Thursday, May 5, 2016

Maajabu ya Hifadhi ya Taifa Kitulo



 Kitulo ina ndege warukao hadi Ulaya

Na Albano Midelo

HIFADHI ya Taifa Kitulo ndilo eneo pekee Tanzania lenye ndege aina ya tandawala machaka(Denhams Bustard) wenye uwezo wa kuruka toka bara moja hadi jingine, wameweka makazi yao.


Hifadhi ya Taifa Kitulo inayopita katika mikoa ya Mbeya na Njombe  ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa mwaka 2005 ikijumuisha sehemu ya eneo la shamba la mifugo,msitu wa Livingstone na bonde la Numbi.

Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 442 ndani ya mwinuko wa kati ya mita 2100 hadi 3000,awali ilijulikana
kama Elton Plateau baada ya Mvumbuzi Fredirick Elton kupita eneo hili mnamo mwaka 1870. Mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo(FAO) lilichukua eneo hili kwa ajili ya ukulima wa ngano na ufugaji wa kondoo.

Kutokana na umuhimu wa eneo hili wadau mbalimbali wa mazingira walipendekeza eneo hili litangazwe kuwa hifadhi ya Taifa ili kulinda umaridadi wa maua,ndege na mimea adimu inayopatikana ndani ya eneo hili.

Dk.Ezekiel Dembe kaimu mkurugenzi wa mipango ya maendeleo na huduma za utalii anasisitiza kuwa ndege aina ya tandawili machaka hawapatikani sehemu nyingine yeyote hapa Tanzania,watalii na watafiti wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani wanafika katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo kwa ajili ya kuwaona ndege hawa ambao wanasafiri umbali mrefu wa kutoka bara moja kwenda bara jingine.

Anasema ndege  hao adimu wanapendwa na watalii wengi duniani  na kwamba hifadhi hiyo ndiyo eneo pekee  ambako ndege hao wanataga mayai na kuzaliana kwa wingi kabla ya kuruka na kwenda katika mabara mengine.

“Utafiti unaonesha kuwa kuna ndege aina ya tandawili machaka ambao waliwekwa alama walipokuwa katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo,ndege hao walionekana na alama zao katika hifadhi moja barani Australia,utafiti huu ndiyo uliothibitisha kuwa ndege aina hiyo wanasafiri kwa kuruka toka bara moja kwenda bara jingine’’,alisema mhifadhi huyo.

Hata hivyo alisema ndege hao wamekuwa na tabia katika msimu Fulani kuruka na kufika katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo kwa ajili ya kutaga mayai na kuangua vifaranga kutokana na mazingira ya hifadhi hiyo kuonekana kuwa ni mahali pekee duniani penye mazingira rafiki ndege hao kuzaliana hivyo mara baada ya kutaga mayai,kuangua vifaranga na ndege  kukua,wanaruka na kwenda katika mabara mengine duniani.

Utafiti umebaini kuwa Katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo  ndege wa aina ya abdims stock,denhams(tandawili machaka) na blue swallow ambao wametoka Afrika ya kaskazini,Afrika ya kusini,Australia na Ulaya  wanaitumia hifadhi ya Taifa ya Kitulo kama makazi yao katika misimu  tofauti.

Watalii wakiwa ndani ya hifadhi ya Taifa ya Kitulo wanaweza kuangalia ndege adimu  katika ziwa Zambwe na misitu,kuweka kambi kwa ajili ya malengo mbalimbali, utalii wa kutembea kwa miguu,kupanda farasi,michezo ya gofu na kukwea milima.

Licha ya ndege adimu waliopo,hifadhi ya Taifa ya Kitulo pia inasifika kwa kuwa na maua  mbalimbali zaidi ya aina 40 ambayo hayapatikani sehemu nyingine yeyote duniani ispokuwa katika hifadhi hiyo pekee na baadhi ya maeneo kusini mwa Tanzania.


Unapoingia katika hifadhi hiyo msimu wa maua kuchanua inakuwa kama vile unga umeanikwa katika miinuko ya hifadhi hiyo hali ambayo inaongeza mvuto kwa kila mmoja ambaye anakuwa amebahatika kuingia ndani ya hifadhi hiyo.

Kana kwamba haitoshi Hifadhi hii imebarikiwa na mwenyezi Mungu kwa kuwa na aina zaidi ya 350 za mimea jamii ya flora.Miongoni mwa mimea maarufu ndani ya hifadhi hii ni jamii ya viazi vya asili vinavyoitwa vikanda ambavyo hutumika kutengeneza chikanda ambavyo vinatajwa kuwa na bei kubwa katika nchi jirani ikiwemo Zambia na Zimbabwe.

