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi
tatu ambazo ni Tanzania,Malawi na Msumbiji.Ziwa hilo lipo kwenye usawa wa meta
500 toka usawa wa bahari kina cha ziwa hilo ni karibu meta 750,urefu wake ni
karibu kilometa 1000.
albano.midelo@gmail.com,simu 0763885442



No comments:
Post a Comment