NA KWIRINUS
MAPUNDA,NYASA
MWENYE ulemavu wa viungo Vikta Komba(Zambia)
ambaye Halmashauri ya Mbinga mkoa wa Ruvuma imeshindwa kumlipa deni lake la
sh.milioni 10 anadai anatarajia kuomba kibali cha kuuza moja ya figo zake ili
kukabiliana na matatizo yanayomkabili.
| Zambia akionesha nyumba yake ambayo imeanguka |
Zambia hivi sasa anaishi katika
umasikini mkubwa katika kijiji cha Nkali kata ya Liuli wilayani Nyasa mkoani
Ruvuma baada ya mradi wake wa kuotesha
miche kukwama kwa kile ambacho amedai Halmashauri ya wilaya ya Mbinga
kushindwa
kumlipa deni lake tangu mwaka 2011.
“Mradi wangu wa kuotesha miche ya miti
mbalimbali hivi sasa umekufa, kwa miaka
mingi niliweza kuotesha miche na kuuza katika maeneo mbalimbali ikiwemo ofisi
za serikali,shule,taasisi za kidini na watu binafsi,sasa nimebakia kuwa
masikini kutokana na Halmshauri kushindwa kunimalizia pesa zangu za
mradi’’,alidai Komba.
Uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma unalalamikiwa kutokana na kudaiwa kushindwa kumlipa mwenye
ulemavu wa viungo Zambia zaidi ya sh. milioni 10 za makubaliano ya uoteshaji wa
miche 42,000 ya korosho.
Komba alibainisha kuwa baada ya kampuni
ya Brink Naturals Enterprises kuchukua eneo lake lenye ekari 12 katika kijiji
cha Nkali na kuharibu mazao yake baada ya kuidhinishwa na Halmashauri ya kijiji
cha Nkali.
“Niliamua kufungua kesi ya madai
mahakamani namba 72 ya mwaka 2007,hata hivyo niliamua kumaliza kesi nje ya
mahakama mwaka 2009 baada ya wadaiwa mwenyekiti wa kijiji cha Nkali,mkurugenzi
wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga na kampuni ya Brink Natural
Enterprises kukubali kutekeleza makubaliano nje ya mahakama yaliofanyika Machi
31,2009 ikiwemo kulipwa kifuta machozi cha shilingi milioni 4.5 ambazo nililipwa”,alisema.
| Zambia akiwa na familia yake |
Komba aliyataja makubaliano mengine
yaliyofanyika mwaka 2009 kuwa ni Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kumpatia kazi
ya uoteshaji wa miche ya korosho zaidi ya 42,000 katika kijiji cha
Nkali ambayo Halmashauri ilitakiwa kumlipa zaidi ya shilingi milioni 21 sawa na
kila mche wa korosho shilingi 500.
“Mkurugenzi aliniandikia barua ya
kukubali kunilipa malipo ya kuotesha miche ya korosho zaidi 42,000 yenye
thamani ya zaidi ya shilingi milioni 21 sawa na shilingi 500 kwa kila
mche,ingawa baadaye wamenilipa kwa bei ya shilingi 240 kwa kila mche
ambayo ni kinyume cha makubaliano hivyo kulipwa shilingi milioni 10 ambayo ni
nusu ya madai yangu’’,alidai Komba.
Hata hivyo Komba ambaye ni mwenye
ulemavu wa viungo anadai tangu mwaka 2009 makubaliano ya kulipwa kiasi
hicho cha fedha hayajatekelezwa hadi sasa ambapo anaidai Halmashauri ya wilaya
ya Mbinga zaidi ya shilingi milioni 10.
Alisema tatizo lake bado halijapatiwa
ufumbuzi hadi sasa na kumsababishia
matatizo makubwa ya kiuchumi katika familia yake ikiwemo kushindwa kukamilisha
ujenzi wa nyumba yake ambayo imeanza kuanguka na watoto wake wanashindwa kusoma
kwa sababu ameshindwa kuwalipia ada.
“Mradi wangu wa kuzalisha miche ya miti
zaidi ya 20,000 kila mwaka umekwama ,hivi sasa katika kitalu changu miche
inayozalishwa haizidi 1000,ninakabiliwa na madeni mengi,mimi ni mwenye ulemavu,nimeongezewa
ulemavu wa kisaikolojia, imefikia mahali malapa tunachangia katika familia naomba serikali inisaidie’’, alisisitiza.
Komba baba mwenye mke na watoto watano
licha ya ulemavu wa viungo alionao ni mkulima na mwanamzingira hodari katika
kijiji chake cha Nkali anadai kuwa kutokana na matatizo kuwa mengi anakusudia
kuuza moja ya figo katika mwili wake ili apate pesa ambazo zinaweza kutatua
matatizo lukuki yanayomkabili.
“Nimepania kwenda kuomba kibali cha
kuuza moja ya figo zangu ili niweze kupata fedha zinakazoniwezesha kutatua
matatizo yangu,sina namna nyingine,nyumba inaanguka, watoto wangu watatu
wanadaiwa ada ninaishi kwa shida kubwa,’’,alidai Komba.
Barua aliyoandikiwa mwenye ulemavu huyo
na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri
ya wilaya ya Mbinga Shaibu Nnunduma ambaye hivi sasa ni mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Mafinga imedai
kuwa malipo ya shilingi milioni 10 ambayo amelipwa mlalamikaji ndiyo
makubaliano halali ambayo wamelipwa waotesha miche ya korosho wote wilayani
Mbinga wakati huo hivyo Halmashauri haidaiwi na mlalamikaji Komba.
“Nakuomba Komba endelea kuheshimu
makubaliano yetu ya awali yaliofanyika Septemba 12,2011 ofisini kwangu kwenye
kikao ,makubaliano yetu yabaki vile vile usigeuke,unatakiwa kuwa na
msimamo ulio thabiti, ’’,imesisitiza
barua ya mkurugenzi huyo.
Mwenyekiti wa chama cha wenye
ulemavu wa viungo mkoa wa Ruvuma Samwel Mapunda amethibitisha kupata taarifa
za madai ya Zambia katika Halmashauri ya
Mbinga na kwamba chama hicho
kimejitahidi kuchukua hatua za kumsaidia mwanachama wao kwa hali na mali ili
aweze kupata haki yake yote,hata hivyo alidai kuwa tangu wakati huo hadi sasa
amelipwa sehemu tu ya madai yake.
No comments:
Post a Comment