Mhifadhi Godwel Ole Meing’ataki mratibu wa miradi, mipango ya maendeleo na uboreshaji huduma vivutio vya utalii kusini(SPANEST) anasema utafiti umebaini kuwa mimea aina ya vikanda vinavyopatikana ndani ya hifadhi ya Taifa ya Kituro vina soko kubwa katika nchi za Zambia na Zimbabwe ambapo debe moja la vikanda hivyo huuzwa kati ya shilingi 80,000 hadi 100,000.

Hata hivyo alisema kabla ya baadhi ya vijiji kuingizwa katika eneo la hifadhi wananchi wanaozunguka eneo hilo walikuwa wanaingia na kuchimba vikanda hivyo na kwamba hivi sasa hawaruhusiwi kuchimba viazi vya asili ndani ya hifadhi hiyo kwa kuwa eneo hilo limetengwa na kwamba kufanya shughuli zozote ndani ya hifadhi ni ujangili.

“Katika hifadhi nyingine kuna ujangili wa wanyamapori lakini ndani ya hifadhi ya Taifa ya Kitulo kuna ujangili wa  viazi vya asili (vikanda) ambavyo huchimbwa na kuuzwa katika nchi za nje kwa bei kubwa’’,alisema.

Yapo mengi ya kujivunia katika Hifadhi ya Taifa  ya Kitulo ukiwemo uwanda wa tambarare, mabonde,vilima na maporomoko ya maji kama Numbi ambapo ndani ya msitu kuna miti ya aina ya cidar yenye urefu wa zaidi ya mita 50 na inakadiriwa kuwa ndiyo miti mirefu kuliko yote duniani.

Hifadhi ya Taifa ya Kitulo inafikika kwa gari  kutoka Chimala,kilometa 78 Mashariki mwa mji wa Mbeya  unapanda milima yenye kona 68 ambazo pia ni kivutio hadi katika  mji wa Matamba wilayani Makete mkoa wa Njombe.

 Reli ya TAZARA hupita karibu na hifadhi ya Taifa ya kitulo.Pia unaweza kufika ndani ya hifadhi hiyo ukitokea Zambia kupitia Tunduma ni wastani wa kilometa 170 au Malawi kupitia wilaya ya Karonga mkoa wa Mzuzu kwa barabara ni wastani wa kilometa 135.

Kutokea jijini Dar es salaam  kupitia Makambako, Njombe,Makete hadi Kitulo ni wastani wa kilometa 963 na kutoka Dar es salaam,Chimala, Matamba hadi Kitulo ni wastani wa kilometa 836.

Huduma za hoteli na malazi zinapatikana kwa urahisi ambapo katika jiji la Mbeya kuna hoteli kadhaa zenye hadhi ya kitalii,pia katika mji wa Matamba ambao upo jirani na hifadhi hii kuna nyumba  za wageni. Hata hivyo kutokuwapo kwa juhudi za kutosha katika kuhamasisha wananchi kutembelea hifadhi hiyo kumechangia vivutio vingi vya utalii kutofahamika hata kwa baadhi ya wenyeji.



Uchunguzi umebaini kuwa  licha ya mkoa wa Njombe kuwa na vivutio adimu vya utalii ikiwemo hifadhi ya Taifa ya Kitulo bado wakazi wake hawana mwamko wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hali ambayo inachangia kutofahamika kwa vivutio hivyo.



Wananchi walio wengi wanadhani wanaostahili kutembelea vivutio hivyo ni watalii kutoka nje ya nchi pekee,ambapo baadhi yao hawajui vivutio vya utalii vilivyopo Njombe wakiamini kuwa fursa ya utalii ipo katika mikoa ya kuskazini pekee  na sio kusini.



Mkurugenzi mkuu wa shirika la  Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA Allan Kijazi akizungumzia hifadhi za Taifa kwa ujumla alisema hadi sasa shirika lake linasimamia hifadhi 16  za Taifa ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kukuza pato la Taifa.

Hata hivyo Kijazi amezitaja changamoto zinazozikabili hifadhi za Taifa kuwa ni pamoja na ujangili unaotokana na biashara za kujikimu,upungufu wa maji katika baadhi ya hifadhi wakati wa kiangazi,migogoro ya mipaka katika baadhi ya hifadhi na muingiliano kati ya wanyamapori na binadamu.

 Sekta ya utalii hapa nchini ni ya pili  katika kuchangia pato la Taifa ambayo inachangia asilimia 17.Sekta hiyo ni muhimu sio kwa Tanzania pekee bali  pia duniani kote kutokana na takwimu za kimataifa kuonyesha kuwa Mapato yatokanayo na utalii duniani yalifikia dola za Marekani milioni 919 mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment